ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, March 10, 2012

Wazee wa kimila wamkataa mwalimu

WAZEE wa kimila (machifu) wa Kata ya Iganzo jijini Mbeya wamemtaka Ofisa Elimu wa Shule za Msingi katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya kumwondoa mwalimu wa Shule ya Msingi Juhudi (jina linahifadhiwa) ambaye alifukuzwa na wananchi wenye hasira kali hivi karibuni shuleni hapo kwa tuhuma za uchawi. 

Wakizungumza na gazeti hili kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya shuleni hapo, machifu hao walisema kuwa baada ya kumbaini kuwa anajihusisha na mambo ya kishirikina shuleni hapo waliamua kumfukuza ili kunusuru maisha ya wanafunzi na walimu wao na kwamba alikuwa kikwazo cha maendeleo ya elimu shuleni kwa muda mrefu. 

Walisema kuwa mwalimu huyo alikuwa akijihusisha mambo hayo ya kishirikina ambapo mara kadhaa Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Charles Mvella alikuwa akikuta vitu vya ajabu ofisini kwake vikiwemo vinyesi, kondomu na vitabu vilivyokuwa vimepangwa kabatini kuzagaa ovyo huku mlango ukiwa umefungwa kama kawaida. 

Waliongeza kuwa baada ya wazazi hao kufika shuleni hapo kumsikiliza mkuu huyo wa shule, walidai kuwa walielezwa hali halisi iliyopo shuleni hapo ndipo wazee wa mila (machifu) waanza kutafiti na kumbaini mwalimu mhusika. 

Chifu Leonard Lunile alisema kuwa baada ya kumbaini mwalimu huyo ndiye anayefanya mambo hayo walimuonya, lakini hakutaka kusikia na kuacha tabia yake ya kishirikina ambapo wananchi waliamua kwenda nyumbani kwake kumvamia na kumshambulia kwa kumpiga mawe hadi alipookolewa na jeshi la polisi waliofika eneo hilo mapema na kunusuru uhai wake. 

“Hata hivyo sisi machifu tunasema hivi asionekane tena jijini hapa akionekana tutajua cha kumfanya walikuwepo wengi kama yeye na sasa hawapo hawezi kutushinda,” alisema Chifu huyo. 

Taarifa zaidi zinasema kuwa mwalimu huyo alikuwa akifanya hivyo kwa lengo la kutaka madaraka shuleni huku akisaidiwa na baadhi ya viongozi waliondolewa katika kamati ya shule hiyo baada ya uchaguzi mpya wa kamati ya shule ndio maana kila alipokuwa akionywa na wazee hao hakutaka kusikia.


Habari Leo

No comments: