ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, December 4, 2011

TAARIFA KWA UMMA
Hivi karibuni kumekuwa na taarifa iliyotolewa na baadhi ya Vyombo vya Habari na baadhi ya Wabunge kuwa posho ya Vikao vya Bunge imeongezeka kutoka Sh.70,000/= hadi 200,000/=.

Suala la mabadiliko ya Posho ya Vikao vya Bunge lilijitokeza katika Mkutano wa Wabunge, tarehe 8 Novemba, 2011 walipoiomba Serikali iangalie upya suala hili kwa lengo la kuboresha. Hadi tunapotoa tangazo hili, Serikali haijatoa taarifa iwapo Posho hiyo imeongezeka kutoka Sh.70,000/= hadi 200,000/=.

Tunasikitika na kushangaa sana kwa kauli hii kwani ina lengo la kujenga chuki baina ya Wabunge na Wananchi wao waliowapigia kura.

Kwa mujibu wa Waraka wa Rais kuhusu Masharti ya Mbunge uliotolewa tarehe 25 Oktoba, 2010 wenye Kumb. Na. CAB111/338/01/83 na kusainiwa na Katibu Mkuu Kiongozi, pamoja na stahili zingine, Mbunge anastahili kulipwa Posho ya Kikao ambayo ni sawa na Sh.70, 000/= kwa kila kikao na masharti hayo hayajafanyiwa marekebisho wala kufutwa.

Kwa hiyo, taarifa hiyo iliyotolewa siyo sahihi na imelenga kuleta chuki baina ya Wabunge na Wananchi. Endapo itatokea mwenye mamlaka kupitisha kiwango kipya cha Posho ya Vikao vya Bunge, itakuwa ni uamuzi kama uamuzi mwingine anaoutoa wa kuwaongezea Watumishi wa umma mishahara, posho, marupurupu na mafao mengine.

Ofisi ya Bunge inahidi kufanya kazi kwa ushirikiano na Vyombo vya Habari kwa lengo la kuleta ufanisi mzuri na kujenga mahusiano mazuri ya kuaminiana kati ya Wabunge, Vyombo vya Habari na Wananchi.

Imetolewa na:

Dr. Thomas D. Kashililah
KATIBU WA BUNGE

No comments: