ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, February 2, 2011

Moto waua wanne, kichanga chabaki yatima

WATU wanne wa familia moja; mama na wanawe watatu wa kijiji cha Minjingu kata ya Ngaiti wilayani Babati, Manyara wamekufa kwa kuteketezwa na moto uliounguza nyumba walimokuwa wanaishi. 

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Parmena Sumary, alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea Januari 28 saa 3.30 usiku. 

Kamanda Sumary aliwataja waliokufa kuwa ni mama wa watoto hao, Mesoni Maji (35), mwanafunzi wa darasa la saba wa shule ya msingi Minjingu, Agness (14), Nduleti (10) na Kalai Matinda (8). 


“Chanzo cha moto huo uliosababisha vifo hivyo bado hakijajulikana ila Jeshi la 
Polisi linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo ili kubaini chanzo halisi,” alisema Kamanda Sumary. 

Alisema, marehemu hao walizikwa juzi saa 6.15 mchana kwenye makabuni ya Minjingu. 

Mmoja wa ndugu wa marehemu hao, Omary Olong’oni, aliwambia waandishi 
wa habari jana kuwa Maji ameacha mtoto mwenye umri wa kati ya miezi sita na minane ambaye alinusurika kwenye ajali hiyo. 

Olong’oni alisema, mtoto huyo alikuwa ndani ya nyumba hiyo ya nyasi na familia hiyo na wakati moto unaanza mama yake alimtoa nje na aliporudia wengine ili awatoe nje bahati mbaya moto ukamzidia. 

Alisema mtoto huyo amebaki yatima kwani hivi karibuni baba yake mzazi Matinda 
Sangeti mkazi wa kijiji hicho, naye alifariki dunia kwa ajali ya kugongwa na gari. 

Alisema kikao cha ukoo wao kinaendelea kukutana ili kupanga mikakati ya kumsaidia mtoto huyo.

No comments: