ANGALIA LIVE NEWS
Wednesday, March 2, 2011
Pinda ashauri wafanyabiashara wainunue Dowans
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda ameishauri sekta binafsi inunue mitambo ya Dowans ili isaidie
kupunguza tatizo la umeme nchini huku kesi na mazungumzo mengine yakiendelea.
Alisema hali hiyo inatokana na Serikali kutoweza kununua mitambo hiyo kutokana na kufungwa na Sheria ya Manunuzi ya Umma, hivyo kuishauri Kampuni ya Songas kuinunua mitambo hiyo kunusuru uchumi.
Akijibu maswali ya wafanyabiashara wakubwa kwenye mkutano wa Jukwaa la Uchumi jana Dar es Salaam, waliotaka kufahamu juu ya tatizo la umeme nchini na kukua kwa uchumi kwa miaka mitano ijayo, Pinda alisema licha ya kuwepo tatizo hilo, bado uchumi wa nchi
upo imara.
Pinda alisema jambo la msingi ni kutafuta njia ya kupunguza upungufu wa megawati 160 kwa
kuwashwa mitambo hiyo ya Dowans, baada ya kununuliwa inayozalisha megawati 100 na kubaki na upungufu wa megawati 60 ambazo zitafidiwa na mvua ndogo itakayonyesha.
Katika mkutano huo kulifanyika majadiliano juu ya jinsi Serikali itakavyokuza uchumi kwa miaka mitano ijayo, alisema kama hali hiyo itashindikana, pia kuna uwezekano wa kufanya
mazungumzo na kukodi mitambo hiyo kwa muda kisha kutoa maelezo yatakayosaidia watu kuelewa madhumuni yake.
Alisema baada ya kupunguza tatizo hilo, ndipo jitihada za kupata umeme wa kutosha ziendelee kwa kutumia gesi na makaa ya mawe.
Akielezea kukua kwa uchumi, alisema mapato ya Taifa yameendelea kukua ambapo kwa mwaka 2011 pato la Taifa limeendelea kukua kwa asilimia 7.2 huku mfumuko wa
bei ukitegemewa kushuka kufikia asilimia 5.0 ifikapo Juni mwaka huu.
Aliwahamasisha wawekezaji kuwekeza katika sekta mbalimbali ikiwemo ya kilimo cha umwagiliaji ambapo kuna asilimia 30 ya ardhi zenye kufaa kwa kilimo hicho huku
asilimia moja tu ndiyo inayotumika.
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu alisema benki za Tanzania zina
hali nzuri inayotoa mikopo ya muda mfupi na wako katika mkakati wa kuanza kutoa mikopo
ya muda mrefu.
Benki ya Kilimo itaanza baada ya miezi sita mwaka huu huku wakiwa katika mikakati ya
kuanzisha utaratibu wa benki kukopesha vifaa mbalimbali badala ya fedha.
Kuhusu kushuka kwa thamani ya Shilingi, alikiri kushuka, lakini alisema iko ndani ya viwango, hivyo hakuna tatizo.
CHANZO:HABARI LEO
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment