ANGALIA LIVE NEWS

Monday, February 28, 2011

DK Slaa atibua mambo kwa Wassira

Katibu mkuu wa Chadema,Dk Wilbroad Slaa
Anthony Mayunga, Bunda na Frederick Katulanda, Butiama
ALIYEKUWA mgombea ubunge wa ubunge kwa tiketi ya Chadema jimbo la Bunda Elias Maarugu ametimuliwa kwenye mkutano wa hadhara wa chama hicho uliohutubiwa na katibu mkuu Dk Wilbroad Slaa baada ya kukataliwa
na wananchi kwa madai kuwa alihongwa na kumwachia Stephen Wasira.

Dalili za kumkataa Maarugu zilianza mapema mara baada ya kuitwa asalimie wananchi mjini Bunda, umati mkubwa wa wananchi ulipiga kelele na kudai hawataki kumsikiliza kwa kuwa aliwasaliti na kuuza haki zao.

Wananchi hao walipiga kelele wakisema hawako tayari kumsikiliza huku wakimtaka atoke  jukwaani kwa kuwa hafai, "hatumtaki huyo mtoeni hapo aliuza kura, alihongwa msaliti hafai mtoeni hatutaki kumsikiliza.”

Kelele hizo zilisikika sauti kwa nguvu za wananchi waliojaza uwanja wa stendi ya zamani.

Licha ya Maarugu kujikakamua na kusema Peoples, wananchi walipaza sauti na kumtaka atoke haraka sana," hatutaki kumsikiliza huyo mtoeni huyo hafai msaliti alikuwa wapi kwanini amekuja leo siku zote alikuwa
wapi?”walihoji.

Kutokana na kelele na wananchi kugoma kumsikiliza Dk Slaa alilazimika kuingilia kati na kusema kuwa, "sauti ya wengi ni sauti ya Mungu, hivyo kama umma wote huu unakukataa ndugu yangu Maalugu kuna kitu naomba utueleze kwa nini watu hawa wanakukataa.”

Hata hivyo katibu mkuu huyo kuwataka wananchi wawe na subira wananchi waliendelea kugoma na kusema kuwa hawako tayari kumwona wala kumsikiliza hivyo wakamtaka atoke eneo hilo.

“Maarugu Chadema inapinga ufisadi ndani na nje ya chama kama unatuhumiwa wewe ni mtu mzima na kuheshimu sana nakuomba uamke taratibu uage uende kwako na sisi tunakuchunguza, natamka kuanzia sasa
kuwa nakufutia ugombea wa miaka mitano ijayo kwa kuwa hufai maana nakataliwa na wananchi, nitatoa taarifa kwenye kamati tendaji ya chama,”alisema.

Kutokana na kauli hiyo Maarugu ambaye aliwahi kuwa mkuu wa wilaya ya Magu na Misenyi alilazimika kushuka taratibu huku akizomewa na maelfu ya wananchi waliokuwa wamefurika hapo,huku Dk Slaa akiwasihi wananchi
wasimpige,kumtukana kwa kuwa suala lake bado linachunguzwa na wananchi watapewa majibu.

Aliagiza kamati tendaji ya chama wilaya kuketi haraka kujadili kisha kutoa taarifa kwake ndani ya wiki mbili, na kama wataridhika nayo wataifanyia kazi,vinginevyo watalazimika kuunda kamati maalumya kufuatilia kwa kuwahoji wananchi wa jimbo hilo.

Mapema Mkurugenzi wa mambo ya Bunge na halmashauri wa chama hicho John Mrema alisema kitendo hicho hakipaswi kuvumiliwa hata kwa viongozi wengine wa chama hicho na kuwa chadema mambo yao yako wazi.

Wakati huo huo Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amekataa madai ya wakazi wa Tarime kudai kuwa kura zao zilichakachuliwa na CCM kushinda Ubunge katika jimbo hilo.

Akizungumza jana katika uwanja wa mpira wa barabara ya Nyamwaga, mwenyekiti wa Chadema, alisema hakubaliani na hoja za watu kusingizia chama chake kilishindwa uchaguzi kutokana na kuchakachuliwa kura bali mgawanyiko wa ndani.

Alisema katika kipindi cha uchaguzi alifika Tarime na kukaa kikao na viongozi wa chama chake Tarime na kubainisha kuwa katika kikao hicho aliwaeleza wazi kama hawajui kushindwa uchaguzi na kama wamesahau kutawaliwa na CCM basi wajue kuwa watajifunza pale ambapo kiti cha ubunge kitakapo ondoka.

“Niliwaeleza katika kikao cha ndani kama hawajui hathari za ubinafsi basi watajifunza pale watakapopoteza kiti cha Ubunge, niliwaeleza kuwa mtajifunza pale mtakapotawaliwa na CCM. Sasa kuniambia kuwa kura zilichakachuliwa nakataa…sababu naijua,” alieleza Mbowe ambaye alionekana kukasirika.

Mwenyekiti huyo ambaye ni kiongozi wa kambi ya upinzani Bungeni, alisema ingawa alitambua mpasuko huo, yeye akiwa kiongozi wa chama mwenye dhamana ya kupitisha majina ya wagombea, walipoletwa waliogombea waliwapima kwa vigezo na kuamua kulirudisha jina la Waitara Chacha.

“Leo nalisema hili ili mjue kuwa pale ubinafsi unapotawala katika harakati za ukombozi ni hatari sana…, Mwera alikuwa anataka kuwa mbunge, Waitara, Heche na Matage, wote hawa waliutaka ubunge lakini hawawezi kuwa wote ni lazima ashinde mmoja,” alifafanua.

Alisema kuwa kila mmoja anayo haki ya kugombea ubunge lakini inapofikia kila mmoja anataka kushinda hapo ndipo inapokuwa ngoma.

“Nasema tulirudisha jina la Waitara, hatujutii hilo na wala watitajutia. Mwera anaona ahaa…, nadhani hakuridhika, siwezi kujadili mtu hapa na Mwera namheshimu. Basi hapa ndipo ukatokea mgawanyiko na ninyi mkawashabikia mkasahau tatizo siyo mtu bali ni kushinda ubunge,” alisema Mbowe.

Alisema lakini tokea kumalizika kwa uchaguzi huo watu wakawa wanasema kuwa walisalitiwa na wao kwa wao na wengine kwenda nje ya wilaya kusaidia kampeni jambo ambalo alisema siyo kweli na kusema kwa vile uchaguzi umekwisha sasa ni zamu ya kujipanga na kuangalia walipokosea na kujiandaa kwa uchaguzi.

“Sitaki kusikia hili la kuchakachuliwa kura Tarime, kama mnadai kuwa mlichakachuliwa kura mlikuwa wapi? Ukerewe ambao walikuwa wakiambiwa mambo kama tarime wameshinda, mabomu yalipigwa lakini wakerewe walikomaa na matokeo yakatangazwa, Mwanza risasi za moto zilipigwa na mabomu usiku kucha siku tatu lakini wakaona looo watangaze sasa Tarime mlikuwa wapi?” alihoji Mbowe.


CHANZO:MWANANCHI

No comments: