Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, amesema gari la serikali alilokabidhiwa kwa ajili ya kutumia kutokana na wadhifa wake Kibunge, amelikabidhi kwa dereva aliyekabidhiwa na Ofisi ya Bunge.
Mbowe, ambaye pia ni Mbunge wa Hai (Chadema) na Waziri Mkuu Kivuli, alisema hayo alipoulizwa na NIPASHE katika viwanja vya Bunge, mjini hapa juzi usiku.
Alisema alilirejesha gari hilo muda mfupi baada ya kutangaza uamuzi wake huo mbele ya waandishi wa habari, muda mfupi baada ya Bunge kupitisha bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha wa 2011/2012.
Uamuzi huo ulichukuliwa na Mbowe, kutekeleza kwa vitendo msimamo wa Chadema wa kukataa wabunge wake kuchukua posho za vikao vya Bunge na kupinga matumizi ya mali za umma bila tija.
“Siwezi kutoa msimamo wangu ule kwa waandishi wa habari halafu leo niendelee kutumia lile gari. Gari langu si unaliona lile pale,” alisema Mbowe, huku akimuonyesha mwandishi mahali gari lake binafsi lilipokuwa limeegeshwa katika viwanja vya Bunge.
Alipotakiwa na NIPASHE kueleza utaratibu alioutumia kulirejesha gari hilo, Mbowe alisema alifanya kama alivyokabidhiwa awali.
Alisema baada ya kuchaguliwa kuwa Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, hakupewa barua wala kusainishwa mahali popote nilipokabidhiwa gari hilo.
Alisema badala yake, alionyeshwa gari hilo pamoja na dereva wa kuliendesha.
“Nilipokuwa nikihitaji kulitumia, naenda tu pale, dereva anakuja. Sijui anatoka wapi, wala sijui yanatoka wapi,” alisema Mbowe.
Swali hilo la NIPASHE kwa Mbowe, linafuatia kauli iliyotolewa na Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel, ambaye Jumatano wiki hii, alisema ofisi yake haijapata barua yoyote kutoka kwa Mbowe inayoeleza uamuzi wake wa kurejesha gari hilo kwa Ofisi ya Bunge.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment