ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, February 1, 2011

Watoto 10 wachanga wafukiwa shimoni

Image
Askari Polisi mwenye mavazi ya kiraia (kushoto) akionesha shuka iliyokutwa imezungushwa kwenye miili ya vichanga vilivyofukiwa kwenye shimo la taka eneo la Fera Msisiri B jirani na makaburi ya Mwananyamala Dar es Salaam. Kulia ni maofisa wa Polisi wakichukua vielelezo vya tukio hilo. (Picha na Robert Okanda).
MIILI ya watoto 10 wachanga imekutwa imefukiwa pamoja katika shimo, Dar es Salaam.

Marehemu hao walikutwa jana katika eneo la makaburi ya Mwananyamala wilayani Kinondoni wakiwa katika kaburi la pamoja wakiwa wameviringwa shuka lenye nembo ya Hospitali ya Mwananyamala. 

Pamoja na shuka hilo ni khanga zilizokuwa na namba ya moja ya wadi za hospitali hiyo nazo zikiwa zimewaviringa maiti hao na kufukiwa katika shimo la taka karibu na makaburi hayo.

Watoto hao ambao wanapishana umri na ambao walikutwa tayari wamefariki dunia ndani ya shimo hilo, ni wa kike watano na wa kiume watano pia.

Kwa mujibu wa shuhuda wa tukio hilo ambaye ndiye mmiliki wa shimo hilo, Amour Mbaga, wakati akienda kutupa taka kwenye shimo hilo alilosema alilichimba mwenyewe, alishangaa kulikuta limefukiwa huku udongo ukionekana mpya.

“Nilishituka kuona shimo langu la taka limefukiwa, nikaenda kuchukua jembe na kufukua na ghafla nikaona mkono wa mtoto, nilishituka zaidi na kukimbilia kwa majirani kuwataarifu,” alisema.

Alisema majirani walimshauri akaripoti tukio hilo Polisi na kufanya hivyo kwenye kituo cha Polisi cha Oysterbay na kurejea nyumbani kwake na askari ambao walifukua shimo hilo wakakuta miili hiyo.

Baada ya miili hiyo kuopolewa shimoni, polisi walimwita Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mwananyamala, ambaye aliwapekua watoto hao na kubaini wameviringwa khanga nyingi na shuka moja lililoandikwa MSD Mwananyamala Hospital Ward 1A.

Aidha, katika moja ya khanga zilizotumika kuwaviringa maiti hao ilikuwa na nembo iliyobandikwa jina la B/0 Ruth Mtanga male 1.6 Premature – uzao wa Ruth Mtanga mtoto wa kiume mwenye uzito wa kilo 1.6 aliyezaliwa njiti.

Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mwananyamala, Dk. Kariamel Wandi, alipohojiwa kuhusu tukio hilo, aligoma katakata kulizungumzia akiahidi kuzungumza baadaye.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa polisi wameanza uchunguzi ili kubaini wahusika. Alisema pia maiti hao wamehifadhiwa katika mochari ya Mwananyamala.

Ingawa hakuna mtu au watu wanaoshukiwa hadi sasa kuhusika na tukio hilo la kutisha na kusikitisha, lakini wachunguzi wa masuala ya kijamii wanahisi kuwa mchezo huo mchafu umefanyika katika hospitali hiyo.

Kuwapo kwa shuka lenye nembo ya hospitali hiyo lakini pia khanga zilizobandikwa jina la mzazi na maelezo ya kidaktari, ni uthibitisho mwingine kuwa hospitali hiyo kwa namna fulani inahusika na tukio hilo.

Zipo pia hisia kuwa kuna kitu kinafichwa ama na watumishi au uongozi wa hospitali hiyo, kwani kwa kawaida, hata mtoto anapofariki wakati anazaliwa, kuna jinsi ya kumsitiri na si kumtupa kwa kumfukia holela kama walivyofanyiwa watoto hao.

Siku za nyuma, hospitali hiyo imekuwa na sifa mbaya zikiwamo za kunyanyasa wagonjwa, ikiwa ni pamoja na kuwatelekeza, hali ambayo ilimlazinmu aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, William Lukuvi, mwaka jana kuhamisha idadi kubwa ya wauguzi.

Hili litakuwa ni doa lingine kwa hospitali hiyo ambayo ni kimbilio la wanyonge kutokana na kuwa ni hospitali ya Serikali ambayo inahudumia idadi kubwa ya wakazi wa Wilaya ya Kinondoni na hata wilaya jirani.

Hili ni tukio la kwanza la aina yake kutokea Dar es Salaam na pengine nchi nzima katika miaka ya karibuni kutokana na kugundulika ‘kaburi’ la pamoja.

Chanzo:Habari Leo

No comments: