ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, March 2, 2011

Gongo la Mboto: Hakuna fidia ya fedha taslimu

2nd March 2011


  Ni kwa waliobomolewa nyumba zao
  Zitajengwa na Shirika la Suma JKT
  Fedha ni kwa vifaa vilivyoharibika tu
Haya ndiyo maisha ya sasa kwa baadhi ya waathirika wa milipuko ya mabomu ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kambi ya Gongo la Mboto.

Wakati kazi ya kuhakiki nyumba zilizoharibiwa na mabomu Gongo la Mboto, iliyotarajiwa kumalizika leo ikiongezewa muda hadi keshokutwa, serikali imesema hakutakuwa na ulipaji wa fedha za fidia mikononi, bali nyumba hizo zitajengwa upya au kukarabatiwa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na kisha kukabidhiwa kwa wamiliki zikiwa zimekamilika.
Fidia pekee ya fedha tasilimu itakayotolewa ni kwa vitu visivyohusiana na ujenzi wa nyumba, ambavyo viliharibiwa na mabomu.
Uamuzi huo umefikiwa na serikali ili kuepuka malalamiko na manung’uniko yanayoweza kujitokeza ya watu kudai kupunjwa fedha za fidia ya uharibifu wa nyumba zao.

Mabomu hayo yalilipuka katika kambi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Gongo la Mboto, jijini Dar es Salaam, Februari 16, mwaka huu na kusababisha vifo vya watu 27, majeruhi zaidi ya 500, wakazi kuzikimbia nyumba zao na mali zenye thamani ya mamilioni ya shilingi kuteketea.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki, alipokuwa akifafanua kwa waandishi wa habari kauli iliyotolewa juzi na Rais Jakaya Kikwete, alipolihutubia taifa katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi kupitia vyombo vya habari. Rais Kikwete alisema ameiagiza JKT kufanya kazi hiyo kupitia shirika lake la uchumi (Suma) ili kuhakikisha maisha ya watu waliokumbwa na maafa hayo, yanarejea kuwa ya kawaida mapema iwezekanavyo.
Sadiki hakutamka waziwazi kwamba wamiliki wa nyumba hizo hawatapewa fedha za fidia ya uharibifu wa nyumba zao mikononi.
Badala yake alisema uamuzi wa serikali kuipa JKT kazi hiyo, ni ili kuepuka malalamiko na manung’uniko yanayoweza kujitokeza ya watu kudai kupunjwa fidia.
“Kitakachofanywa na JKT ni kuirejesha nyumba iliyoharibiwa katika hali yake ya mwanzo. Na pengine kwa kiwango zaidi ya kile cha mwanzo na kukabidhiwa mmiliki. Kama ilikuwa na dari, itarejeshwa,” alisema. Aliongeza: “Nyumba ‘zilizokreki’ (zilizopata nyufa), JKT watazikarabati. Vitu vilivyoathiriwa vitafidiwa kwa utaratibu. Na hicho ndicho kinachofanywa na timu zetu za uthamini. Hakuna ambaye atatupwa.”
Alisema hadi kufikia jana, kazi ya uhakiki nyumba zilizoharibiwa ilikuwa bado ngumu, hali ambayo imewafanya kuongeza muda hadi keshokutwa badala ya leo. Sadiki alisema kinachosababisha ugumu wa kazi hiyo, ni pamoja na kusambaa kwa baadhi ya nyumba zilizoharibiwa na mabomu na hivyo kuwa vigumu kuzifikia kwa haraka.
Sababu nyingine ni nyumba zilizokutwa na timu ya uhakiki zikiwa na nyufa kuwa nyingi, hivyo kuwa vigumu kuthibitika kama nyufa hizo zina uhusiano na mabomu, na pia kuthibitika vitu vilivyoathiriwa na mabomu.
“Hatutaki watu wapuuzwe, tunataka wasikilizwe ili baadaye kusiwe na malalamiko. Kutokana na hilo, huenda (timu ya uhakiki) ikawachukua hadi siku ya Ijumaa (keshokutwa) watakuwa wamemaliza. “Lakini kuna maeneo mengi wanakuta mwenye nyumba hayuko, inabidi warudi tena,” alisema. Alisema hadi kufikia jana, nyumba 69 zilikuwa zimetambuliwa kiwango cha uharibifu zilioupata.
MISAADA ZAIDI YAMIMINIKA
Wakati hayo yakijiri, waathirika wa milipuko hiyo, jana walimwagiwa misaada zaidi.
Miongoni mwa waliotoa misaada jana, ni pamoja na Shirika la Madini la Taifa (Stamico) ambalo lilitoa kilo 100 za mchele, kilo 500 za unga wa sembe, kilo 1000 za mahindi, kilo 500 za sukari na viroba vinne vya sabuni, vyote vikiwa na thamani ya Sh. milioni tano.
Wengine waliotoa misaada ni Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchikavu na Majini Nchini (Sumatra) iliyotoa mafuta ya kula, mchele, sukari, unga na maharage vyenye thamani ya Sh. milioni mbili. Wengine ni Shirika la Posta Tanzania (TPC) ambalo lilitoa magodoro 20, vyandarua 20, mashuka 20, foronya 20, vitenge 40 na khanga 40, vyenye thamani ya Sh. milioni 2.5, Chama cha Wachimbaji Madini chenye wanachama 60 ambao walitoa unga wa sembe, sukari na lishe za watoto, vyenye thamani ya Sh. milioni 11.1.
Wengine ni Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) iliyotoa tani tano za mchele, tani tano za unga, tani tatu za maharage na katoni 50 za mafuta ya kula, vyote vikiwa na thamani ya Sh. milioni 20.
JWTZ YAFAFANUA KIPIGO KWA RAIA
Katika hatua nyingine, JWTZ, imetoa ufafanuzi wa taarifa za askari wake waliodaiwa kufanya fujo na kupiga raia eneo la Gongo la Mboto wiki iliyopita.
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Habari na Mahusiano Makao Makuu ya Jeshi hilo, ilieleza kuwa askari wake mmoja alivamiwa na vibaka usiku wa Februari 24, mwaka huu.
Ilieleza kuwa tukio hilo lilitokea wakati askari huyo, ambaye ni dereva alipokuwa akinunua mahitaji katika eneo hilo, ambapo ghafla alivamiwa na kundi la vibaka. Katika hali hiyo, taarifa hiyo ya JWTZ ilieleza, askari huyo alijaribu kujihami na kuomba msaada kwa watu waliokuwa jirani bila mafanikio.
“Ndipo askari huyo alipopiga simu kambini akiomba msaada. Baada ya muda mfupi, askari wenzake walifika katika eneo la tukio na kumuokoa,” ilieleza taarifa hiyo.
Iliongeza: “Kufuatia tukio hilo askari huyo aliripoti polisi na kupewa RB namba SIK/3030/2011 na sasa polisi wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.” Hata hivyo, taarifa ya JWTZ haikusema ilikuwaje wananchi wanane wakapata ngeu na kuripoti kituo cha polisi cha Sitaki Shari.

MABOMU YALIPULIWA IRINGA
Zoe la siku tano la kuyaharibu mabomu pamoja na milipuko iliyokwisha muda wake katika Kambi ya JWTZ Kikosi cha Mafinga mkoani Iringa, limeanza rasmi katika eneo la Katenge Wilaya ya Njombe.
Kutokana na zoezi hilo, Serikali imewataka wananchi wanaoendesha shughuli za kiuchumi ikiwemo kugonga kokoto, kulima na kuchunga mifugo jirani na eneo la Katenge kutosogelea eneo hilo ili kuepuka kupata madhara wakati wa utekelezaji wa kazi hiyo.
Onyo hilo lilitolewa jana na Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Sara Dumba, wakati akizungumza na NIPASHE.
Kwa mujibu wa Dumba, tayari serikali imekwisha kutoa elimu kwa wananchi waliopo karibu na eneo hilo kwa ajili ya kuchukua tahadhari kutokana na milipuko itakayosikika wakati wa zoezi hilo.
CHANZO: NIPASHE

No comments: