ANGALIA LIVE NEWS

Friday, February 4, 2011

Noti mpya zaitikisa BoT-Mwananchi

MTAALAMU  KUTOKA NJE  ALETWA KUTHIBITISHA UBORA
Claud Mshana na Boniface Meena
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imelazimika kumleta nchini, Mkurugenzi wa Kampuni ya Crane Curreny, ya Sweden iliyoshinda zabuni ya kutengeza noti mpya zilizoanza kutumika Januari mwaka huu, kueleza ubora wake baada ya noti hizo kuhisiwa kuwa zinachuja na ni rahisi kughushiwa.

Ujio wa mtaalamu huyo, Peter Brown ni utekelezaji wa ahadi ya Gavana wa BoT, Professa Benno Ndullu aliyoitoa wiki mbili zilizopita kuhusu taasisi yake kufuatilia ubora wa noti mpya ambao ulianza kutiliwa mashaka na baadhi ya wananchi.

Januari 23, mwaka huu gazeti hili liliripoti habari ya uchunguzi iliyoelezea mashaka kuhusu ubora wa noti hizo mpya, baada ya kubainika kuwa baadhi zinachuja na kuacha rangi zikilowa maji au jasho.
Kwa mujibu wa uchunguzi huo, noti hizo hasa za Sh5,000 na Sh10,000 pia zilibainika kuwa zikikandamizwa kwenye karatasi nyeupe bila kulowanishwa na maji au jasho, huacha rangi.

Hali hiyo ilisababisha baadhi ya watu kuanza kutilia mashaka ubora wake, huku wasomi wakitaka Serikali kuwa makini kwa kuwa inaweza kupata hasara kubwa.
Katika kufuatilia suala hilo, Gavana Ndulu aliliambia Mwananchi kwamba BoT itafuatilia utta huo ikiwa ni pamoja na kuwasiliana na mzabuni ambaye ni kampuni ya Crane Currency ili kasoro zinazojitokeza ziweze kurekebishwa mara moja.

Maelezo ya mtaalamu Brown

Jana, Brown ambaye ni Mkurugenzi Mauzo wa Kampuni ya Crane Currency, Kanda ya Afrika alitoa ufafanuzi kuhusu ubora wa noti mpya ili kuondoa mashaka yaliyojitokeza.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Brown alisema kutoa rangi ni moja ya alama za usalama na ubora wa noti hizo.
Brown alifafanua kuwa noti hizo zimetengenezwa kwa teknolojia ijulikanayo kama ‘Intaglio’ ambayo imekuwa ikitumika kwa muda mrefu katika kuchapisha noti mbalimbali duniani. Alisema teknolojia hiyo inatoa uhakika mkubwa wa usalama wa noti.

Brown alifika nchini juzi na jana alifanya mkutano na uongozi wa BoT na kusema kampuni yake imekuwa ikichapisha noti mbalimbali duniani, zikiwemo dola za Marekani na kwamba noti zote zilizochapishwa kwa kutumia teknolojia hiyo huwa na wino mwingi katika kingo zake.
Kampuni hiyo ya Crane Currency yenye makao yake nchini Sweden ndio iliyoshinda zabuni ya kuchapisha noti mpya za shilingi 500, 1,000, 2,000, 5,000 na 10,000.
Akifafanua juu ya madai kuwa noti hizo zikilowa kwa jasho au maji zinatoa rangi, Prof Ndulu alisema uchujaji huo hauwezi kumaliza rangi iliyotumika katika utengenezaji na kwamba noti hizo zinaweza kuendelea kuwa katika ubora ule ule kwa muda mrefu.
“Noti zote hizi zinapotengenezwa kiwandani, zinapitishwa kwenye test (majaribio), zinawekwa kwenye maji, zinapitia cycles (mizunguko) yote na zinapotoka zinatakiwa zibaki vilevile,” alifafanua.
Maelezo ya Gavana Ndulu
Gavana Ndulu kwa uapnde alieleza kuwa noti hizo kutoa rangi wakati zimesuguliwa kwenye karatasi au kulowana ni moja ya alama zake za usalama.

Hata hivyo, wakati BoT wakitangaza katika vyombo vya habari kuhusu alama za usalama (security features) katika noti hizo, hawakuwahi kutaja hilo la kuchuja kwa rangi za noti hizo kuwa miongoni mwa vigezo vya ubora wake.

Ndulu alisema rangi hiyo inyotoka katika noti hizo, huwezi kuiona katika noti bandia na kwamba teknolojia iliyotumika inasaidia noti hizo kukaa muda mrefu bila kuchakaa.
Prof Ndulu aliwaambia waandishi wa habari kuwa hata noti za zamani za Sh 5,000 na 10,000  pia zikisuguliwa kwenye karatasi huacha rangi.
“Ukitaka kujua noti halali, kama ukiisugua kwenye karatasi, lazima iache rangi na rangi inapokuwa imekolea zaidi, inaacha zaidi,” alisema Prof Ndulu na kuongeza:
"Noti bandia haziwezi kuacha rangi kwa kuwa hazikutengenezwa kitaalamu na hiyo ni njia nzuri kwa mtumiaji kugundua noti bandia na noti halali na pia noti ikiwa na rangi nyingi inakuwa ni imara na haichakai mapema".
Kuhusu kuwepo kwa noti za zamani na za sasa katika mzunguko wa fedha alisema noti zote ni halali na zitaendelea kutumika hadi zile za zamani zitakapoisha kwenye mzunguko.
Prof Ndulu alisema noti hizo zitachukua mwaka mmoja kupotea, hivyo zote zitaendelea kuwa halali kwa manunuzi ya nchini.
Alisema hivi sasa kuna watu wameshaanza kutengeneza noti bandia na tayari ameshaiona moja ya aina hiyo na kufahamisha kuwa suala la kubadili fedha kila baada ya muda linatokana na kuwakwepa wajanja ambao hutengeneza bandia.
Akizungumzia akiba ya fedha za kigeni ambayo Tanzania inayo hadi hivi sasa, Prof Ndulu alisema kuwa nchi ina dola za Marekani 3.8 bilioni ambazo zinaweza kununua huduma kwa nchi nzima kwa miezi sita mfululizo.
Alisema kiasi hicho cha fedha ni kikubwa kupita nchi yeyote ya Afrika Mashariki.
"Hatuna shida kwenye hilo kwa kuwa hata kwa benki za biashara zina kiasi cha Sh1 bilioni na watu wa kawaida wana Sh1.5 bilioni,"alisema Prof Ndulu na kuongeza kuwa nchi kwa ujumla ina zaidi ya Sh5 bilioni ya fedha za kigeni.

Mtazamo wa Jamii
Baadhi ya watu waliowasiliana na gazeti hili wamelalamikia tatizo la noti mpya kuchuja na kuitaka Benki Kuu (BoT) kulifuatilia kwa karibu na kulipatia ufumbuzi.

Lawrence Mkina ambaye mkazi wa jijini Dar es Salaam aliiambia Mwananchi kwa njia ya simu kuwa haamini kama noti mpya zina ubora unaotakiwa.

Alisema aliweka noti mpya za Sh 5,000 lakini kwenye mfuko wa shati jeupe baadaye alipozitoa shati lilikuwa limechafuka kwa rangi ya noti hizo.

Mkina alidai kuwa huenda noti hizo zitakuwa ‘zimechachakuliwa’ na wanjanja mitaani kwani hata ukiisugua katika karatasi nyeupe inaacha rangi kama vile carbon paper.

Ili kuthibitisha madai hayo, gazeti hili ilichukua noti mpya ya Sh 5,000 na kuisugua kwenye karatasi ya nyeupe na noti hiyo iliacha rangi nyingi ya bluu.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk Honest Ngowi alieleza madhara ya noti zisizokuwa na ubora kuwa ni pamoja na kugushiwa kirahisi.

“Ubora wa noti ni kitu muhimu na kama ikikosa ubora inaleta maswali mengi na moja ya athari itakayojitokeza ni kugushiwa kirahisi,’’ alisema Dk Ngowi.

Dk Ngowi ambaye ni mwanazuoni aliyebobea katika taaluma ya uchumi, alisema noti ikikosa ubora, huchakaa mapema na kuleta utata katika kukubalika kwenye soko.

“Kutokana na kuchakaa mapema, serikali italazimika kuchapisha noti nyingini hali ambayo italigharimu taifa fedha nyingi katika muda mfupi. Pia inawezekana nchi za Jumuiya ya Afrika ya Afrika Mashariki, zikakataa kuzitumia noti hizo,’’ alisema.

Kuhusu sifa na ubora wa noti, Dk Ngowi alisema ni lazima iwe katika kiwango bora ikiwamo kuwa na karatasi ngumu isiyochakaa na kuchanika mapema na kuwa na uzito.

“Noti yenye ubora ni lazima iwe na sifa ya Durabillity, isiyoharibika mapema na iwe nzito,’’ alisema Dk Ngowi.

Ahadi ya Gavana

Kutokana na hali hiyo, Gavana Ndullu, alisema BoT inafuatilia kwa karibu matatizo yanayojitokeza katika noti hizo mpya na kuyafanyia kazi.

“Hili linawezekana ingawa wewe ndio mtu wa kwanza kujitokeza kueleza, lakini kama tatizo hili lipo, tutalifanyia kazi,’’ alisema Profesa Ndullu.

Akaongeza: “ Kwa sasa BoT ina monitor (Fuatailia) kwa ukaribu usambazaji wa noti mpya pamoja na kuangalia matatizo yanayojitokeza na kuyafanyia kazi haraka iwezekanavyo.’’

Gavana huyo alisema matatizo yote yatakayojitokeza katika noti hizo yatafikishwa kwa mzabuni aliyezichapisha ili kufanyiwa kazi.

No comments: