Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, akizungumza na Spika wa Bunge Anne Makinda (kulia), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Dk Mary Nagu (kushoto) na Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid baada ya kufunga semina ya Wabunge kwenye ukumbi wa hoteli ya Pearl Ubungo Plaza Dar es Salaam. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
WAKATI Mkutano wa Pili wa Bunge la 10 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ukitarajiwa kuanza Jumanne ijayo, Serikali imewataka wabunge kuepuka malumbano yasiyo na msingi ya kuhoji utendaji wa mihimili mingine, kwa kuwa hayana msingi wala msaada wa kimaendeleo kwa wananchi.
Badala yake, imewataka wajenge uhusiano mwema na ushirikiano na mihimili hiyo huku wakitekeleza wajibu uliowapeleka bungeni kwa kuzingatia sheria, mipaka ya kazi zao, maadili, utawala bora na haki za binadamu, kwa lengo la kuliepusha Taifa na athari zinazoepukika.
Akizungumza wakati wa kufunga semina ya siku 10 kuhusu kanuni, taratibu za Bunge na mambo mengine Dar es Salaam jana, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, alisema yamekuwepo malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kuhusu mmomonyoko wa maadili unaotokana na malumbano ya viongozi, jambo linaloashiria kukiukwa kwa maadili, sheria, mipaka ya kiutendaji na utawala bora.
Kwa mujibu wa Pinda, maendeleo ya nchi na wananchi wake yatatokana na viongozi wanaofuata maadili, misingi ya utawala bora, haki za binadamu, sheria na mipaka ya kazi zao, hivyo wabunge hawana budi kulitazama hilo kwa makini na kulifanyia kazi.
“Ili muweze kuwajibika kwa makini, kirahisi, kwa upendo na kuepuka matatizo katika utendaji wenu, someni vizuri Katiba ya nchi na marekebisho yake ya mara kwa mara, hakikisheni mmeielewa vema, someni sheria, kanuni na mipaka ya kazi zenu ili kusiwe na malumbano, ukiukwaji wa maadili wala utawala bora,” Pinda alishauri.
Alifafanua kuwa kiongozi yeyote asiyefuata utawala bora, hawezi kulinda maadili ya kazi yake wala haki za binadamu na ili wabunge wawawakilishe wananchi wao ipasavyo, lazima waoneshe mfano kwa kufuata na kulinda maadili ya kazi zao, ikiwa ni pamoja na kutekeleza majukumu yanayowapasa bila visingizio.
Mbali na hilo, Pinda alisema Serikali imebaini kuwa wabunge wengi wanaolalamika kutopewa huduma wanazoomba serikalini, hawazingatii mfumo wa uendeshaji wa kazi za Serikali na kwamba itakuwa ikiwachukulia hatua watakaobainika kuzikiuka.
“Hata kama ni Mbunge, unapaswa kufuata taratibu za kiutendaji za serikalini, ndipo upewe huduma unayohitaji ... hata hivyo, tumeona umuhimu wa kuhakikisha taasisi mnazosimamia zinawapa uhuru wa kufanya kazi zenu kwa kuandaa namna mtakavyopata posho zenu, kwa kazi mnazozifuatilia huko, ili msitegemee taasisi hizo mnazozifanyia kazi, kwa kuwa inaweza kusababisha msiseme upungufu mnaouona huko,” Pinda alisema.
Kuhusu suala la haki za binadamu, Waziri Mkuu aliwataka wabunge kuhakikisha kuwa mikataba ya haki hizo inayosainiwa inawekewa sheria zisizopingana, ili iweze kutekelezeka.
Kadhalika, alisema wakati wa kujadili mipango ya nje ya Serikali, kila jambo litazamwe kwa hadubini itakayolinda haki za binadamu na pia wanapaswa kuelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kutafuta haki kwenye vyombo vya sheria, badala ya kujichukulia sheria hizo mikononi.
Wakati huo huo, Pinda alizungumzia suala la rushwa na kusema ni lazima vita dhidi ya rushwa ishinde na tatizo hilo likome.
Aliitaka Takukuru isikae kimya kuhusu mafanikio yake dhidi ya rushwa kwa kuwa kimya hicho kinawafanya wananchi wakose imani nayo.
“Si kweli kwamba hakuna tulichofanya dhidi ya rushwa, Takukuru wambieni wananchi ... vilio vya rushwa bado ni vingi, waonesheni mmefanya nini hadi sasa,” alisema.
Bunge lililopita liligubikwa na malumbano kuhusu mikataba ya madini, likiwamo suala la mitambo ya kufua umeme ya Richmond na baadaye Dowans, malumbano ambayo yanaendelea hivi sasa nje ya Bunge, huku baadhi wakitaka yarejeshwe bungeni kujadiliwa.
Bunge la sasa linatazamiwa kuwa na malumbano pia kutokana na wabunge wengi kuwa vijana na wenye ‘moto’ na munkari hasa kutoka kambi ya Upinzani.
Wachunguzi wa masuala ya kisiasa wanaamini kauli hii ya Waziri Mkuu, huenda ikamsaidia Spika Anne Makinda kuliongoza Bunge hilo kwa utulivu mkubwa na kutumia zaidi kanuni zinazoliongoza. |
No comments:
Post a Comment