ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, April 19, 2012

Mapya yaibuka mauaji ya kichanga

Sakata la mtoto wa miezi saba, Angela David, anayedaiwa kuuawa na mfanyakazi wa ndani limezidi kuchukua sura mpya, baada ya baadhi ya sehemu za mwili wake kupelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Akizungumza na NIPASHE jana jijini Dar es Salaam, baba mzazi wa mtoto huyo, David Salakana, alisema mwanae amechukuliwa utumbo, nyama, kipande cha ini pamoja na damu kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi zaidi ili ibainike chanzo cha kifo chake ni nini hasa.

Salakana alisema kuwa ripoti ya uchunguzi wa awali waliyopatiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) umebaini kuwa mtoto wake alibanwa puani na kukabwa kooni na kwamba chakula kilionekana katika koo lake.

Hata hivyo, Salakana, alisema kwa sasa wanashughulikia mazishi ya mtoto huyo na kwamba watakapomaliza zoezi hilo ndipo watajielekeza kwenye uchunguzi wa kifo cha binti yao.

Salakana alisema kuwa mfanyakazi huyo wa ndani hajapatikana na kwamba simu yake ilikuwa inaita mpaka juzi.



“Simu yake bado ilikuwa inaita mpaka juzi, sasa polisi wameniambia niachane naye wao watamshughulikia na mimi nimeamua kukaa kimya. Kwa leo (jana) sijamtafuta sasa sielewi kama simu yake bado inaita au la,” alisema Salakana.

Mwili wa marehemu huyo uliagwa jana majira ya saa 6:00 mchana Muhimbili huku ndugu na majirani wakiwa katika hali ya majonzi kutokana na kifo cha mtoto huyo.

Wakizungumzia kifo hicho, walisema kuwa kimewasikitisha na kitendo kilichofanywa na mfanyakazi huyo na kuamua kukimbia na mizigo yake huku akiacha mtoto huo akiwa amekwisha kufa.

“Hata kama ni bahati mbaya amefariki huyu mtoto ni kwa nini akimbie huyo house girl (mtumishi wa ndani) anakijua alichokifanya,” alisikika muombolezaji mmoja akisema.

Msiba huo ambao ulijaa simanzi hospitalini hapo wakati wa kuaga mwili, mama wa mtoto alijikuta katika wakati mgumu aliposogelea jeneza na kumuona mwanae na kuishiwa na nguvu na kujikuta akishikwa na watu baada ya kushindwa kujizuia.

Baada ya ndugu, jamaa na marafiki kuuga mwili huo, safari ya kwenda Rombo, mkoani Kilimanjaro, kwa mazishi ilianza majira ya mchana.



Aidha, Salakana, alisema kuwa mazishi ya mtoto huyo yanatarajia kufanyika leo majira ya mchana katika kijiji cha Kirongo Juu, Tarafa ya Useri, wilayani Rombo.

Naye Bibi wa mtoto huyo, Beatrice Ndemasi, alisema kwa sasa wanachokisubiri ni majibu kutoka kwa Mkemia Mkuu.

Alisema tayari uchunguzi wa awali umeonekana na kwamba wanataka kuona hatua zitakazofuata kwani tukio hilo limewapa masikitiko makubwa.

“Kama ilikuwa ni bahati mbaya kutokea kwa kifo hicho ni kwa nini mfanyakazi huyo akimbie na hata alipopigiwa simu kuulizwa kwa nini umeamua kumuua huyu mtoto akajibu kuwa kwa hiyo tunaamuaje. Majibu yake aliyotupa yana utata, hivyo sampuli itatuletea majibu kujua kifo chake kimesababishwa na nini,” alisema Ndemasi.

Alisema msichana wa kazi baada ya kuona anasumbuliwa kwenye simu, alimua kuacha kuipokea.

“Jambo jingine lililotusumbua ni kwa nini alibeba mizigo yake yote, hivi kifo kama hicho kinatokea unawezaje kufungasha mizigo yote?” alihoji bibi wa mtoto huyo.

KAULI YA KENYELA

Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alithibitisha mtoto huyo kuchukuliwa sampuli katika mwili wake na kupelekwa kwa Kemia Mkuu wa Serikali kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Kenyela alisema bado Jeshi la Polisi linaendelea kumtafuta mfanyakazi huyo na kuongeza kuwa uchunguzi unaendelea.

Alisema Jeshi la Polisi linalaani kitendo cha kinyama kilichofanywa na mfanyakazi huyo kwa kumtelekeza mtoto huyo na kukimbia bila kuwasubiri wazazi wake wafike.

Hata hivyo, Kenyela aliwataka wananchi kuwa makini na watumishi wa ndani ambao wanawaajiri kwa kubaini tabia na mienendo yao. Pia aliwashauri kuhakikisha wanafahamu walikotoka.

 Alisema matukio kama hayo yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara na kwamba walichokigundua ni kuwa wafanyakazi hao hawafahamiki walikotoka hali ambayo inasababisha kushindwa kuwapata pale wanapotenda makosa na kutoroka.

Kamanda Kenyela alisema mtu yoyote ambaye atamuona mfanyakazi huyo alisaidie Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa ili iwe rahisi kumkamata.

Tukio hilo lilitokea Aprili 16, mwaka huu baada ya mtoto huyo kukutwa kitandani majira ya mchana akiwa amefariki dunia huku mfanyakazi huyo akiwa omeondoka na mizigo yake.

Mtoto huyo aliachwa na mfanyakazi huyo aliyetajwa kwa jina moja la Marietha (19) baada ya wazazi kuondoka nyumbani asubuhi kuelekea katika shughuli zao.

CHANZO: NIPASHE

1 comment:

Anonymous said...

Kwa maoni yangu ni kuwa huyu kichanga alikwamwa"choke" na na hicho chakula kinachosemwa kukutwa katika koo lake. Watu wengi hasa kama hawa wafanyakazi wa ndani ya nyumba, huwa hawafahamu ni vipi wawasaidie watu wanaokwamwa na kitu katika njia inayopitatisha hewa katika mwili wa mwanadamu. Kwa hiyo inawezekana hicho kichanga kilikutwa na masahibu hayo hadi kufariki na mfanyakazi asijue la kufanya, akapata mfadhaiko na kuamua kukimbia.