ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, January 5, 2012

KUMBUKUMBU YA TAREHE 5 JANUARI

CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO – CHADEMA MKOA WA ARUSHA
TAARIFA KWA UMMA
Ndugu wananchi na wakazi wa Arusha.
Tarehe 5 Januari ni siku ya kumbukumbu ya maana sana katika chama chetu kwenye mkoa wetu na halmashauri ya jiji letu la Arusha.

Tarehe 5 Januari mwaka 2011 ulifanyika mkutano mkubwa ambao ulikuwa umebeba ujumbe wenye madai ya wananchi kuhusu ukiukwaji wa demokrasia katika suala la uchaguzi wa UMEYA katika jiji la Arusha. Wakazi wa Arusha walijitokeza kwa wingi kwa sababu walikuwa wameelewa nini hasa kilikuwa kinalalamikiwa.


Kwa yote yaliyotokea mwaka mmoja umepita sasa, chama kinawapa pole makamanda wote na kuwataka tujipe moyo kwa safari ya ukombozi tuliyoianza. Sote tufahamu kuwa iko siku tena sio muda mrefu wakazi wa Arusha na Watanzania kwa ujumla tutafaidi matunda ya rasilimali zetu nyingi ambazo kwa ujumla wake iwapo zitasimamiwa vizuri kwa haki na usawa hatupaswi kuitwa maskini.

Tarehe 5 Januari, CHADEMA tulipaza sauti zetu tukiwa na madai ya msingi sana ambayo yanabeba maisha ya wakazi wa Arusha. Suala la uchaguzi wa MEYA wa jiji la Arusha ambao ulichakachuliwa kwa uwazi, makusudi na aibu kwa waliotenda. Bado madai ya wakazi wa Arusha na chama kwa ujumla yanabaki pale pale kuwa hatumtambui MEYA wa CCM aliyechaguliwa kwa mazingira yasiyo ya haki.
Kwa vile suala la maandamano lipo mahakamani, hatutalizungumzia, tunasubiri haki na sheria vichukue mkondo wake katika kuamua kuhusu suala hilo.

Sambamba na hili, tunawapongeza wakazi wa Arusha kwa ujasiri na umahiri wao katika kupigania na kusimamia bila woga masuala ya msingi. Ujasiri huu ndio unaopelekea wakazi wa Arusha kutokubali kunyanyaswa hasa inapokuja kwenye masuala muhimu ya haki za binadamu.

Kwa wakati wote hali ya Arusha katika uhalisi imeendelea kuwa ya amani na utulivu na watu wamekuwa wakifanya shughuli zao kama kawaida licha makada wa chama tawala CCM na baadhi ya viongozi wa serikali kutoa maneno yenye utata kwa kuizungumzia hali ya kisiasa kwa sura ya kukejeli demokrasia na haki za watu.    

Tunaendelea kuwasihi wakazi wa Arusha waendelee kuwa majasiri, waendelee kuwa wachapakazi na kuwa tufanye kazi kwa kujituma kwa maendeleo yetu na ya watoto wetu.

Mwaka wa 2012 uwe ni mwaka wa kitofauti katika kuifanya Arusha yetu kwa kuleta na kufikia mabadiliko chanya ya kiuchumi, kisiasa na kijamii na zaidi sana kushughulikia kwa dhati suala la ajira kwa wasio na ajira.

Amani Golugwa
KATIBU WA CHADEMA MKOA WA ARUSHA.

No comments: