ANGALIA LIVE NEWS

Monday, February 28, 2011

Mama Maria Nyerere ateta na Chadema

FEB 28,2011
Mama Maria Nyerere akiteta jambo na katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willbrod Slaa, wakati viongozi wa Chama hicho na baadhi ya wabunge, walipomtembelea nyumbani kwake Butiama jana.

Viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), jana walimtembelea mjane wa Baba wa Taifa, Maria Nyerere, na kuzuru kaburi la Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere.
Baada ya kuteta na Mama Maria nyumbani kwao katika kitongoji cha Mwitongo, kijijini Butiama, mkoani Mara, viongozi hao wa juu wa Chadema, wabunge wake na viongozi wengine, walikwenda katika kaburi la Mwalimu Nyerere na kusali sala fupi kisha kuweka mashada ya maua katika kaburi hilo. Akizungumza na viongozi hao, Mama Nyerere alivitaka vyama vya siasa kushirikiana katika kulijenga taifa la Tanzania, ambalo bado linahitaji umoja.

Mama Maria alisema kuwa vyama vyote vya siasa vina lengo la kujenga nchi, hivyo hakuna haja ya kupigana kwa sababu ya vyama kwani kwake yeye vyama vyote vya siasa ni sawa na haoni kama kuna tofauti. “Mimi ni mama wa taifa hivyo vyama vyote kwangu ni sawa, hakuna tofauti kwani wote ni wamoja,” alisema Mama Maria Nyerere.
Pia, aliwapongeza Chadema kumtembelea na kuzuru kaburi la muasisi aliyelipatia uhuru taifa. Naye msemaji wa familia hiyo, Magige Kambarage, mtoto wa tatu wa Mwalimu Nyerere, alisema kuwa maandamano yanayofanywa na Chadema ni ishara kubwa kuwa chama hicho kinazidi kupendwa na wananchi, hasa kutokana na maandamano yao yanavyoitikiwa na maelfu ya wananchi kila yanapoitishwa.
Juzi, Chadema kiliitisha maandamano ya amani mjini Musoma na kukusanya maelfu ya watu walioandamana na baadaye kufanya mkutano mkubwa katika viwanja vya Shule ya Msingi Mkendo.
Akizungumzia kuhusu uchache wa wapiga kura waliojitokeza katika Uchaguzi Mkuu uliopita, Magige alisema ni wajibu wa vyama kuwashawishi wananchi wa maeneo ambayo wapigakura hawakujitokeza kwa wingi kuwapigia kura.
“Mbali na kazi nyingine, kazi nyingine kubwa ya vyama vya upinzani ni kuhakikisha wale ambao hawajapiga kura katika uchaguzi uliopita wanapiga kura na kupata ushindi mkubwa, hiyo ni moja ya kazi yetu nawapongeza sana, ingawa mimi ni mwana-CCM,” alisema Magige.
Baada ya ziara hiyo ya Butiama, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, alihutubia wananchi wa Mwibara wilayani Bunda na kuwaambia kuwa CCM inadai kuwa vyama vya upinzani ni vyama vya wakati wa uchaguzi, wakati sio kweli na kusema:
“Si mnatuona, tumekuja hata kama hakuna uchaguzi na tutaendelea kuwatembelea kusikiliza matatizo yenu.”
Pia, aliwashukuru wananchi wa Mwibara kwa kukipigia kura Chadema licha ya kutopata mbunge na kuwataka katika chaguzi nyingine wawe makini ili wasiibiwe kura zao.
Mbali na viongozi wa juu, Freeman Mbowe (Mwenyekiti) na Dk. Slaa, ziara hiyo iliwajumuisha karibu wabunge wote wa chama hicho kutoka majimbo mbalimbali na wale wa viti maalum.
Chadema imekuwa ikiendesha maandamano kuishinikiza serikali kutoilipa fidia ya Sh. bilioni 94 kampuni ya kufua umeme ya Dowans Tanzania Limited, kupunguza bei ya umeme na kupinga uchaguzi wa Meya wa Arusha, ambao chama hicho kinaulalamikia kuwa ulijaa mizengwe.
Wakati jana Dk. Slaa akihutubia mikutano ya hadhara Mwibara na Bunda, Mbowe alihutubia Tarime huku wabunge wengine wakifanya ziara katika wilaya za Musoma Vijijini, Shirati na maeneo mengine ya Mkoa wa Mara kusambaza ujumbe huo.
CHANZO: NIPASHE

No comments: