2nd March 2011
Wachezaji wawili wa Simba, Joseph Owino na Hillary Echessa huenda wakashindwa kuikabili Yanga katika mechi yao ya marudiano ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara itakaofanyika Jumamosi kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Nyota hao wa kigeni waliachwa jijini Dar es Salaam juzi na jana walikuwa wanaendelea na matibabu huku wakisubiri majibu ya vipimo ili hatma yao iweze kujulikana.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Afisa Habari wa Simba, Clifford Ndimbo, alisema kuwa wachezaji wengine wanaendelea na mazoezi chini ya kocha wao mkuu, Mzambia, Patrick Phiri, na wanaamini kwamba wataibuka na ushindi dhidi ya watani zao na hawana hofu juu ya mchezo huo.
"Echessa na Owino walibaki na kesho (leo) jioni ndio majibu ya Owino yanatarajiwa kutoka, ila Emmanuel Okwi amepona na tayari ameshajiunga na wenzake Zanzibar kwa ajili ya kujifua," alisema Ndimbo.
Ndimbo alisema kuwa katika kuhamasisha zaidi watu kujiunga na klabu hiyo, zoezi la kutoa kadi kwa wanachama wapya limefunguliwa ambapo kila muombaji atatakiwa kulipia kiasi cha Sh. 24,000 kama gharama ya kadi na ada ya uanachama pamoja na Sh. 20,000 au zaidi kama mchango wa ujenzi wa uwanja wa michezo wa klabu hiyo unaotarajiwa kujengwa katika eneo la Boko hapa jijini.
Alisema pia uongozi unawakumbusha wanachama wa zamani kulipia ada zao za mwaka na kuchangia ujenzi huku wakisema kuwa atakayetoa fedha zaidi ya Sh. Milioni moja atakabidhiwa cheti maalumu cha kutambua mchango wake.
Alisema pia keshokutwa mwenyekiti wa klabu hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Tabora Mjini, Ismail Aden Rage, atakabidhi bendera na katiba kwa viongozi wa matawi mbalimbali ambayo yatakuwa yamehakikiwa.
Phiri alisema kuwa atafanya kila linalowezekana ili timu yake ishinde na kujihakikishia nafasi ya kutetea ubingwa.
Alisema kuwa maandalizi yake yanalenga pia mechi yao ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika dhidi ya TP Mazembe itakayofanyika Machi 20 mjini Lubumbashi nchini Kongo.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment