TUMSHUKURU Mungu pamoja marafiki kwa kuruhusu neema yake kwetu, hatimaye tumefanikiwa kuuona mwaka mpya wa 2012! Furaha ilioje? Ahsanteni wote mlionitumia meseji za Heri ya Mwaka Mpya, ambao hamkubahatika kufanya hivyo msijali, nipo pamoja nanyi.
Kabla sijaendelea na mada yetu, napenda kuwashauri marafiki zangu, tutumie udhaifu wetu wa mwaka 2011 na kufanya marekebisho makubwa mwaka huu. Tukianza na maisha yetu ya kawaida. Tunapaswa kuhakikisha kwamba, mwaka huu unakuwa na mafanikio makubwa zaidi.
Tuboreshe ndoa, familia na uhusiano na wenzi wetu. Migogoro isiwe na nafasi kabisa katika maisha yetu kwa mwaka huu. Sijajua wewe umejiandaaje, lakini kauli mbiu yangu ya mwaka huu ni; 2012 ni mwaka wa kazi, mwaka wa mafanikio!
Baada ya hayo, sasa tunarudi moja kwa moja kwenye mada yetu ya msingi. Naamini itabadilisha mtazamo wako, hasa wewe ambaye upo mbioni kuingia kwenye ndoa. Wiki jana nilisema, lazima mwenzi ambaye unatarajia kuingia naye kwenye ndoa, awe mwanamke/mwanaume wa ndoto zako.
Pia, nilizungumzia kigezo cha sura na umbile. Yupo rafiki yangu mmoja aliyechangia kwenye mtandao wetu, alisema sura ni kigezo kikuu cha kuchagua mwenzi. Alisema: “Shaluwa nakubaliana na mada yako, imenisaidia sana na itawabadilisha wengi. Yote sawa, lakini hapo kwenye kigezo cha sura napingana na wewe.
“Huwezi kuishi na mtu ambaye hakuvutii, lazima awe mzuri, halafu hayo mambo mengine yatafuata.”
Marafiki zangu, naomba kuweka hapa sawa kidogo; mapenzi hayana uhusiano wowote na sura au umbile la mtu. Nilipotaja kigezo cha awe mwenzi wa ndoto zako, maana yake awe ni yule ambaye ukimuona moyo wako unaridhika.
Huwezi kuridhishwa na mtu ambaye humpendi. Nimesema sura si kigezo, lakini ndugu zangu, lazima mkumbuke kwamba, inawezekana wewe unaye girlfriend wako, unaamini ni mzuri sana, lakini kumbe washkaji wanakushangaa! Wanaona unatoka na mwanamke asiye na mvuto. Kifupi mzuri utamuona wewe. Utamkubali wewe. Unaridhika naye wewe! Mmeelewa marafiki? Sasa tuendelee...
ANAJUA MAPENZI?
Ndugu zangu, msinielewe vibaya katika kipengele hiki, msije mkadhani nahamasisha ngono kabla ya ndoa. Hapa namaanisha mapenzi kwa maana ya upendo.
Je, mwenzi wako mtarajiwa ni faraja kwako? Anakusaidia unapokuwa na matatizo makubwa ya kiafya? Yupo nawe bega kwa bega katika maswaiba yanayokukuta? Lazima awe na mapenzi ya dhati na wewe.
Lazima mwenzi wa maisha yako awe anakupenda kweli kweli. Ambaye anaweza kuifanya siku yako kuwa bora. Ndugu zangu, unaweza usione umuhimu wa jambo hili, lakini nataka kuwaambia kwamba, mwenzi ambaye hata kutumia neno baby, sweetie, mumy, dear, d na mengineyo ni shida, ni tatizo.
Unatakiwa kuwa na mtu ambaye ukiwa na matatizo kazini, anakuambia: “Usijali baby, yataisha. Nipo kwa ajili yako. Mimi ndiyo faraja yako.”
Dalili za mwenzi wa aina hii utaziona mapema sana. Anza kumfuatilia kuanzia sasa hivi utagundua. Lazima awe na maneno matamu ambayo yatakutuliza jazba zako wakati ukiwa na mambo binafsi yanayokukwaza.
Nawe ambaye unatarajia kuingia kwenye ndoa na mwenzako, jifunze kuwa na maneno matamu. Kuwa mtu wa karibu na mwenzako muda wote, sikiliza shida zake, kuwa mshauri wake mkuu. Hapa nasisitiza, sizungumzi na jinsi moja. Wote wanahusika.
KWANZA AKUPENDE...
Ni lazima mwenzi ambaye unatarajia kuingia naye kwenye ndoa awe anakupenda kwa dhati. Pendo ndiyo msingi wa kila kitu. Kama kweli anakupenda ni rahisi pia kutimiza kipengele kilichopita hapo juu.
NAWE UMPENDE
Kama niivyotangulia kusema, huwezi kuingia mkataba wa maisha na mtu ambaye humpendi kwa dhati. Lazima wewe pia umpende. Achana na utamaduni wa kuingia kwenye ndoa ukiwa mguu nje, mguu ndani kwa mategemeo kwamba eti utampenda ukiwa tayari mmeshaoana!
Hakuna kitu kama hicho rafiki yangu. Lazima nafsi yako ikuhakikishie kuwa ni kweli umempenda ndipo mambo mengine yafuate. Mapenzi hayalazimishwi. Acha kujaribujaribu! Kama unampenda, utajua tu, kama humpendi usipoteze muda wa mwenzako; Mwambie ukweli, jitoe.
AMEKUFANYIA NINI KISICHOSAHAULIKA?
Kati ya mambo ambayo yanaongeza mapenzi ya dhati kwa wawili ni pamoja na kufanyiwa kitu kisichosahaulika. Je, kuna kitu ambacho umefanyiwa na mwenzako huwezi kukisahau? Chunguza hili kwa makini. Marafiki zangu, hapa sizungumzii zawadi za sketi au suruali. Sipo kwenye upande wa manukato au mikufu? Yapo mambo makubwa, ambayo ukitafakari na kukumbuka namna mpenzi wako alivyokusaidia unaona kweli anastahili kuwa mwenzi wako wa maisha katika ndoa takatifu.
Hakuna majaribio kwenye ndoa ndugu zangu, ni maagano. Ni kifungo, wengine wanasema ni kitanzi! Umejiandaaje? Fanyia kazi kabla hujajutia ukiwa tayari ndani. Utatokaje?
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayendikia magazeti ya Global Publishers. Ameandika vitabu vya True Love na Let’s Talk About Love vilivyopo mitaani.
No comments:
Post a Comment