ANGALIA LIVE NEWS

Friday, February 4, 2011

Unaumizwa na mapenzi, umesimama kundi gani?-GPL

TUMEKUTANA tena kwenye kona yetu ya mahaba ambayo kila kukicha inazidi kushika chati na kupata maswali mengi juu ya matatizo ya kimapenzi. Nimekuwa nikipata ujumbe wa pongezi na kukosoa pia juu ya masuala ya mapenzi.

Wapo walioniuliza kwa njia ya simu na moja kwa moja niliwajibu lakini wengine walionitumia ujumbe mfupi na niliwajibu.
Pia wapo niliowajibu kupitia njia ya gazeti ambao majibu ya maswali yao huwagusa watu wengi. 


Dada yangu mmoja aliniuliza kwa nini ameachwa mara nne na wanaume tofauti, swali hilo nililipata pia kutoka kwa ndugu yangu aliyeachwa na mpenzi wake bila kosa. Penzi lao lililodumu kwa miaka minne tangu walipokuwa shuleni.

Najua nikikuuliza wewe jibu laweza kuwa jepesi utakalompa au mtu akuulize kwa nini watu huachana. Nina imani swali la hapo juu linajieleza.

Majibu ya swali lililopo hapo juu, kila mmoja ana lake la kujibu ukimuuliza swali hili. Kabla sijalijibu kwa kirefu ngoja nimjibu dada yangu na ndugu yangu msomi ambaye masomo kwa sasa hayapandi baada ya kupigwa kibuti na mpenzi wake.

Wote wamejiona hawana kosa mpaka ikafikia hatua ya kuuliza maswali, si hao tu wapo wengi waliokumbwa na tatizo kama hili lakini wamekaa kimya na kuumia moyoni.

Siku zote unapoachwa na mpenzio bila sababu maalumu na kuwa na uhakika hajafanya kosa lolote. Jibu ni jepesi kuwa uliyekuwa naye hakuwa na mapenzi nawe bali alikupenda kwa sababu fulani.

Utajiuliza wewe ni mzuri una kila sifa ya kuwa binti mrembo au mtanashati mwenye mvuto, lakini bila kutegemea mpenzio anaamua kukuacha bila ya wewe kuelewa tatizo.

Sehemu hii naomba utege sikio kwa makini ili uelewe kwa nini umeachwa bila sababu. Ni kweli una sifa zote pengine mpenzio alikuhangaikia kwa muda mrefu hadi kukupata au kabla ya kumpata umeweza kutimiza masharti magumu mpaka kumtia kwenye himaya yako.

Mwanzoni mapenzi yenu yalikuwa moto kila mmoja alijituma ipasavyo. Bila kutegemea mpenzio anakatisha penzi lake ghafla bila sababu maalum na ukiuliza swali anakujibu “Nimeamua tu.” Hapo lazima uelewe nini maana ya mambo haya katika mapenzi, kupenda na kutamani.

Hivi vitu huwachanganya watu na kushindwa kuvitofautisha ambavyo mara nyingi huleta majuto kwa watu, pale unaposhindwa kuelewa mwenzio yupo kundi gani katika mapenzi. Mapenzi yana kanuni zake ambazo najua wengi hamzijui na utakapozijua hutumia sana pale penzi lako litakapovunjika ghafla bila sababu.

Ili kuyajua yote tukutane wiki ijayo kuiendeleza mada yetu hii ambayo ina mambo mengi naimani yanaweza kuwa mageni upande wako na kukupa muono mpya katika mapenzi.

No comments: