ANGALIA LIVE NEWS
Monday, March 12, 2012
CCM kujibu mapigo ya Chadema Arumeru leo
Waandishi Wetu, Arumeru
RAIS Mstaafu, Benjamin Mkapa leo anatarajiwa kuongoza uzinduzi wa kampeni za CCM za uchaguzi mdogo wa ubunge Arumeru Mashariki zitakazofanyika katika Kata ya Usa River, wilayani Meru, Arusha.
Uzinduzi wa kampeni za CCM unakuja siku moja tangu wapinzani wao wakuu, Chadema wazindue kampeni katika Uwanja wa Leganga, Usa River wakiongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.
Vyama hivyo viwili vyenye upinzani mkubwa nchini, vinatarajiwa kubeba ajenda mbili kuu; migogoro ya ardhi na uhaba wa upatikanaji maji kwa matumizi ya nyumbani na kilimo.
Baadhi ya wakazi wa Arumeru wanasema mbunge wanayemtaka ni yule atakayeweza kuwaondoa katika migogoro ya ardhi ambayo inachochewa na maeneo makubwa kuchukuliwa na wawekezaji.
Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha, Mary Chatanda aliwaambia waandishi wa habari jana kwamba viongozi mbalimbali wa kitaifa watakuwa na vikao vya ndani katika kata zote 17 za jimbo hilo.
“Tayari tumekutana na makundi yote na sasa hali ni shwari. Makundi yote yameungana kumuunga mkono mgombea wetu Siyoi Sumari ambaye tuna uhakika atashinda,” alisema Chatanda.
Awali, kulikuwa na utata kama Rais mstaafu huyo, atafika kuzindua kampeni hasa kutokana na mpasuko mkubwa wa viongozi uliotokana na kura za maoni na makundi ya wanaojipanga kuwania urais mwaka 2015.
Alisema uzinduzi huo utahudhuriwa na viongozi kadhaa, akiwemo Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama na Mlezi wa chama hicho Mkoa wa Arusha, Stephen Wassira... “Kabla ya uzinduzi ambao utaanza majira ya saa 9:00 alasiri, kutakuwa na maandamano ya wafuasi wa CCM kutoka nyumbani kwa mgombea wetu eneo la Akheri hadi Usa River. Hatutaraji kuleta watu kutoka Arusha au Hai kama wenzetu (Chadema), sisi tutakuwa na watu wa Arumeru na watajaa uwanjani.”
Ardhi na maji
Masuala ya migogoro ya ardhi na maji yanapewa nafasi kubwa katika uchaguzi huo mdogo, huku suala la uwekezaji mkubwa unaochukua sehemu kubwa ya ardhi likigonganisha vichwa vya wagombea.
Mkazi wa Kijiji cha Nshupu, Anna Zacharia alisema migogoro mikubwa ya ardhi inatokana na kukua kwa miji midogo ya Usa River, Kikatiti, Maji ya Chai na Tengeru ambayo watu wake hawapati maeneo kwa ajili ya kuanzisha makazi yao kutokana na maeneo mengi kukaliwa na wawekezaji.
Mkazi wa Maji ya Chai, James Moirana alisema: “Mbunge tunayemtaka lazima ahakikishe kwamba suala la ardhi linapata suluhu, tumechoka kunyanyaswa katika nchi yetu.”
Migogoro ya ardhi na maji imesambaa katika maeneo mengi ya Wilaya ya Meru na wananchi wamekuwa wakilalamika kwamba Serikali imeshindwa kuitatua.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), Zitto Kabwe akizungumza kwenye uzinduzi wa kampeni za chama chake juzi alisema migogoro ya ardhi ni moja ya ajenda zitakazobebwa na chama hicho kwenye uchaguzi huo.
Mgombea wa chama hicho Joshua Nassari pia aliwaahidi wananchi wa Meru kwamba akichaguliwa, atachukua hatua kuhakikisha wanapata haki ya kumiliki ardhi kwa ajili ya kuendesha maisha yao.
Jana, Nassari aliwaomba kura wafanyabiashara wa Soko la Usa River akiwaahidi kuhakikisha soko hilo linakuwa na choo na mazingira bora ya kufanyia biashara.
Nassari alisema hakuna mbunge ambaye anawapa wananchi fedha na kuwaahidi kushirikiana nao kuhakikisha soko hilo linakuwa la bora na la kisasa... “Nasikitika sana mnalipa kila siku Sh500 lakini hapa hakuna choo, hakuna mazingira mazuri, ndugu zangu nawahakikishia kuwa mkinichagua tutakaa pamoja na kuhakikisha tunaboresha soko hili.”alisema Nassari.
Alisema Halmashauri ya Meru ni moja ya zile zinazokabiliwa na ubadhilifu mkubwa kwa kuwa hakuna diwani yeyote wa Chadema.
Siyoi akatiwa rufani
Katika hatua nyingine, Chadema kimekata rufaa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kikitaka kuenguliwa katika uchaguzi huo, mgombea wa CCM, Siyoi Sumari kwa maelezo kwamba si raia wa Tanzania.
Hatua ya Chadema imekuja saa chache baada ya Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Arumeru Mashariki, Trasias Kagenzi kutupa mapingamizi yote ya wagombea katika uchaguzi huo mdogo.
Kagenzi alisema Chadema na AFP, walimwekea mgombeahuyo wa CCM pingamizi kuwa si raia na kwamba waliomdhamini wana utata.
Kwa mujibu wa nyaraka za Chadema, ambazo zinanukuu, barua ya siri ya Ofisa Uhamiaji Mkoa wa Arusha, D. Namomba kwenda kwa Mkuu wa Mkoa, aliyetaka kujua uraia wa Siyoi, mgombea huyo wa CCM anadaiwa kuzaliwa Thika, Kenya na kuna utata kama aliwahi kuukana uraia wake wa awali.
Meneja wa Kampeni wa Chadema, Vicent Nyerere alisema wana ushahidi kuwa uraia wa Siyoi una tata hivyo, hawakubaliani na uamuzi wa Kagenzi... “Tunakata rufani NEC kwani tuna ushahidi kuwa raia wa mgombea wa CCM una utata.”
Pingamizi jingine ni lile la UPDP kilichokuwa kimepinga uteuzi wa mgombea wa Chadema, Joshua Nasari kwamba hakujaza maelezo ya kazi anayofanya kwa sasa.
“Baada ya kupitia mapigamizi haya pamoja na wanasheria wangu tumejiridhisha kuwa yote hayana nguvu kisheria na hivyo tumeyatupa,” alisema Kagenzi.
Akizungumza na gazeti dada la The Citizen kwa simu kutoka Dar es Salaam jana, Kamishna Mkuu wa Idara ya Uhamiaji, Magnus Ulungi alisema haoni tatizo lolote kuhusu uraia wa Sioi.
Alisema ni kweli kwamba alizaliwa Kenya lakini hiyo haimuondolei haki ya kuwa Mtanzania, wala hana haja ya kuukana uraia wa Kenya ambao hakuwahi kuwa nao.
“Wasichofahamu hao waliotoa pingamizi kwa Sumari ni Sheria ya Uhamiaji. Iko wazi kwamba mtoto aliyezaliwa na wazazi wote Watanzania ana fursa ya kupata uraia wa kurithi kutoka kwa wazazi wake…. hatakiwi kukana uraia ambao hakuwa nao,” alisema Ulungi.
Chadema mamilioni
Chadema kimekusanya Sh8 milioni kutokana na harambee ya kukichangia iliyoanza juzi katika uzinduzi wa kampeni za jimbo hilo.
Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba alisema fedha hizo zimekusanywa kupitia michango ya papo kwa papo na simu. Alisema Sh2.2milioni zilikusanywa uwanjani na Sh5.7 milioni zilikusanywa kwa njia ya simu hadi kufikia juzi jioni.
Alisema chama hicho kimeandaa chakula cha jioni Ijumaa wiki hii kwa ajili ya kukusanya fedha za kugharamia kampeni hizo... “Nia ya kukusanya fedha hizi ni kutaka watu wajione ni sehemu ya Chadema katika shughuli mbalimbali za chama.”
Imeandikwa na Neville Meena, Mussa Juma na Filbert Rweyemamu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment