Tuesday, February 1, 2011

Mambo kumi yanayoweza kumfanya mwanaume akuache

Bila shaka u mzima wa afya mpendwa msomaji. Leo nimeandaa mada juu ya mambo kumi yanayoweza kukufanya mwanamke ukaachwa na mume/mpenzi wako. Twende pamoja...

1.KUWA MWIGIZAJI
Uigizaji unaozungumzwa hapa siyo wa filamu lakini ni ile hali ya kujitengenezea tabia ambazo siyo rasmi. Kwa mfano wewe ni masikini lakini unajifanya ni mtoto wa tajiri au wakati mwingine unaazima nguo za watu kwa lengo la kujiweka juu na tabia za kufanana na hizo. Ukiwa mwanamke uliyependwa, usithubutu kudanganya uhalisia wako kwa kitu chochote. Wanaume hawapendi kabisa tabia hiyo.


2.KUWA TEGEMEZI
Katika ulimwengu huu tunaoishi sasa, wanaume wengi hawapendi wanawake tegemezi. Katika hili uchunguzi umeonesha kuwa wanawake wenye kazi ni rahisi kuolewa kuliko wasiokuwa na kazi. Hii ina maana kwamba wanaume hawapendi kutegemewa kwa kila kitu na inapotokea hali hiyo ni rahisi kwao kubwaga manyanga na kutafuta penye unafuu. Kamwe usikubali kuwa mwanamke wa ‘nitumie vocha’, ‘naomba hiki’, ‘naomba kile’ kila siku, utaachwa.

3. USIKIVU
Ingawa tafiti zinaonesha kuwa wanawake huzungumza zaidi kuliko wanaume, ukweli unabaki kuwa wanaume hutaka kusikilizwa katika machache wanayosema au kuagiza. Endapo mwanaume atakuwa akisema jambo fulani na mwanamke haoneshi usikivu, ni rahisi kwake kufikiria kuwa anadharauliwa na hivyo kuamua kuachana na mwanamke huyo. Kwa mantiki hiyo, wanawake wanatakiwa kuwa wasikivu kwa wanaume vinginevyo watajiweka katika mazingira ya kuachwa.

4.MATUMIZI MAKUBWA
Inawezekana jambo hili linasababishwa na ugumu wa maisha ambao umewafanya wanaume wengi kubana matumizi. Inapotokea mwanamke akawa na matumizi makubwa ya fedha na vitu, humkera mumewe/mpenzi wake. Ewe dada/ mwanamke, katika kulinda uhusiano wako jitahidi kuhakikisha kuwa matumizi yako yanakuwa ya chini kuanzia mnapotoka ‘out’ na mumeo mpaka kwenye fedha za matumizi ya nyumbani unazoachiwa.

5. UBINAFSI
Maisha ya mapenzi yanataka umoja. Wanaume wanaamini sana kwenye hili hivyo wanapoona wenza wao wamekuwa wabinafsi katika mafanikio au mipango yao ya kimaisha, huingiwa na wasiwasi na kuhisi kuwa hawapendwi. Ikifikia hatua hii, huamua kujitoa kama njia ya kujihami au kutetea uanaume wao.

6. KUMTAFSIRI
Wanawake wengi wamekuwa na tabia ya kuwatafsiri wanaume kadiri wajuavyo wao bila umakini: “Nilijua uliposema hivyo ulitaka niondoke.”

Wanaume huamini kuwa wao ni walimu hivyo linapotokea suala la mwanamke kushindwa kuelewa na kutafsiri maneno kinyume na lengo la mhusika, hujiweka kwenye kundi baya la uelewa mdogo na hivyo kujiongezea hatari ya kuachwa. Unapokuwa kwenye mazungumzo na mumeo, usimtafsiri na endapo hilo litatokea basi jitahidi kutafsiri kwa usahihi kile alichokiongea.

7. KULAZIMISHA VITU
Uchunguzi unaonesha kuwa, wanaume hawapendi kulazimishwa kufanya mambo na inapotokea mwanamke akaweka msukumo mkubwa wa kuhakikisha mwanaume anatekeleza kitu fulani (bila kujali umuhimu wa jambo lenyewe), ulazima huo hugeuka kuwa kero inayoweza kumfanya apoteze penzi lake. Ushauri kwa wanawake ni kwamba hata kama jambo fulani lina umuhimu, wasiweke lazima yenye kukera.

8. KUTENDA KINYUME
“Naomba pesa hii uiweke, ikifika elfu kumi tutanunua unga.” Litakuwa jambo la ajabu na lenye kuvunja moyo kama mwanaume ataagiza hivi halafu akakuta baadaye mwanamke kazitumia zile pesa kununulia nyama kwa hoja kwamba walikuja wageni. Wanaume hupenda wanawake wafanye sawa na walivyoagiza na linapotokea jambo la kubadilisha basi waulizwe kwanza.

9. KUTOJIAMINI
Mitindo ya wanawake kuwafuata fuata wanaume kwa kupekua simu zao na mitandao yao kwa lengo la kujihami na usaliti ni jambo linalowaudhi wanaume wengi. Uchunguzi unaonyesha kuwa wanaume wanapenda kuwa huru na kuheshimiwa siri zao kuanzia mishahara na hata nyendo zao na marafiki zao wakiwemo wa kike.

Hali ya kuwauliza na kuwabana wanakopita walikuwa na nani huondoa mshawasha wao wa kimapenzi na kujikuta wakiamua kuutafuta uhuru wao kwa kuachana na kero hiyo ya kufuatiliwa kupita kiasi. Ukiwa kama mwanamke, jiamini na uache mumeo ajichunge mwenyewe. Gubu la kujilinda halifai kabisa.

10. KUMGEUZA KITABIA
Licha ya kuwa wanawake wana jukumu la kuhakikisha wenza wao wanaishi katika njia sahihi, wanaume hawapendi kubadilishwa tabia kwa nguvu. “Kwa nini umekunywa pombe? Si nilikukataza? Leo utalala chini.” Njia hii ya kumgeuza tabia mwanaume kwa lazima haifai na inaweza kusababisha akuache. Nenda pole pole ukiamini kubadili tabia siyo kitu cha siku moja.

No comments: