ANGALIA LIVE NEWS

Monday, February 28, 2011

Milipuko ya mobomu yazua kihoro vijijini

  Wakumbuka ya Mbagala, Gongo la Mboto
  Ni mirindimo ya ulipuaji mabomu kikosini
  Uthamini Dar wakwama, kazi bado nzito
Moja ya bomu lililodondoka kwenye moja ya nyumba katika milipuko ya mabomu iliyotokea katika kambi ya Gongo la Mboto na Mbagala, mkoani Dar es Salaam.

Hofu imetanda katika vijiji kadhaa vilivyopo jirani na mji wa Shinyanga kufuatia Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kuendesha zoezi la ulipuaji wa mabomu.
Wananchi wa vijiji hivyo walikumbwa na hofu hiyo tangu mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya kusikika kwa milio ya mabomu iliyokuwa ikitoka katika kambi ya JWTZ ya Kizumbi iliyopo nje kidogo ya mji wa Shinyanga.

Vijiji vilivyokumbwa na hofu hiyo ni Kuzumbi, Nyeregani, Kitangiri, Buhangisha, Ibingamata na baadhi ya maeneo ya Manispaa wa Shinyanga.
Mmoja wa wananchi waliokumbwa na hofu hiyo, Masumbuko Masunga, alisema wananchi hao walikimbia makazi yao kuhofia kupigwa na mabomu kama ilivyotokea katika kambi ya Gongo la Mboto na Mbagala, mkoani Dar es Salaam.
Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga lilithibitisha kuwepo kwa zoezi hilo, lakini likasema JWTZ walikwisha kutoa taarifa kwa viongozi wa vijiji hivyo kuwa watalipua mabomu kuanzia Ijumaa iliyopita hadi leo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Diwani Athumani, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo, lakini akawataka wananchi kuondoa hofu kwa kuwa ulipuaji huo unafanywa kwa utalaamu wa hali ya juu.
Alisema ulipuaji huo haujasababisha madhara yoyote kwa kuwa mabomu yalikuwa yanaelekezwa katika maeneo ambayo hayakaliwi na watu.
UTHAMINI DAR WAKWAMA
Kazi ya kuthamini hasara ya nyumba zilizobomoka kufuatia milipuko ya mabomu, katika ghala la kuhifadhi silaha kwenye kambi ya JWTZ Gongo la Mboto, jijini Dar es Salaam, Februari 16, 2011, imekwama kuanza leo kama ilivyotarajiwa.
Habari zinasema kuwa kukwama huko kunatokana na uzito wa kazi ya uhakiki, kwani nyumba zote zilizoathirika hazikuwa zimefikiwa zote hadi jana.
Kutokana na tukio hilo, watu 26 waliripotiwa kufariki dunia, wengine zaidi ya 500 kujeruhiwa, nyumba zaidi ya 75 zenye familia 115 kuharibika na mali nyingine zenye thamani ya mamilioni ya shilingi kupotea na wengine kuyakimbia makazi yao.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki, alikaririwa akisema kazi ya kuhakiki nyumba zilizobomoka ingekamilika jana na kutoa fursa kwa kazi uthamini wa hasara za nyumba hizo kuanza rasmi leo. Hata hivyo, akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu Tawala Msaidizi Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo, Eliya Ntandu, alisema kazi ya uthamini wa nyumba hizo imeshindikana kuanza leo.
Alisema hali hiyo imetokana na kazi ya kuhakiki nyumba hizo kuwa kubwa, kinyume cha walivyotarajia.
“Tulitarajia uthamini uanze kesho (leo), lakini matarajio na hali halisi vimekuwa tofauti kabisa. Kazi ya kuhakiki imekuwa kubwa, kinyume cha tulivyotarajia,” alisema Ntandu.
Alitoa mfano wa Kata ya Majohe, eneo ambalo limeathirika zaidi na tukio hilo, hadi kufikia juzi, kamati ya kuhakiki ilikuwa haijamaliza kazi hiyo katika nyumba zilizoko katika mtaa mmoja. Kata hiyo ina mitaa saba.
Hata hivyo, alisema kamati hiyo imekwishamaliza uhakiki wa nyumba zilizoko katika maeneo ya Kwembe, Saranga, Kibamba na Mbezi wilayani Kinondoni.
Alisema mbali na nyumba hizo, pia shule nane za serikali na moja ya binafsi zilizoko katika kata 12, wilayani Ilala, zimeathirika.
Shule hizo ni Amani, Maarifa, Juhudi, Kajiungeni, Majohe, Gongo la Mboto, Bangulo na Pugu (za serikali) na Liku (ya binafsi).
MAJERUHI MWINGINE ADAIWA KUFARIKI
Katika hatua nyingine, Mbunge wa Ukonga (CCM), Eugen Mwaiposa, alisema jana kuwa alipokea taarifa za kufariki dunia kwa majeruhi mwingine wa tukio hilo, mkazi wa Pugu, aliyemtaja kwa jina la Salma Abdallah.
Ntandu alipoulizwa na waandishi wa habari, alithibitisha kamati ya maafa kupokea taarifa za kifo hicho.
Alisema aliielekeza Hospitali ya Amana kwenda kuchukua mwili wa mtu huyo ili ufanyiwe uchunguzi kuthibitisha kama kifo chake kina uhusiano wowote na tukio hilo au la.
Alisema taarifa walizopata jana, zilidai kuwa mtu huyo alifariki jana alfajiri baada ya kuruhusiwa kutoka Hospitali ya Amana alikokuwa amelazwa baada ya kupata majeraha katika tukio hilo.
Kifo hicho sasa kitafanya idadi ya watu waliokufa kutokana na milipuko hiyo kufikia 27 iwapo uchunguzi utathibitisha kuwa kifo chake kina uhusiano na tukio hilo.
Ntandu pia alisema kufikia jana, idadi ya majeruhi wa tukio hilo waliolazwa hospitali, walikuwa wamebaki watu 23.
Alisema kati yao, mmoja amelazwa katika Hospitali ya Amana, 11 Muhimbili (MNH) na wengine 11 katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa (Moi) Muhimbili.
MISAADA ZAIDI YAPOKELEWA
Wakati hayo yakijiri, misaada ya kibinadamu kwa waathirika wa tukio hilo, jana imezidi kumiminika, baada ya wasamaria wema zaidi kuwasilisha misaada hiyo kwa Kamati ya Maafa ya Mkoa wa Dar es Salaam jana.
Waliowasilisha misaada hiyo inayojumuisha vyakula, maji, nguo, viatu, busati, mashuka na sabuni, ni Kanisa Katoliki St. Immaculata Upanga na Jumuiya ya Immaculata; Redio Sauti ya Qur’an na Jumuiya ya Watuma Salamu wa Redio hiyo.
Wengine ni kampuni ya Super Sippy Limited; Youth United Nations of Associations of Tanzania; Suzana Rengo; Uhuru One na Devotha Joseph wa Kurasini, jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maafa ya Redio Sauti ya Qur’an, Shamim Khan, alisema misaada waliyoitoa jana, ni ya awali na kwamba, wataendelea kutoa misaada zaidi kwa waathirika kwa miezi sita zaidi na kwamba, ikibidi watafanya hivyo zaidi kutokana na kuguswa na janga lililowapata watu hao.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, leo anatarajiwa kupokea msaada kwa ajili ya waathirika hao kutoka kwa Balozi wa Urusi nchini.
WALIOPIGA RAIA HAWAJAkAMATWA
Jeshi la Polisi mkoa wa kipolisi Ilala, limesema halijakamata kikundi cha watu waliowapiga wakazi wa Gongo la Mboto usiku wa kuamkia Ijumaa iliyopita.
Kaimu Kamanda wa mkoa huo, Sara Juma, aliliambia NIPASHE jana kuwa, bado hawajafanikiwa kuwakamata watuhumiwa wa tukio hilo.
Sara alisema upelekezi wa tukio hilo unaendelea. Siku ya tukio ilidaiwa kuwa, kikundi hicho kiliingia mtaani majira ya saa 6:00 usiku eneo la Gongo la Mboto stendi ya daladala na kuanza kuwapiga walinzi pamoja na wauza chips waliokuwepo hapo.
Aidha, katika tukio hilo, watu wanane walijeruhiwa sehemu mbalimbali mwilini wa walitoa taarifa polisi juu ya tukio hilo.
Baadhi ya wananchi hao walisema kuwa walivamiwa na kikundi cha watu wapatao 30 waliokuwa wamevaa sare za jeshi na kuanza kuwashambulia kwa kuwapiga na mikanda ya sare zao pamoja na fimbo zilizofanana na nyaya za umeme.
Imeandikwa na Muhibu Said, Romana Mallya (Dar) na Ancenth Nyahore (Shinyanga).
CHANZO: NIPASHE

No comments: