ANGALIA LIVE NEWS

Monday, January 2, 2012

Diwani aliyechomwa Kisu afariki dunia

Tusekile Mwakyoma Enzi ya Uhai Wake
Diwani wa Chama cha Kata ya Mtibwa, wilayani Mvomero, mkoa wa Morogoro Chadema, Tusekile Mwakyoma(28), amefariki dunia, baada ya kuchomwa kwa kisu na mchumba wake.
Diwani huyo alifariki jana majira ya saa 6:00 mchana katika  Hospitali ya  misheni ya Bwagala alikokuwa amelazwa, baada ya kuchomwa na kisu na mchumba wake  kwa kile kinachoelezwa kuwa wivu wa mapenzi.


Marehemu Tusikile anadaiwa kuchomwa na kisu Desemba 26, mwaka jana katika ziwa la kushoto na mchumba wake ambaye ni Mkurugenzi wa Mafunzo na Uenezi wa Chama cha Chadema katika wilaya ya Mvomero, Songa Mgweno.
Mtuhumiwa ambaye ni mkazi wa kijiji cha Kilimanjaro, inadaiwa kuwa baada ya kufanya kitendo hicho alitoweka.
Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (RCI) Mkoa wa Morogoro, Hamis Selemani,alithibitisha kutokea kwa kifo cha diwani huyo na kueleza kuwa Jeshi la Polisi linaendelea kumtafuta mtuhumiwa huyo ili afikishwe mahakamani.
Kwa mujibu wa ofisa huyo, kabla ya kufikwa na mauti hayo, marehemu alieleza kuwa siku ya tukio, mchumba wake Mgweno alimpigia simu saa mbili usiku aende nyumbani kwake katika kijiji cha Kilimanjaro ili akachukue fedha alizokuwa akimdai Shilingi 200,000.


Akisema kuwa marehemu likwenda huko na kuamua kulala na ilipofika alfajiri alimuamsha na kumuuliza amefanya juhudi gani kuhakikisha wazazi wake wanakubali amuoe ambapo marehemu alimwambia kuwa hana jibu.


“Tuliendelea kulala lakini baada ya muda aliendelea kunipapasa nikasikia maumivu makali chini ya ziwa la kushoto baada ya kujichunguza nikaona kisu kikininginia,“ alisema marehemu wakati alipokuwa amelazwa.


Marehemu alieleza kuwa Mgweno aliendelea kumkaba koo na kuchomoa kisu hicho na kutaka kumpiga kingine, lakini alijitahidi kumdhibiti huku akipiga kelele kuomba msaada ambapo ndugu wa mwanaume waliamka na kwenda chumbani kwao kutoa msaada.


 Alieleza kuwa ndugu wa Mgweno waliamua kumchukua na kumpeleka marehemu katika hospitali ya misheni ya Bwagala ambapo alipatiwa matibabu, lakini hali yake iliendelea kuwa mbaya mpaka alipofariki dunia.


Akizungumza kwa simu na gazeti hili, Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero, Jonas Zeland, alithibitisha kifo cha diwani huyo na kueleza kuwa alipata taarifa hizo kupitia kwa wazazi wa marehemu.


Zeland alisema kuwa anawasiliana na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero, Sara Linoma, kwa ajili ya kusafirisha mwili wa marehemu leo kuelekea mkoani Mbeya kwa ajili ya mazishi.

CHANZO: NIPASHE

No comments: