Simba Sports Club
Vital"O FC
Mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati maarufu Kombe la Kagame yanatarajiwa kuanza leo nchini ambapo Simba itashuka dimbani kuwakaribisha mabingwa wa soka wa Burundi, Vital'O, katika mchezo wa pili wa Kundi A utakaofanyika kuanzia saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Mechi ya kwanza, ambayo pia ni ya kundi A, itawakutanisha wawakilishi wa Zanzibar, Zanzibar Ocean View, dhidi ya Etincelles 'Moto' kutoka Rwanda saa 8:00 mchana.
Akizungumza na gazeti hili jana asubuhi ambapo timu yake haikuwa na mazoezi, kocha wa Simba, Moses Basena, alisema kwamba kama wenyeji wamejipanga kufanya vizuri kwenye mashindano hayo na kwamba makosa yote yaliyotokea katika mechi za Klabu Bingwa Afrika na Kombe la Shirikisho yamefanyiwa kazi na huu ni wakati wa kuonyesha uwezo wao.
Basena alisema kwamba mechi zilizopita zilikuwa ngumu kwao kutokana na ratiba zilivyoshtukiza lakini mashindano haya yalikuwa kwenye programu yake hivyo ni nafasi nyingine ya kuonyesha matunda ya mazoezi waliyoyafanya kwa zaidi ya mwezi.
"Timu ni mpya na kila mchezaji anataka kunionyesha kwamba anaweza, tunatarajia kupata matokeo mazuri ili tutimize malengo ya kuchukua ubingwa licha ya kwamba timu zote pia zimekuja Tanzania kwa lengo la kushinda," alisema kocha huyo ambaye amefungwa mechi mbili na kushinda moja tangu ajiunge na timu hiyo baada ya kumalizika kwa msimu wa ligi kuu ya Tanzania Bara, ambapo Simba ilimaliza ikiwa katika nafasi ya pili.
Nahodha wa Simba, Nico Nyagawa, alisema kuwa kama wenyeji huu ni wakati wao wa kupigana na kuhakikisha wanang'ara kwenye mashindano hayo.
"Kila kitu kinakwenda vizuri, kila mchezaji anafahamu kocha nini anataka tufanye, naamini tutarejesha heshima yetu kupitia mashindano haya," alisema.
Kocha wa Vital'O, Yaounde Jean Kagabo, alisema jana mchana kuwa wamekuja kushindana na kushiriki kama ilivyo miaka mingine.
Kagabo alisema kwamba timu yake inaundwa na wachezaji wengi chipukizi wakiwemo watatu wanaocheza katika kikosi cha kwanza cha timu ya taifa ya Burundi ambao wana uzoefu wa mechi za kimataifa. "Hatuiogopi Simba, tumekuja kushindana na si kusindikiza, tutaonyesha uwezo wetu uwanjani," alisema kocha huyo.
Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka la Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Nicholas Musonye, alisema jana kuwa maandalizi ya mashindano hayo yamekamilika na timu ya Red Sea kutoka Eritrea iliongezwa baada ya kupata usafiri wa ndege ambao ulisimama kwa muda nchini kwao kufuatia volkano iliyokuwepo angani.
Musonye alisema kuwa timu hiyo imepangwa katika Kundi A na kuongeza kuwa kundi hilo sasa litatoa timu tatu kwenda hatua ya robo fainali wakati Kundi B na C kila moja litatoa timu mbili na nyingine itakayokuwa na matokeo bora kucheza hatua hiyo ya pili.
Alimtaja Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Emmanuel Nchimbi, kuwa ndiye mgeni rasmi atakayefungua mashindano hayo leo na fainali zake zitachezwa Julai 10.
Mabingwa watetezi wa mashindano hayo ni APR ya Rwanda iliyokuwa mwenyeji wa michuano iliyopita katika jiji la Kigali.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment