Masimango na juhudi za kutaka kunusuru ndoa vimekuwa ndoano kwa mwanakamke, Neema Nestory (25), ambaye aliiba kichanga ili kuepuka adha hiyo, lakini sasa amekamatwa na yuko mikononi mwa polisi akisubiri sheria ichukue mkondo wake.
Hali hii imebainika baada ya wanakijiji wa kijiji cha Kisaba katika kisiwa cha kata ya Meisome ziwani Victoria wilayani Sengerema, mkoa wa Mwanza, kumkamata Neema kisha kumkabidhi kwa Jeshi la Polisi baada ya kumkamata na kichanga cha mwezi mmoja aliyemuiba kutoka kwa mama yake mzazi, Tatu Matunda (19).
Tukio hilo lilitokea juzi katika kijiji cha Kisaba baada ya Tatu kufika kijijini hapo kwa lengo la kumtafuta mtu aliyeiba mtoto wake baada ya kupewa taarifa na wasamaria wema kwa njia ya simu.
Akizungumzia tukio hilo, Tatu alidai kuwa alikutana na mtuhumiwa katika kijiji cha Buselesele sokoni wilayani Chato, Mkoa wa Kagera na kujifanya wanafahamiana na ndipo alipomuomba kumbeba mtoto huyo na kumkubalia.
Alisema baadaye aliongozana na mtuhumiwa hadi nyumbani kwa dada yake alipokuwa anaishi mlalamikaji na walipofika alimuomba akanunue vocha kwa ajili ya kuongeza salio kwenye simu yake na kuondoka na mtoto, lakini hakurejea.
Tatu alitoa taarifa katika kituo cha polisi cha Buselesele wilayani Sengerema na kuanza kumtafuta bila mafanikio.
Tatu alisimulia kuwa tukio hilo lilitokea Januari 3, mwaka huu saa 4:00 asubuhi na kwamba tangu wakati huo alikuwa anamtafuta mtoto wake hadi juzi. Alisema juzi saa 11:00 alfajiri ndipo walipofanikiwa kumkamata Neema akiwa na kichanga hicho katika kambi ya wavuvi ya Bugombe alikokuwa anaishi na mumewe.
Tatu alisema kuwa baada ya kukamatwa, Neema alikiri na kumuonyesha mtoto huyo na kujitetea kuwa aliiba kichanga hicho kwa lengo la kunusuru ndoa yake baada ya kuishi zaidi ya miaka kumi na mumewe bila kupata mtoto.
Alisema kuwa Neema alisema kutopata mtoto kulikuwa kunahatarisha ndoa yake.
Inadaiwa kuwa mtuhumiwa huyo mwezi mmoja kabla ya kurejea kutoka kwao wilayani Chato, alimwambia mumewe kwamba alikuwa na ujauzito na kwamba alikuwa anataka kwenda kujifungulia kwao hivyo mumewe alimkubalia na baada ya mwezi mmoja alirejea akiwa na kichanga hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na tukio hilo jana, Diwani wa Kata ya Meisome, Mtazania Mazabari, alisema kuwa mtuhumiwa alitiwa mbaroni kwa ushirikiano wa wanakijiji juzi alfajiri katika kambi ya Bugombe kisiwani humo.
Aliongeza kuwa baada ya kutiwa mbaroni, Neema alikiri kumuiba mtoto huyo na kisha kuomba asamehewe, kitendo kilichokataliwa na wanakijiji na mlalamikaji na kisha kumkabidhi katika kituo cha polisi cha Bupandwa jana asubuhi.
Mazabari aliongeza kuwa wakati anakamatwa mtuhumiwa, mume wake aliyemtaja kwa jina la Joramu Msuasa, hakuwepo ingawa wote wamekuwa wanaishi katika kambi la uvuvi katika kijiji cha Kisaba kwenye kisiwa cha Meisome. Diwani huyo alimtaja mtoto aliyekuwa ameibiwa kuwa ni Saada Masunga na kuwa alipatikana akiwa na hali nzuri.
Afisa Mtendaji wa kata hiyo, Cliford Maulubi, alisema kuwa tayari wamemkabidhi mtuhumiwa kwenye kituo cha polisi cha Bupandwa.
Polisi wa kituo hicho wamethibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kwamba hatua za kisheria zimeanza kuchukuliwa.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Simon Sirro, hakupatikana jana kuzungumzia tukio hilo kutokana na simu yake kufungwa.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment