Advertisements

Sunday, May 15, 2011

'Sangoma’ auawa kwa kukataa ramli

ATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, mganga wa kienyeji wa kijiji cha Kaozye katika Bonde la Ziwa Rukwa wilayani Sumbawanga, Amos Kapufi (38), ameuawa na ndugu wawili baada ya kuwakatalia kuwapigia ramli ya kumbaini mwizi wao wa mpunga. 

Inadaiwa kuwa ndugu hao, Sylvanus (32) na Justine Mwanandeje (28) wakazi wa kijiji hicho, walimwua mganga huyo wakimlazimisha awapigie ramli na kuwakatalia akisema uwezo wake ni wa kutibu wagonjwa na si vinginevyo. 

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa, Isuto Mantage akithibitisha tukio hilo alisema lilitokea Kaozye Mei 10 saa 11 jioni. 


Alisema siku moja kabla ya mauaji hayo, Sylvanus na mdogo wake huyo ambao ni wakulima wa mpunga, waligundua mpunga wao umeibwa shambani, na baada ya kutafuta wezi wao bila mafanikio, walimfuata Kapufi ili awapigie ramli. 

Mganga huyo aliwakatalia akisisitiza kamwe hapigi ramli kwa wateja wake. 

“Vijana hao hawakukubaliana na mganga huyo wakamlazimisha awapigie ramli hali iliyozua ugomvi na mmoja wao kuchukua jiwe na kumpiga mganga huyo kichwani na kumwua papo hapo na wao kutoroka,“ alisema Kamanda Mantage. 

Kwa mujibu wa Kamanda, baada ya msako polisi waliwakamata ndugu hao ambao bado 
wanahojiwa na watafikishwa mahakamani uchunguzi wa awali utakapokamilika. 

Katika tukio lingine, Polisi Sumbawanga inamshikilia mganga mwingine, Emmanuel Sadala (32) mkazi wa kijiji cha Zimba Bonde la Ziwa Rukwa wilayani humo, kwa tuhuma za mauaji yaliyotokana na ramli iliyombaini Thobias Malema (41) kuwa analoga ndugu zake. 

Ilidaiwa kuwa, Thobias aliuawa Mei 12 usiku wa manane na watu wasiofahamika baada ya kumvamia akiwa amelala nyumbani kwake na kumkatakata kwa vitu vyenye ncha kali, hali iliyosababisha kuvuja damu nyingi na kufariki dunia. 

Kwa mujibu wa Kamanda Mantage, uchunguzi wa awali wa Polisi ulibaini kuwa tangu Novemba mwaka jana, kulikuwa na mgogoro kati ya Thobias na mdogo wake, Frank 
Malema (31), baada ya kuugua kwa muda mrefu na kwenda kwa Sadala kupigiwa ramli. 

“Sadala alipopiga ramli alimtaarifu Frank kuwa amerogwa na Thobias na ukatokea mgogoro mkubwa huku Frank akiapa kuwa ipo siku atamwua kaka yake,” alisema Mantage. 

Kwa mujibu wa Mantage, Frank anashikiliwa na Polisi na watuhumiwa wote akiwamo Sadala wanahojiwa na watafikishwa mahakamani uchunguzi wa kesi yao utakapokamilika.

No comments: