Tausi Ally
MFANYABIASHARA maarufu nchini, Yusuf Manji, jana alipanda kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam kutoa ushahidi katika kesi aliyomfungulia Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, Regild Mengi na kumdai fidia Sh1.
Lakini katika kile kilichothibitisha kukua kwa teknolojia, Manji alitoa sehemu kubwa ya ushahidi kwa kuonyesha mkanda wa video badala ya kuzungumza.
Mkanda huo wa picha wa (DVD) ulionyesha hotuba ya Mengi wakati akizungumza na waandishi wa habari na kumtaja Manji kuwa miongoni mwa mafisadi papa wanaoihujumu nchi.
Mkanda huo ulionyeshwa katika mahakama ya wazi, mbele ya Hakimu Mkazi Aloyce Katemana, wakati Manji akitoa ushahidi wake katika kesi hiyo iliyokuwa kivutio cha aina yake jana mahakamani hapo.
Katika mkanda huo Mwenyekiti huyo wa Makampuni ya IPP, alionekana na kusikika akiwataja watu watano wanaotuhumiwa kuhusika na ufisadi mkubwa nchini na kuitaka serikali iwashughulikie haraka ili kuinusuru nchi isiyumbishwe nao.
Katika hotuba yake hiyo pamoja na Manji, Mengi aliwataja mafisadi wengine aliowaita papa kuwa ni pamoja na Mbunge wa Igunga na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CC-CCM) na Halmashauri Kuu ya Chama hicho (NEC-CCM) Taifa, Rostam Aziz. Wengine ni wafanyabiashara, Tanil Somaiya, Jeetu Patel na Subash Patel, ambao alisema wanatuhumiwa kuiba mabilioni ya wananchi na kuzihamishia nje ya nchi.
Baada ya kumaliza kuonyesha mkanda huo (DVD) mahakamani hapo, Manji aliiomba mahakama iipokee DVD hiyo kama moja ya kielelezo cha ushahidi wake katika kesi hiyo.
Mbali na mkanda huo, katika ushahidi wake Manji pia alitoa nyaraka mbalimbali ikiwemo mikataba yake ya kazi pamoja na vyeti vya shule na vyuo mbalimbali alivyosoma na kuvionesha mahakamani hapo kama vielelezo vya ushahidi kwenye kesi hiyo.
Katika ushahidi huo Manji alidai kuwa tuhuma zilizotolewa na Mengi dhidi yake zilimshushia heshima kwa taifa, familia yake, wafanyakazi wake na wabunge kwa kuwa waliamini yaliyosemwa na Mengi.
Alidai kuwa baada ya Mengi kutoa tuhuma hizo ambazo alidai kuwa yeye(Manji) ni Fisadi Papa, alialikwa kwenye mkutano (public conference) ambao ulishirikisha wabunge kutoa hotuba, lakini kutokana na tuhuma zilizotolewa na Mengi aliambiwa kuwa hotuba yake imefutwa kwa sababu ‘si mtu mzuri kwa Tanzania’ hivyo akawa mgeni wa kawaida hatua ambayo ilimnyanyasa.
Akiendelea kutoa ushahidi wake, Manji alidai kuwa yeye hausiki katika kashfa inayohusu kampuni ya Richmond, ambayo ilitiliana saini na Shirika la Umeme nchini (Tanesco) mkataba tata wa kufua umeme wa dharura.
Pia alidai ahusiki katika kashfa nyingine ya akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) kwenye Benki Kuu ya Tanzania (BoT), wala kampuni ya Dowans Tanzania Limited iliyorithi mkataba tata wa Richmond.
Alidai pia hahusiki katika ununuzi wa helikopta na magari ya jeshi, ndege ya Rais, rada, Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mfuko wa Pensheni ya Watumishi wa Umma (PSPF), Bahati Nasibu ya Taifa na Mradi wa Makaa ya Mawe wa Mchuchuma kama ilivyodaiwa.
Hata hivyo, Hakimu Katemana ameiahirisha kesi hiyo hadi leo ambapo Manji ataendelea kutoa ushahidi wake.
Kufunguliwa kwa kesi
April 29, 2009, Manji alimfugulia kesi Mengi pamoja na Kituo cha runinga cha ITV kinachomilikiwa na Mwenyekiti huyo wa IPP akidai alipwe fidia ya Sh1 kama fidia ya kumkashifu kwa kumwita fisadi papa pamoja na wafanyabiashara wengine.
Manji alifungua kesi hiyo katika mahakama ya hakimu mkazi Kisutu, Dar es Salaam kupitia kampuni ya muwakili ya Muganda, Kamugisha na Bwana.
Wakili John Kamugisha, aliyemwakilisha Manji wakati wa kufungua kesi hiyo alipoulizwa sababu ya mteja wake kudai shilingi moja kama fidia, alisema mteja wake huyo (Manji) anaamini kuwa heshima na utu vina thamani kuliko fedha. Kwa mujibu wa Kamugisha kesi hiyo ni ya kwanza kudai kiwango kidogo cha fedha na kwamba ilitarajiwa kuwashangaza wengi.
Katika kesi hiyo Manjia anadai kuwa Mengi kupitia kipindi maalumu cha ITV kilichorushwa April 23, 2009 mara baada ya taarifa ya habari ya saa mbili usiku alimkashifu kwa kutoa matamshi yanayomdhalilisha.
No comments:
Post a Comment