ANGALIA LIVE NEWS

Monday, July 11, 2011

Wanafunzi wa kike watelekezwa gesti

WANAFUNZI wawili wa kike wa kidato cha pili katika sekondari ya Enyeitu mkoani Arusha, wametelekezwa katika nyumba ya kulala wageni Dar es Salaam kwa mwezi mmoja sasa. 

Wasichana hao wakazi wa Mianziani, Arusha, walifika Dar es Salaam Juni 4 wakifuatana na mwanamume anayejulikana kwa jina la Rwaka au Swai. 

Mwanamume huyo aliwafikisha katika nyumba hiyo ya Flamingo iliyopo Nzasa A Mbagala katika wilayani Temeke. 

Wanafunzi hao Neema Abel (17) anayedai anaishi na mjomba wake, Amos Michael na Tatu Salim (16) aanayeishi na dada yake Aisha Salim, walifika katika nyumba hiyo siku hiyo saa nane usiku na kupokewa na mhudumu Zainabu Abdallah. 


Mwandishi wa habari hizi alifika katika nyumba hiyo ya kulala wageni juzi na kuwakuta wanafunzi hao wamekaa nje kama wapo nyumbani tena wakicheza bao na baadaye akazungumza nao. 

Awali, mhudumu huyo alidai kuwa mwanamume huyo aliwaandika katika daftari la wageni wanafunzi hao kuwa ni Aisha Salim (Tatu) na Angela Amos (Neema) ambaye alidai mwanamume huyo ni baba yao mdogo na walifika naye jijini Dar es Salaam kwa lengo la kutembea. 

Alisema, baba huyo alikuwa akifika kila siku katika nyumba hiyo na kuwapa fedha za chakula na kulipia gharama ya chumba namba nane walichokuwa wakiishi kwa wiki tatu. 

Zainabu alisema, baadaye walishangaa kutomwona huyo mtu na hivyo wasichana hao wakashindwa kulipia chumba na chakula ndipo wakafichua kuwa hakuwa baba yao na amewatelekeza na wanadaiwa Sh 35,000 za chumba. 

Mabinti hao wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili, walidai kuwa, mwanamume huyo ambaye ni mtu wa makamo, alikutana nao Arusha na kuwa marafiki wa kawaida.

Tatu alisema, baada ya kufunga shule, baba huyo aliwaambia waje Dar es Salaam kuona mji, ndipo naye akamtafuta rafiki yake, Neema, ambaye wanasoma wote shule moja na kutorokea Dar es Salaam. 

Alisema, walipofika jijini, mwanamume huyo aliwaambia waseme kuwa ni baba yao mdogo na kuwaacha kwenye nyumba hiyo naye akaenda kwa mkewe, na akawa akifika mara kwa mara akiwa na rafiki yake na kuwaachia matumizi. 

Alisema, siku moja alifika na kumtaka kimapenzi alipokataa, ndipo alikawaambia kuanzia siku hiyo watajua wenyewe watalala wapi, kula wapi na hata nauli ya kurudi Arusha. 

Alisema, kuanzia siku hiyo wamekuwa wakipika chakula pamoja na wahudumu wa nyumba hiyo, huku bado wakiwa na deni la Sh 35,000 na bila kusema fedha wanazochanga kwa ajili ya chakula wanazipata wapi. 

Angela alisema, wanachohitaji sasa ni nauli ya kuwarudisha Arusha, ili kuendelea na masomo, kwa kuwa shule wanayosoma ilifunguliwa jana na wamejifunza kutokana na makosa waliyofanya. 

Baadhi ya wafanyakazi wa nyumba hiyo, walidai wasichana hao walisitishiwa huduma baada ya mwanamume huyo kuwakuta wakiwa na vijana wadogo na baada ya kusitishiwa huduma, wamekuwa wakitoka usiku na kwenda kwenye kumbi za starehe ili kupata fedha za kujikimu.


Habari Leo

No comments: