Mbwana Samatta alifunga 'hat-trick' yake ya kwanza tangu aanze kuichezea Simba msimu huu na Amri Kiemba akaongeza jingine wakati Simba iliporejea kwa kishindo kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Bara kwa ushindi wa 4-1 dhidi ya Mtibwa Sugar ya Manungu kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam jana.
Samatta aliye katika kiwango chake cha juu aliifungia Simba goli la utangulizi katika dakika ya 13 kwa shuti la karibu na lango baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa Amri Kiemba.
Katika dakika ya 46, Kiemba aliifungia Simba goli la pili baada ya kuunganisha wavuni kwa kichwa kona iliyopigwa na Rashid Gumbo na Hussein Javu aliifungia Mtibwa goli lao la pekee katika dakika ya 55 kufuatia kazi nzuri ya Salum Machaku, aliyemtoka beki Juma Nyosso kabla ya kumpasia mfungaji.
Shija Mkina alipiga krosi safi katika dakika ya 66 na kumkuta Samatta aliyepiga shuti lililokwenda moja kwa moja wavuni baada ya kumshinda kipa wa Mtibwa Soud Slim aliyeruka bila mafanikio.
Samatta alifunga goli lake la tatu na la nne kwa Simba kwa njia ya penati katika dakika ya 90 baada ya kipa Slim kumuangusha Mussa Hassan 'Mgosi' ambaye aliwalamba chenga mabeki wawili wa Mtibwa na kujaribu kumpiga kanzu kipa huyo.
Awali Simba walikaribia kuhesabu goli la kwanza katika dakika ya tatu wakati Amri Kiemba alipofunga lakini refa Amon Paul kutoka Mara alilikataa kwa kuwa kipa Omary Ally wa Mtibwa alikuwa ameumia kabla ya mfungaji kutumbukiza mpira kimiani. Kipa Omari alitoka na nafasi yake kuchukuliwa na Slim.
Katika mechi hiyo, kipa chaguo la kwanza wa Simba na timu ya taifa, Juma Kaseja aliachwa benchi kwa mara nyingine msimu huu na Ally Mustafa 'Barthez' alisimama katikati ya milingoti miwili ya wana Msimbazi.
Kabla ya kuanza kwa mechi hiyo iliyohudhuriwa na mamia ya mashabiki, mjumbe wa kamati ya utendaji ya Simba, Swedi Nkwabi aliripotiwa kupelekwa kwenye Kituo cha Polisi Chang'ombe kwa tuhuma za kumtolea bastola mlinzi wa mlangoni baada ya kuulizwa tiketi wakati akitaka kuingia uwanjani. Hata hivyo, hakukuwa na taarifa za kipolisi kuthibitisha ripoti hiyo.
Simba sasa imefikisha pointi 37, mbili juu ya Azam na Yanga wanaofuatia katika nafasi ya pili na ya tatu, lakini Azam wakicheza mechi moja zaidi ya wapinzani wake.
Ligi hiyo inaendelea tena leo kwa mechi moja wakati Yanga watakapokuwa wageni wa Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
CHANZO: NIPASHE
i