ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, June 25, 2011

Mahita aangukia pua Mahakama Kuu


Mkuu wa Jeshi la Polisi Mstaafu, Omar Mahita
Mahakama Kuu ya Tanzania, jana imeitupilia mbali rufaa ya Mkuu wa Jeshi la Polisi Mstaafu, Omar Mahita, na kukuamuru kulipa Sh. 100,000 kila mwezi kwa ajili ya matunzo ya mtoto wake aliyemzaa na mfanyakazi wake wa ndani kisha kumtelekeza.
Mahita alikata rufaa hiyo kwa lengo la kupinga hukumu ilitoyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni jijin Dar es Salaam Septemba 14, mwaka 2009.

Hukumu ya rufaa hiyo ilitolewa jana na Jaji Dk. Fauz Twaib, ambapo alisema kuwa hakubaliani na sababu nne zilizotolewa na Wakili wa Mahita, Charles Semgalawe.
Sababu ya kwanza iliyotolewa na Semgalawe ni kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kinondoni ilikosea kisheria kuhusisha suala la mahusiano kuwa halina ukomo na kwamba kesi hiyo ilifunguliwa nje ya muda.
Jaji Dk.Twaib alisema mrufaniwa, Rehema Shabani, ana haki ya kufungua kesi muda wowote kutokana na sheria kuruhusu hata kama alijifungua baada ya miaka tisa kupita na kwamba kinachotakiwa ni ushahidi wa kweli kuhusiana na mtoto huyo.
Katika sababu ya pili, Semgalawe alisema mahakama ilihitimisha kuwa Mahita alikataa kwenda kupima chembechembe za vinasaba (DNA) wakati jambo hilo halikuwa la kweli.
Jaji Dk. Twaib alisema kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkemia Mkuu, Mahita hakujitokeza kwa siku sita kwa ajili ya kwenda kufanya kipimo cha DNA huku mrufaniwa akiwa anafika mara kwa mara na mtoto wake kwa ajili kufanya kipimo hicho.
Alisema licha ya Mahita kutoonyesha kuwa hakutaka kupima, lakini ushahidi unaonyesha kuwa hakuwa tayari kufanya hivyo.
Jaji alisema sababu ya tatu ni kwamba wakili wa Mahita alikuwa Twalib alipinga uamuzi wa Mahakama ya Kinondoni iliyomtaka alipe Sh. 100,000 kwa mwezi kwa ajili ya malenzi ya mtoto wakati sheria inamtaka ilipie Sh. 100 tu na hata sheria hiyo iliporekebishwa mwaka 2002, kiwango hicho hakikubadilishwa.
Jaji huyo alitupilia mbali sababu hiyo kwa kuwa kiasi hicho hakilingani na hali halisi ya mazingira kwa kuwa gharama za maisha zimepanda, hivyo akamtaka kulipa Sh. 100,000 kwa mwezi.
Sababu ya nne aliyoitoa wakili wa Mahita, alisema kuwa mahakama ilikosea kuamuru kumlipa fidia mrufaniwa toka mwaka 2003 mpaka siku ya hukumu ilipotolewa mwaka 2009.
Hata hivyo, Jaji huyo alipokuwa akihitimisha hukumu yake alieleza kushangazwa kwake na msimamo wa kuhoji maamuzi ya kumlipa fidia mlalamikaji kuanzia mwaka 2003 wakati fidia hiyo ilitakiwa aanze kuilipia tangu mtoto huyo alipozaliwa tena kwa kiasi cha Sh 110,000.
Alisema sababu hizo nne alizozitoa wakili wa Mahita amezitupilia mbali na kwamba anaungana na hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kinondoni.
Awali, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni ilimuamuru Mahita kutoa Sh. 100,000 kila mwezi za matunzo ya mtoto huyo (jina tunalihifadhi) hadi atakapojitegemea, baada ya kubainika kuwa ni baba yake halali.
Kadhalika, mahakama hiyo ilimuamuru Mahita kulipa fidia ya matunzo tangu alipositisha kutoa mwaka 2003 hadi siku iliyotolewa hukumu mwaka 2009 ambazo ni sawa na Sh. milioni 7.2 kwa muda wa miaka sita.
Amri hiyo ilitolewa na Hakimu Mkazi, Susan Kihawa, aliyekuwa anasikiliza kesi hiyo wakati akisoma hukumu hiyo mwaka 2009.
Hakimu Kihawa alisema mbali na Mahita kugoma kwenda kupima DNA, mahakama ilithibitisha na kutambua kwamba ni baba halali wa mtoto huyo na kwamba anastahili kubeba jukumu la kumlea hadi atakapojitegemea.
Aidha, alisema kutokana na mazingira ya baba mzazi (Mahita) kuwa mbali na mtoto wake, ataendelea kuwa chini ya uangalizi wa mama yake Rehema Shabani.
Awali, mahakama hiyo iliamuru Mahita, mtoto huyo na Rehema kwenda kupima DNA ili kuthibitisha uhalali wa baba wa mtoto huyo ambapo Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kiligharamia Sh. 300,000 za kufanya vipimo hivyo baada ya mlalamikiwa kudai kuwa hana uwezo wa kutoa fedha hizo.
Hata hivyo, siku ya kufanya vipimo, Mahita hakwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), lakini mahakama ilithibitisha kuwa ni baba halali wa mtoto.
Mapema Agosti 10, mwaka 2006 kesi hiyo ilifunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, ambapo ilipangwa kusikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Said Msuya.
Hata hivyo, jalada la kesi hiyo lilihamishiwa kwa Jaji Pellagia Khaday (wakati huo akiwa Hakimu Mkuu Mkazi) katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Aidha shauri hilo lilifutwa baada ya Hakimu Khaday kusema kesi hiyo inastahili kusikilizwa katika mahakama ya ngazi ya wilaya na sio Kisutu, ambapo Februari 26, mwaka 2007 Rehema alifungua madai ya matunzo ya mtoto katika Mahakama ya Kinondoni, chini ya usimamizi wa LHRC.
Semgalawe, alidai kuwa Rehema aliacha kazi nyumbani kwa Mahita tangu mwaka 1995 na hakuwa na mawasiliano naye na kuanzia 1996 hakuwahi kuwa na mtumishi wa ndani, hivyo alikanusha kuwa sio baba wa mtoto huyo.
Utetezi huo ulitupiliwa mbali na mahakama ambayo imetambua kuwa Mahita ni baba halali wa mtoto huyo.
Baada ya Jaji Dk. Twaib kumalizika kusoma hukumu hiyo jana, Rehema Shabani, aliwaambia waandishi wa habari kuwa amefurahiwa na uamuzi huo, huku akimshukuru wakili wake, Fredrick Mkatambo, pamoja na LHRC.
Alisema mtoto huyo kwa sasa anasoma kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari ya Ananasifu, Kinondoni jijini Dar es Salaam.
CHANZO: NIPASHE


No comments: