*Wampongeza kusaini muswada mabadiliko ya katiba
*Wasema uamuzi huo umezingatia kilio cha Watanzania
*Sasa waahidi kumuunga mkono hatua zote za utekelezaji
Na Peter Mwenda
CHAMA cha Wananchi (CUF), kimeridhia na kupongeza hatua ya Rais Jakaya Kikwete kusaini muswada wa kuratibu maoni ya kutekeleza Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya 2011. Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Bwana
Julius Mtatiro, alisema ujumbe wa chama hicho ulikwenda Ikulu kuonana na Rais Kikwete sambamba na kupongeza hatua ya Serikali kukubali madai ya muda mrefu ya Watanzania kutaka Katiba Mpya.
Alisema katika Ilani ya Uchaguzi wa CUF mwaka 1995, 2000, 2005 na 2010 ilikuwa na madai ya kutaka Katiba Mpya pamoja na Tume Huru na Uchaguzi ambapo madai hayo ndio yalichangia kufanyika maandamano ya amani yaliyoitishwa na chama hicho Januari 27,2001.
“Tunapofikia hatua ya Rais Kikwete kukubaliana na madai ya wananchi, hatua budi kumpongeza na kumuunga mkono katika hatua zote za utekelezaji wa suala hili muhimu katika historia ya nchi yetu,” alisema Bw. Mtatiro.
Alisema mapendekezo waliyowasilisha kwa Rais Kikwete, wameomba uteuzi wa Makamishna wa Tume ya Katiba na sekretarieti yake, wateuliwe na Rais Kikwete kwa kushauriana na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Dkt. Ali Mohammed Shein.
Alisema Makamishna na sekretarieti hiyo wawe watu waadilifu, wanaoheshimika mbele ya jamii na wenye ujuzi na uzoefu wa kutosha katika masuala ya katiba wakiwa na uelewa mpana wa mambo ya sheria, siasa, uchumi na maendeleo.
Bw. Mtatiro alisema pia CUF inapendekeza wajumbe wa Sekreterieti ya Tume ambao kwa mujibu wa Sheria watateuliwa na Waziri wa Katiba na Sheria wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Bi. Celina Kombani na Waziri wa Katiba Zanzibar, wawe watu wenye sifa na vigezo sawa na Makamishna wa tume.
Alisema CUF imemwomba Rais Kikwete baada ya kupokea hadidu za rejea za maoni ya wananchi, yasipelekwe moja kwa moja kwa rais badala yake tume itoe hadharani na kuzichapisha moja kwa moja katika vyombo vya habari.
Aliongeza kuwa, pia kuwepo upana usio na vikwazo kwa wananchi kutoa maoni yao kwa sababu wao ndiyo watakaoihodhi na kuimiliki katiba, ila wafanye hivyo kwa njia ya amani na utulivu na kuondoa dhana potofu kuwa lengo la serikali ni kubana uhuru wa wananchi katika kutoa mapendekezo.
Bw. Mtatiro alisema CUF imependekeza Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), zinanyiwe marekebisho kuwa Tume Huru kabla ya 2014, ili zisiweze kutiliwa shaka katika matokeo ya kura.
“Vyama vya siasa haturidhiki wala hatukubaliani na mfumo wa sasa wa NEC kuwatumia Wakurugenzi wa Halmashauri na wasaidizi wao kuwa ndiyo wasimamizi wa uchaguzi katika wilaya na majimbo.
Aliongeza kuwa sheria ya uchaguzi zifanyiwe marekebisho ili kuweka muundo mpya wa Tume ya Uchaguzi na sekreterieti yake ambapo tume ikiendelea kukusanya maoni, mchakato wa kufanya marekebisho ya katiba sasa na sheria za uchaguzi uanze kwa kushirikisha serikali, wadau wa vyama vya siasa na kiraia.
Alisema CUF inapendekeza marekebisho ya kifungu 6(4) kuondoa sharti linalokataza kiongozi wa chama cha siasa ngazi ya Taifa, Mkoa na Wilaya kuteuliwa kuwa mjumbe wa Tume ya Katiba kwa sababu kazi hiyo inahitaji watu wazoefu katika mambo ya siasa.
Kifungu 9(2) CUF wamependekeza maeneo yaliyotajwa kuanzia kifungu (a) hadi (I), yasiwekwe vikwazo wakati wananchi wakitoa maoni yao na wawe huru kutoa maoni yote waliyonayo ambayo itakuwa ni jukumu la tume kuyaratibu na kuyakusanya.
Alisema pia CUF imependekeza kuwa kifungu 32, kiwango cha kura za wananchi kuhalalisha Katiba Mpya, kibadilishwe kutoka zaidi ya asilimia 50 kwa Tanzania Bara na 50 kwa Tanzania Zanzibar hadi theluthi mbili za kura za ndiyo.
Aliongeza kuwa, walipendekeza kifungu cha 33 kifanyiwe marekebisho ili Tume ya Katiba ivunjwe mara baada ya kukamilisha kazi yake, kukabidhi ripoti na rasimu ya Katiba Mpya kwa Rais.
“Kama kila mjumbe mmoja analipwa sh. 500,000 kwa siku wakati wamekamilisha kazi yao, huo ni ubadhirifu wa fedha za umma, wakikamilisha kazi tume hiyo ivunjwe,” alisema Bw. Mtatiro.
Alisema CUF imetoa mapendekezo hayo kwa kuzingatia kuwa, ilishiriki katika muswada huo bungeni na kasoro walizogundua na kuziwasilisha zitafanyiwa marekebisho.
Bw. Mtatiro alisema kutokana na maafikiano waliyofikia, CUF hawataitisha maandamano ya kulazimisha mapendekezo hayo yakubaliwe
Majira
No comments:
Post a Comment