Advertisements

Wednesday, March 16, 2011

Mitambo ya Dowans yadaiwa kuuzwa nje

Baadhi ya mitambo ya Kampuni ya kufua umeme ya Dowans iliyopo ubungo jijini Dar es salaam
Exuper Kachenje
WAKATI Serikali ikiwa mbioni kurekebisha Sheria ya Ununuzi wa Umma kwa kile kinachoelezwa kuwa ni kutaka kuinunua mitambo ya Kampuni ya kufua umeme ya Dowans, kuna taarifa zinazodai kuwa tayari mitambo hiyo imeshauzwa.
Habari zilizolifikia gazeti hili jana zinaeleza kuwa mitambo hiyo imeuzwa nje ya nchi na kinachosubiriwa sasa ni kumalizika kwa taratibu za kimahakama katika kesi ya Dowans dhidi ya Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco) iliyoko Mahakama Kuu ya Tanzania.
Kwa mujibu wa habari hizo, tayari mnunuzi wa mitambo hiyo kutoka Cyprus ameilipa Dowans, lakini ameipa masharti kampuni hiyo kabla ya kuchukua fedha hizo.Katika masharti hayo, kampuni hiyo ya Cyprus inaitaka Dowans ihakikishe kwamba mitambo hiyo inapata


mkataba usiopungua miezi sita wa kuzalisha umeme nchini na ikishindwa, ihakikishe mitambo hiyo imepakiwa ndani ya meli tayari kwa kusafirishwa ndipo iruhusu kuchukuliwa kwa fedha hizo.Mkurugenzi wa Fedha wa Dowans (Tanzania), Stansalus Munai alipoulizwa kuhusu taarifa hizo, hakukanusha wala kukubali: "Mitambo yetu haijakosa soko. Wanaoihitaji ni wengi na ni wanaotaka kuisafirisha nje ya nchi.”
“Wanakuja wengi kila siku wa ndani na nje, mazingira ya huko nyuma yalizuia tusiuze sasa hilo linaelekea kwisha.”
Alipotakiwa kueleza kama watakuwa tayari kuiuza mitambo hiyo kwa Serikali, Munai alisema hawatalazimisha biashara nayo lakini wakienda kwa nia ya kuinunua wataisikiliza na kuifikiria. Hata hivyo, hakuweka wazi bei ya mitambo hiyo.“...Hatutalazimisha biashara na Serikali, hawajaja ila wakija tutawasikiliza. Tutawafikiria kama watu wengine, bei inategemea,” alisema Munai bila kufafanua zaidi.
Chini ya sheria ya mwaka 2004, inayotumika sasa, Serikali hairuhusiwi kununua bidhaa au mitambo ambayo tayari imetumika.Lakini iwapo sheria hiyo ya ununuzi itarekebishwa, itatoa nafasi kwa Serikali kununua mitambo iliyokwishatumika kama hiyo ya Dowans iliyoingizwa nchini mwaka 2006 kwa ajili ya kuzalisha umeme wa dharura baada ya kuwapo kwa ukame uliosababisha kupungua kwa kina cha maji katika mabwawa ya kuzalishia umeme nchini.
Hivi sasa taifa linakabiliwa na upungufu mkubwa wa umeme na wafanyabiashara wanashinikiza mitambo ya Dowans iwashwe ili kupunguza ukubwa wa tatizo hilo.Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo alilithibitishia Mwananchi kuwa Serikali imekwishalijadili kwa kina suala hilo na juzi lilianza kujadiliwa na Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi.
Kamati hiyo inajadili na baadaye kupata maoni kutoka kwa wadau mbalimbali kabla ya kuwasilisha bungeni muswada wa kurekebisha sheria hiyo unaotarajiwa kuwasilishwa katika Mkutano wa Tatu wa Bunge mwezi ujao.
“Jambo hili si la siri. Litajadiliwa kwa uwazi na ninyi waandishi wa habari ni miongoni mwa wadau muhimu. Kwa hivyo waambie na wenzako… Katika mjadala huo, ripoti ya Serikali itasomwa na wadau mtapewa nafasi kuijadili,” alisema Mkulo.
Habari zinasema tayari mawaziri wote wamepewa dokezo kuhusu mkakati huo wa Serikali kushughulikia suala hilo la kubadili sheria ambalo Mkulo alisema ni siri.“Hilo ni ‘confidential’ (siri),” alisema Mkulo alipotakiwa na Mwananchi kufafanua kuhusu maelezo yaliyo katika waraka uliotumwa kwa mawaziri wote. Habari zinasema hatua ya Serikali kutaka kubadili sheria ya ununuzi wa umma, inalenga katika kuifanya iwe huru kununua kitu kilichotumika hasa taifa linapokumbwa na majanga au jambo la dharura.
Sheria ya sasa inayoizua Serikali kutonunua bidhaa au vitu vilivyotumika ilitafsiriwa katika Sheria ya ununuzi wa Benki ya Dunia (WB), inayolenga kuepuka mazingira ya ufisadi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, January Makamba alisema kuwa hatua ya Serikali kutaka kurekebisha Sheria ya ununuzi ya Umma imechelewa kwani ilitakiwa iwe imeshafanyiwa marekebisho siku nyingi.
Alikumbusha kwamba miaka ya nyuma Serikali iliwahi kuiomba kamati hiyo irekebishe sheria hiyo lakini ikaonekana kwamba kilichohitajika ni marekebisho ya kanuni, jambo ambalo alisema lingeweza kufanywa na waziri husika na kutangazwa katika Gazeti la Serikali.
Alisema anaunga mkono hatua ya kurekebisha sheria hiyo akieleza kuwa ina vikwazo vingi na mchakato mrefu. Kwa mujibu wa Makamba, vikwazo na mchakato huo mara nyingi huchelewesha mahitaji husika na wakati mwingine husababisha kupanda kwa gharama za miradi, hivyo kuharibu bajeti za miradi na kuwakwaza wahisani.
“Serikali imechelewa kufanya jambo hili, inasubiri mpaka kuwe na ‘crisis’ (mgogoro), lakini naunga mkono hatua hiyo kwa sababu Sheria ya ununuzi ina vikwazo vingi, mlolongo mrefu. Hii inachangia gharama za mradi kupanda hata kukwaza wafadhili,” alisema Makamba.Alisema Serikali imekuwa ikikiuka sheria hiyo, akitolea mfano wa ununuzi wa ndege zilizokwishatumika.
Mwaka 2008 Kampuni ya Dowans ilitangaza zabuni ya kuuza mitambo yake ya kuzalisha umeme ikiwa ni miezi mitatu baada ya Serikali kusitisha mkataba wake na Tanesco. Baadaye ilielezwa kuwa mitambo hiyo tayari imeuzwa kwa Sh101bilioni nje ya nchi.Dowans ilirithi mkataba wa kuiuzia umeme wa megawati 120 Tanesco kutoka kwa Kampuni ya Richmond Development LLC ambayo ilibainika kuwa ni kampuni hewa. Serikali ilifikia uamuzi wa kusitisha mkataba huo baada ya kuridhika kuwa haukuwa halali wala wenye nguvu kisheria.
Sakata la mkataba kati ya Tanesco na Richmond lilisababisha kuundwa kwa Kamati iliyokuwa chini ya uenyekiti wa Mbunge wa Kyela, Dk Harrison Mwakyembe (CCM). Matokeo ya ripoti hiyo yalisababisha aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa na mawaziri wengine wawili, Dk Ibrahim Msabaha na Mustafa Karamagi, kujiuzulu.

CHANZO:MWANANCHI

No comments: