ANGALIA LIVE NEWS

Monday, December 5, 2011

Sitta ajitosa kubeba zigo la mgogoro wa Arusha

Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, amekubali kubebeshwa mzigo wa kuwa chachu ya kusuluhisha mgogoro wa umeya wa Halmashauri ya Jiji la Arusha.
Hata hivyo, Sitta ametoa ushauri binafsi kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kupunguza ukorofi kupitia kwa Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema.

“Napenda kumwomba Lema na wenzake wa Chadema kidogo wapunguze ukorofi…watu vijijini kidogo wanashindwa kuwaelewa kwa sababu chama kinachotarajia kushika madaraka kidogo kiwe na muonekano wa kushika uongozi na sio kufanya maandamano kila siku, vinginevyo, mtaendelea kupata kura za mijini tu, huo ni ushauri wangu,” alisema Sitta jana mjini hapa wakati wa harambee maalum ya kuchangia ujenzi wa Kanisa Kuu jipya la Kiaskofu katika Parokia ya Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu iliyoko katika Jiji la Arusha
Sitta alisema kuwa amekubali kuwa chachu ya kusaidia juhudi za upatanishi kutokana na suala hilo kuwa kwa Waziri Mkuu.
Mgogoro huo uliibuka baada ya Chadema kupinga matokeo ya umeya mwishoni mwa mwaka jana, kwa madai kuwa taratibu zilikiukwa hadi sasa chama hicho hakijamtambua meya.
Madiwani wake watano waliomtambua meya huyo na kufikia mwafaka kwa kugawana nafasi za uongozi wa halmashauri ya Jiji hilo walivuliwa uongozi na Kamati Kuu.
LEMA, MEYA WASALIMIANA, WASHIKANA MIKONO
Kwa kuanzia, Sitta amewafanya mahasimu wakubwa katika mgogoro huo, Mbunge Lema na Meya wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Gaudence Lyimo (CCM), kushikana mikono na kusalimiana.
Mahasimu hao kwa nyakati tofauti, walisema imekuwa ni mara ya kwanza kwao kupeana mikono tangu mgogoro wa umeya ulipozuka mwishoni mwa mwaka jana.
RC: SINA UGOMVI NA LEMA
Kabla ya kushikana mikono kati ya Mbunge na Meya, tendo hilo lilifanyika kati ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo na Lema, ambapo mkuu wa mkoa alisema tangu ateuliwa na Rais kushika wadhifa huo mkoani hapa hivi karibuni, jana ndio ilikuwa mara yake ya kwanza kukaa jukwaa moja.
“Leo (jana) ni mara ya kwanza kwangu kukutana ‘live’ na Lema, namkaribisha ofisini kwangu tukapige maneno,” alisema na kuahidi kuchangia Sh. 500,000.
KAULI YA LEMA
Akikwepa kumtaja kwa cheo cha umeya, Lema, alisema hana ugomvi binafsi Lyimo kama diwani wa Kata ya Olorien, isipokuwa ugomvi wake ni mfumo uliomwingiza kuwa meya kwamba haukuwa halali.
KAULI YA MEYA
Kwa upande wake, Lyimo ambaye alitoa fedha taslimu Shilingi milioni moja, alisema anashukuru tukio hilo kuwakutanisha, na kwa mara ya kwanza wameweza kushikana mikono . Tumeshikana mikono leo licha ya mambo mengi mabaya ambayo amenifanyia, ninamsamehe na yote ninamwachia Mungu ndiye atakayeamua,” alisema Meya Lyimo.
Baada ya kusema hivyo, baadhi ya waumini walianza kuguna na wengine kuzomea kidogo kama ishara ya kutoridhika na kauli yake.
Mapema kabla ya kuwasimamisha Lema na Lyimo mbele ya jukwaa, Sitta alisema, “aliposimama hapa Lema, aliniomba nisaidie upatanishi wa umeya wa Arusha…tunaanza hii safari pamoja kwani Injili ya Mathayo imesema, ‘Heri waliowapatanishi….’ hivyo, nachukua fursa hii kusema nitakuwa chachu ya kupatanisha mgogoro huu.” Kukubali kwake kunafuatia ombi la Lema, ambaye alichangia Shilingi milioni moja, alimuomba Sitta kusaidia kutafuta ufumbuzi wa mgogoro huo.
“Najua mazungumzo ya kutafuta mwafaka wa umeya Arusha yamefikia ngazi ya juu na sasa yapo kwa Waziri Mkuu, nakuomba Mheshimiwa Sitta usaidie kuhamasisha ili mazungumzo hayo yasaidie kupata muafaka ili tutakapoanza mwaka mpya tuanze na mambo mapya,” alisema Lema.
Alisema anapenda haki na ataendelea kuitafuta haki kwa sababu anachukia dhambi.“Naomba Mheshimiwa Sitta, harakisha ili mazungumzo ya kutafuta muafaka yafikie mwisho,” aliongeza.
Katika hatua nyingine, Lema aliwataka viongozi wa dini kuhakikisha kwamba madhabahu hayatumiki na watu wenye fedha kujipatia nafasi za uongozi katika uchaguzi mkuu ujao.
“Mimi ninapenda ukweli na haki kama viongozi wa dini hamtakuwa imara, watu wanaweza kutumia madhabahu kuingia kwenye nafasi za uongozi,” alisema na kuongeza: “Wapo watu wenye fedha nyingi sana wanaweza kutumia madhabahu ili waingie ikulu.”
Wakati wa kuanza kwa harambee hiyo, Sitta, ambaye ni Mbunge wa (Urambo Mashariki CCM), alikubali kubebeshwa mzigo huo.
SITTA: SIKUJA KUJISAFISHA
Aidha, alisema hatarajii kutumia jukwaa hilo kuomba radhi au kujisafisha kwa sababu hana sababu ya kufanya hivyo kwani yeye ni mwaminifu na wananchi wanatambua hilo.
“Wananchi mnawatambua viongozi wenu ambao ni waadilifu na pia mnawatambua wale wengine (hakuwataja), sitarajii kulitumia jukwaa hili kwa kufanya hivyo ingawa ninayo mambo mengi ya kisiasa ya kuzungumza,” alisema na kuongeza: “Wananchi mnatujua hata tukisemaje.”Hata hivyo, wakati akiwatambulisha viongozi waliokuwa jukwaani, alipofika kwa Lema alisema huyu ni kijana machachari sana na kama alivyokuwa yeye (Sitta) enzi zake alikuwa machachari hivyo hivyo na akamtaka kuendelea kutetea haki.
Aliwataka Wakristu wenzake kujihadhari sana na dhambi ya unafiki na kusengenyana.
Wakati akisema hayo Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Lazaro Nyarandu alikuwa ndio ameingia muda sio mrefu na kukaa jukwaani hapo, na Sitta akasema Lema ni machachari kama alivyokuwa Nyarandu.
Alisema wao sasa ni wazee na hivyo wanajivunia kuwaachia vijana ambao ni waadilifu ili kuliongoza taifa na kulirejesha kama lilivyokuwa enzi za utawala wa Rais wa kwanza, Marehemu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Nyalandu ambaye alifika katika harambee hiyo alikuwa akitokea kwenye shughuli kama hiyo katika Kanisa la St. James ambako Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alialikwa kuwa mgeni rasmi.
Nyalandu alichangia harambee hiyo Sh. milioni mbili na akaahidi kiasi kingine kilichosalia ili kifike Shilingi milioni 10 atawasilisha nyumbani kwa Sitta Dar es Salaam. Membe alitoa mchango wa Sh milioni moja na ulikabidhiwa kwa Mwenyekiti wa kamati ya Ujenzi wa kanisa hilo, Valerian Shayo.
WATU MASHUHURI WACHANGIA
Katika harambee hiyo, familia ya Sitta ilitoa kiasi cha Shilingi milioni mbili; Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alitoa ahadi ya Shilingi milioni tano; Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi, alitoa ahadi ya Shilingi 10 na Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye ahadi ya Shilingi milioni moja.
Wengine aliwataja kuwa ni wabunge kutoka Mkoa wa Tabora, Kigwangalah na Aden Rage wote walitoa ahadi ya Shilingi milioni moja kila mmoja wakati Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji), Dk. Mary Nagu, alitoa ahadi ya Shilingi 500,000.
Wengine waliochangia ni Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Raymond Mushi pamoja na wenzake Sh. milioni mbili, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Aisha Nyerere Sh. milioni tano; Elias Mshiru, Sh. milioni moja na Aloyce Gonzaga Sh. milioni moja na harambee ilikuwa ikiendelea hadi jioni.
Katika harambee hiyo, jumla ya Shilingi 143,418,500 zilipatikana fedha taslimu zikiwa Sh. 73,736,500 na ahadi Sh. 69,682,000.
Ujenzi wa kanisa hilo hadi kukamilika kwake mwaka 2013, unatarajiwa kutumia zaidi ya Sh. bilioni sita.
CHANZO: NIPASHE

No comments: