ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, March 11, 2012

Ripoti mauaji ya Songea hadharani

Serikali mkoani Ruvuma imepokea na kutoa hadharani taarifa ya kamati iliyoundwa na Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu, kuhusiana na vurugu zilizotokea Februari 22, mwaka ambapo watu wawili walipoteza maisha kwa kupigwa risasi na polisi na baadhi ya wananchi kujeruhiwa.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Mwambungu ameyataja mambo kadhaa ambayo kamati hiyo imeyabaini kuwa chanzo cha vurugu hizo.
Mambo hayo ni pamoja na imani za kishirikina zilizohusisha mauaji yaliyokuwa yakitokea katika maeneo mbalimbali ya mji huo, kwamba watu wanaouawa wanatolewa baadhi ya viungo vya mwili kitu ambacho kamati hiyo imebaini siyo kweli na hakuna uthibitisho wowote uliopatikana.
Pia uvumi wa mambo mbalimbali kuhusu kauli ambazo hazina ukweli kuibuka na kusambazwa na baadhi ya wananchi bila kutafuta ukweli wa jambo wanalolizungumza, hali ambayo ilisababisha uvumi huo kuaminiwa na kundi kubwa la wananchi ambao hawakutaka kujiridhisha na badala yake kuanzisha vurugu hizo zilizotokea.
Alisema kuwa sababu nyingine ni namna ya wananchi kufikisha malalamiko yao kwa viongozi kulikosababisha mauaji ya watu wawili kutokea kwani waliamua kuchukua sheria mkononi badala ya kufuata taratibu za kuwasilisha malalamiko yao kwa njia isiyo ya hatari kwao na kwa viongozi wao.
Pia alisema yapo mambo ya kitaalamu na kisheria yaliyobainishwa na kamati hiyo ya watu nane inayoongozwa na Katibu Tawala Msaidizi, Sevelin Tosi na yameanza kufanyiwa kazi na mamlaka husika kwa kufikishwa mahakamani wahusika waliokamatwa siku hiyo ya tukio.
Kuhusu hali ya usalama wa mji wa Songea, Mwambungu amesema mpaka sasa hali ni shwari na ulinzi unazidi kuimarishwa kwa ushirikiano mkubwa baina ya jeshi la polisi na wananchi. Pia ameonya wananchi kutochukua sheria mkononi bali wafuate taratibu za kisheria.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments: