AFISA MTENDAJI WA KATA YA SANGE (KULIA) AKIMSHUKURU MKUU WA WILAYA YA ILEJE BAADA A ZOEZI LA KUTOA FEDHA KWA WAKULIMA WA KAHAWA WA WILAYA HIYO AKIASHIRIA UZINDUZI WA MALIPO HAYO.
MKUU wa wilaya ya Ileje mkoani Mbeya Ester Wakali amevunja ukimya na kusema kuwa Serikali ya wilaya hiyo pamoja na wakulima hawataacha kushirikiana na Kampuni ya Lima inayopigwa vita na baadhi ya watu katika masuala ya biashara ya Kahawa wilayani humo.
Hayo aliyasema katika uzinduzi wa Malipo ya awamu ya Pili ya wakulima wa zao hilo waliokuwa wameuza Kahawa katika kampuni ya Lima Ltd uliofanyika katika viwanja vya Ofisi ya Afisa mtendaji wa Kijiji cha Sange wilayani humo.
Wakali alisema kuwa sababu kubwa inayosababisha kutoweza kuacha ushirikiano wa Serikali na kampuni hiyo ni kutokana na ushirikiano mkubwa wa kimaendeleo unaotolewa na kampuni hiyo wilayani humo likiwemo suala zima la kuhifadhi mazingira, udongo na mimea kupitia mradi wa kilimo hai sambamba na kuinua ubora wa zao la kahawa.
‘’Ndugu zangu watumishi wa Lima msikatishwe tamaa na maneno ya kuwakataza kununua kahawa mbichi (Chery) hii ni changamoto ambayo tunawapa ili muweze kuwainua wakulima kwa kuwalipa bei nzuri kwa ajili ya kugawana faida na wakulima wala si kumnyonya mkulima’’ alisema Mkuu wa wilaya huyo.
Alisema kuwa katika msimu wa mwaka jana, baada ya Serikali ya wilaya hiyo kukataza uuzaji wa kahawa mbichi, wakulima walisafirisha kahawa yao na kuenda kuiuza wilayani Rungwe mkoani hapa ambapo waliongeza mapato ya wilaya ya Rungwe yenye uchumi imara kuliko wilaya ya Ileje.
Kwa Upande wake Kaimu Meneja mkuu wa kampuni hiyo ya Lima Ltd, Felix Mtawa alimshukuru Mkuu wa wilaya hiyo kwa risala yake nzuri ya uzindizi wa Malipo hayo na kusema kuwa kampuni hiyo licha ya kununua kahawa hiyo haitaacha kutoa elimu kwa wakulima ambapo malipo hayo hya pili wananchi hao watanufaika kwa kupewa Shilingi Milioni 93, 792,150/=.
‘’Lima licha ya kununua kahawa kwa bei elekezi ya Serikali, hatutaacha kutoa elimu kwa wakulima kwa ajili ya kuboresha zao hili la kahawa ikiwa ni pamoja na kuzalisha miche bora katika vitalu, miche inayouzwa kuanzia Shilingi 1000 na wakulima waliotuuzia kahawa kwa msimu uliopita watapata fedha zao jumla ya Milioni 93’’ alisema Mtawa.
Alisema wakulima waachane na kasumba ya kudhani kuwa kilimo siyo muhimu bali ni utamaduni wa mazoea, aliwaomba wazee wa kata ya Sange na mahala popote inapozalishwa kahawa kuwapatia mashamba watoto wao ili waweze kujikita katika kilimo hicho cha zao la Kahawa na kama hawatakuwa na Mbegu wawasiliane na uongozi wa kampuni hiyo.
Naye meneja wa kampuni hiyo kanda ya wilaya ya Rungwe Iddy Kimwaga alisema kampuni hiyo itatoa mabaki kwa wakulima wote waliouza kahawa kwa msimu wa mwaka 2011-20012 ambapo kila kilo moja iliyonunuliwa itaongezewa shilingi 400.
Alisema mkulima aliyekuwa ameuza kahawa yake kwa shilingi 5000 atapatiwa 1,400 kwa kila kilo moja, aliyeuza 5,500 atapatiwa 900, aliyeuza 5,700 atapatiwa 700 na aliyekuwa ameuza kwa shilingi 6000 atapatiwa Shilingi 400 na hiyo inatokana na bei ya soko kwa msimu huo.
Mkuu wa wilaya hiyo katika uzinduzi huo aliwakabidhi wakulima watatu pesa zao kama ishara ya uzinduzi wa malipo hayo huku wakulima wakisema kuwa hawapo tayari kutekeleza maazimio ya viongozi wachache wa Serikali ya mkoa ambao msimamo wao ni kutowaruhusu wakulima kuuza kahawa yao mbichi ili hali hawawasaidii huku Serikali kuu ikiwa imekaa kimya juu ya maamuzi hayo kandamizi kwao. |
No comments:
Post a Comment