ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, February 3, 2011

Polisi aliyegongwa na waziri afariki dunia-Habari Leo

ASKARI wa Jeshi la Polisi, Koplo Ali Khamis Haji ambaye aligongwa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Ramadhan Abdallah Shaaban, amefariki dunia na kuzikwa Jumamosi iliyopita wakati akikimbizwa hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja. 

Ajali hiyo ilitokea Januari 13 mwaka huu, katika eneo la Mombasa, mkabala na kijiji cha watoto yatima cha SOS, ambapo Waziri Shaaban aliyekuwa akiendesha gari namba Z 247 BH lilikuwa likiingia katika barabara kuu kutoka barabara ndogo ya SOS jirani na klabu ya Nyuki na kumgonga askari huyo ambaye alikuwa amepakiwa kwenye pikipiki aina ya Vespa namba Z 830 CA. 


Askari huyo ambaye alikuwa akitoka katika kituo chake cha kazi cha Polisi Ng'ambo, aligongwa na kupata majeraha mguu wa kushoto na katika uti wa mgongo, na afya yake iliendelea kuzorota hadi kifo chake saa 4.30 asubuhi Januari 28 akiwa njiani kupelekwa Mnazi Mmoja. 

Viongozi wa Jeshi la Polisi Zanzibar, akiwamo Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Aziz Juma Mohamed na Mkuu wa Kikosi cha Usalama wa Barabarani Mjini Magharibi, Shafi Iddi Hassan, waligoma kuzungumzia suala hilo, lakini Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo. 

Kamishna huyo, alisema tayari uchunguzi umeanza, ingawa alisema umegawanyika katika maeneo mawili, sehemu ya kwanza ni kujua chanzo cha ajali baina ya wapanda pikipiki hao na Waziri, na sehemu ya pili ni kujua chanzo cha kifo cha koplo Ali mwenye namba E.3665, ambaye ni mkazi wa Muungano eneo la Kisauni Wilaya ya Magharibi mjini hapa. 

Kamishna Mussa alisema baada ya ajali hiyo, alilazwa siku moja Mnazi Mmoja, na kisha kurejea nyumbani, kabla ya hali yake kubadilika na kulazimika kukimbizwa hospitali ambako alifariki dunia. 

"Maiti kabla ya kuzikwa alilazimika kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu, na ripoti yake itatusaidia kukamilisha uchunguzi wa kadhia hiyo," alisema Kamishna Mussa. 

Uchunguzi wa gazeti hili, ulibaini kwamba tayari suala hilo, limeripotiwa makao makuu ya Jeshi la Polisi Zanzibar, kwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, lakini hadi jana, kesi hiyo ilikuwa haijawasilishwa mahakamani tangu ajali hiyo itokee Mombasa ambako ni maarufu kwa burudani katika klabu ya Nyuki inayomilikiwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ). 

Juhudi za kumpata Waziri Shaaban, zilishindikana, kutokana na simu yake ya mkononi kutopokewa mara kadhaa wakati akitafutwa kuelezea mazingira ya ajali yalivyokuwa. 

Waziri Shaaban, ambaye ni Mjumbe wa Kuteuliwa wa Baraza la Wawakilishi, amewahi kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba na Utawala Bora, Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo. 

Habari zilisema marehemu Koplo Ali alizikwa Kisauni Januari 28 na maziko yake kuhudhuriwa na watu mbalimbali wakiwamo askari wenzake pamoja na Waziri Shaaban.

No comments: