ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, February 2, 2011

Tume kuchunguza kutupwa maiti za vichanga Mwananyamala.


KUFUATIA vifo vya vichanga 10 vilivyokutwa vimefukiwa katika shimo jirani na Hospitali ya Mwananyamala, jijini Dar es Salaam, jopo la wataalam mbalimbali limeundwa kwa ajili ya kuchunguza tukio hilo.


Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana alisema Serikali imeunda tume ya watu watano (5) kufanya uchunguzi wa chanzo cha tukio hilo ambayo itakamilisha uchunguzi huo ndani ya siku saba.

Alisema juzi jioni alipopata taarifa hizo alifika katika eneo la tukio na kukuta vichanga kumi vikiwa vimefukiwa katika shimo na kwamba walizaliwa wakiwa wamekufa.





“Ni kweli taarifa za awali tulizozipata ni kwamba watoto saba walikuwa hawajafikia hatua ya kuzaliwa na wengine watatu walikuwa wamefikisha wakati wa kuzaliwa na sasa tayari uchunguzi unaendelea, kubaini aliyesababisha kufukiwa kwa watoto hao katika shimo,”alisema Rugimbana.

“Hata kama viumbe hivyo vimekufa, ni lazima taratibu zifuatwe sio kufanya kitendo kile. Kweli kinasikitisha, kwa hiyo uchunguzi unaendelea muda sio mrefu jamii itapata majibu sahihi, tunaiomba jamii ivumilie wakati uchunguzi ukiendelea,”alisema Rugimbana.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Raphael Nduguru alisema kwa mazingira ya tukio hilo lazima uongozi wa Halmashauri ujiridhishe kwa kufanya uchunguzi wa kutosha na kubaini chanzo cha tukio hilo na kwamba kama kuna uzembe ulifanywa na baadhi ya watumishi wa hospitali ya Mwananyamala watachukuliwa hatua za kisheria.

“Kwa kawaida kuna taratibu za kumzika mtu mara baada ya kufariki sio kama ilivyotokea, hili ni tukio la kusikitisha kwa hiyo tunawaomba wananchi wawe na subira ili uchunguzi ufanyike na ukweli utajulikana,”alisema Ndunguru.

Hata hivyo, tayari wanaharakati wamepinga tume hiyo wakitaka isishirikishe mfanyakazi yeyote wa Manispaa ya Kinondoni.

Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali linalojishughulisha na utawala bora na afya la Sikika, Irenei Kirio alisema kuwa tume hiyo ni batili na kwamba isithubutu kufanya kazi yoyote.

"Tume iliyoundwa ni kiini macho kwa sababu ni watendaji wa manispaa hivyo watakuwa wanajichunguza wenyewe, ni walewale. Tunaomba tume huru isiyomhusisha mtendaji hata mmoja wa manispaa hiyo au hospitali ya Mwananyamala,"alisema Kirio.

Akizungumza katika mkutano uliowahusisha viongozi wa Manispaa ya Kinondoni na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Kinondoni, Charles Kenyela alisema mtu mmoja ametiwa mbaroni akidaiwa kuhusika na tukio hilo, huku uchunguzi ukiendelea kubaini chanzo chake.

Alisema kuwa kwa sasa upelelezi unaendelea kubaini watu wengine waliohusika katika tukio hilo.

“Kwa sasa tayari kuna mtu mmoja amekamatwa, anaendelea kuhojiwa na polisi wakati upelelezi wa kuwakamata wengine ukiendelea na baada ya hapo tutatoa taarifa za chanzo cha tukio hilo,”alisema Kenyela.

Alisema kuwa katika hatua ya uchunguzi zipo taarifa za wote waliojifungua watoto hao, ambapo alisema wataitwa na tume hiyo ili kuhojiwa na kujua ukweli.

"Kwa bahati nzuri anuani za wale wazazi wa vile vichanga tunazo, kwa hiyo tutawatafuta na watahojiwa ili kupata ukweli wa mambo yalivyokuwa," alisema Kenyela.

Hata hivyo, malumbano yalizuka baina ya wanahabari walioshuhudia tukio hilo awali na uongozi wa manispaa kuhusu watoto hao kufikia au kutofikia hatua ya kuzaliwa.

Kuzuka kwa malumbano hayo kulitokana na Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mwananyamala, Dk Sofinias Ngonyani kudai kuwa watoto saba kati ya kumi waliofukiwa walikuwa hawajafikia muda wa kuzaliwa bali mimba zilizotoka (abortion) na watatu pekee ndio waliofikia hatua ya kuzaliwa.

Kauli hiyo ilipingwa vikali na wanahabari walioshuhudia tukio hilo juzi na jana kuhudhuria mkutano huo wakisema mganga huyo anajaribu kuuhadaa umma.

“Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya kati ya waandishi walioshuhudia tukio hilo na kupiga picha, mimi ni miongoni mwa hao. Kama kuna ubishi tunaweza kuwaonyesha picha za watoto hao ili kupata uhakika wa suala hili maana walikuwa wamefikia muda wa kuzaliwa,” alisema mwanahabari Sam Mahela wa ITV mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni.
 
Source: Mwananchi.

No comments: