ANGALIA LIVE NEWS

Monday, January 20, 2025

POLISI PWANI WAMEMNASA ANAYESAMBAZA PICHA CHAFU SHULE YA BAOBAB




Na Khadija Kalili Michuzi Tv
JESHI la Polisi Mkoa wa Pwani linamshikilia mtu mmoja (jina kapuni) kwa kosa la kusambaza picha mjongeo kwenye mitandao ya kijamii kwa lengo la kuichafua Shule ya Sekondari BAOBAB iliyopo Wilayani Bagamoyo Mkoani Pwani.

Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Januari, 20 kwenye mkutano uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Jeshi la Polisi Pwani Kamishna Msaidizi wa Polisi Salim Morcane amesema kuwa Januari 3 ,2025 walipokea malalamiko kutoka kwa uongozi wa shule ya Baobab kuhusu kusambazwa picha chafu katika mitandao ya kijamii picha za mjongeo za utupu na zenye maudhui machafu kimaadili na kinyume na sheria za nchi.

"Picha hizo chafu na zisizo na maadadili imebainika kuwa waliotengeneza waliunganisha na baadhi ya majengo ya Shule ya Baobab ili kuaminisha umma kuwa vitendo hivyo vinafanyika shuleni hapo" .

Morcane amesema kuwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani limefanya uchunguzi na limefanikiwa kumkamata mtu mmoja ambaye uchunguzi wa kitaalam unesaidia kumfikia na kumkuta na picha hizo na kifaa cha kieletroniki ambacho alikuwa akikitumia kusambaza picha hizo chafu.

ACP Morcane amesema kuwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani linaendelea kuwasaka watu wengine walihusika katika kutengeneza na kusambaza picha mjongeo.

RPC Morcane amesema kuwa Jeshi la Polisi Pwani wanatoa onyo kwa watu wenye tabia kama hizo za kutengeneza na kusambaza picha kama hizo kwa malengo ya kuchafua wengine au taasisi kwani mkono wa sheria lazima utawafikia na hata kama hautawafikia mapema wataendelea kupata shida ya kujificha na kuacha kufanya shughuli zao za kujiletea maendeleo

Wakati huohuo Mkurugenzi wa Shule ya Baobab Shani Khalfan Swai amesema kuwa taarifa hizo zimewaathiri kwa kiasi japo muitikio wa wazazi kupeleka wanafunzi Shuleni hapo ni mkubwa.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Baobab Swai amesema kuwa kusambaa kwa picha hizo chafu za mjongeo ziliwapa taharuki kubwa wao uongozi wa shule pamoja na wazazi kwani simu zilikua za moto jambo lililowafanya waamue kukaa kimya huku wakitafakari njia sahihi ya kujisafisha na kubainisha ukweli ndipo walipotoa taarifa kwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani ambao wanauwezo wa kufanya uchunguzi na jambo la kushukuru kwa upande wao waliposikia mtu mmoja mwenye nia ovu anashikiliwa na Jeshi hilo huku uchunguzi ikiendelea. Swai ameongea kwenye mkutano na Waandishi wa Habari waliofika Shuleni hapo.

"Sisi Baobab tunaimani kubwa na Jeshi la Polisi kwamba wataisafisha Taasisi yetu iliyochafuliwa.

"Wazazi wa wanafunzi walipatwa na taharuki wengi walipiga siku kuhitaji kupewa ufafanuzi na sisi tuliwafafanulia kwamba hakuna tabia chafu hapa shuleni kwetu na hata zile picha mjongeo wale siyo wanafunzi wetu japo kuna picha za mahafali mdukuzi alizidukua akaunganisha na kwa upande mwingine mazingira ya mabweni yako tofauti na ya kwetu sisi" amesema Swai.

No comments: