ANGALIA LIVE NEWS

Monday, January 2, 2012

Simba watua Z`bar bila Boban, Okwi

Simba Sports Club

Mabingwa watetezi wa Kombe la Mapinduzi, Simba walianza kutua visiwani Zanzibar jana kwa ajili ya kushiriki katika mashindano yanayotarajiwa kuanza leo ya Kombe la Mapinduzi bila nyota wao Haruna Moshi Boban na Mganda Emmanuel Okwi.
Akizungumza na NIPASHE kutokea Zanzibar jana, Afisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga, alisema kuwa wachezaji wao waliotangulia walitua salama Zanzibar majira ya saa 9:05 alasiri, ambapo katika msafara huo walikuwemo wachezaji 21 na viongozi watano.
Kamwaga alisema kuwa Boban, Okwi na Ulimboka Mwakingwe ni miongoni mwa wachezaji wengine watano walioshindwa kuongozana na wenzao kutokana na sababu mbalimbali.
"Tupo na wachezaji 21, lakini kuanzia kesho (leo), wachezaji wengine tuliowaacha watakuja na kuungana na wenzao," alisema Kamwaga.

Aliongeza kuwa beki wao wa kati Victor Costa ‘Nyumba’, Boban na Ulimboka wanatarajiwa kuungana na wenzao visiwani Zanzibar leo.
Alisema kuwa kipa Wilbert Mweta ameshindwa kuondoka naye kwa kuwa amekwenda nyumbani kwao kwenye msiba wa kaka yake wakati mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda, Emannuel Okwi, bado yupo nchini kwao alikokwenda kwa mapumziko.
Hata hivyo, Kamwaga alisema kuwa Okwi anatarajiwa pia kuungana na wenzake visiwani Zanzibar kwa ajili ya kutetea taji la michuano hiyo.
"Okwi alikubaliana na uongozi kuwasili nchini baada ya mwaka mpya. Tumewasiliana naye na hivyo atawasili wakati wowote," aliongezea Kamwaga.
Simba itaanza kutupa karata yake kesho kwa kucheza usiku mechi yao ya utangulizi dhidi ya Jamhuri ya Pemba. Mechi nyingine ya Kundi lao la B kesho itakayoanza kwa kuchezwa jioni itakuwa ni kati ya Miembeni United na KMKM.
Simba walitwaa ubingwa wa michuano iliyopita baada ya kushinda 2-0 katika mechi ya fainali dhidi ya mahasimu wao wa jadi, Yanga.
Kama ilivyokuwa katika michuano iliyopita, mashindano ya mwaka huu pia yanafanyika kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar na Simba wanatarajia kuyatumia kujiandaa na mzunguko wa pili wa ligi ya Bara na pia kujiandaa kwa mechi yao ya awali ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Kiyovu ya Rwanda.
CHANZO: NIPASHE

No comments: