Jaji Frederick Werema |
MWANASHERIA Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema amewataka wabunge kuacha uvivu wa kufikiri na kutoa lawama juu ya sheria zinazotungwa bungeni kwa maelezo kuwa matatizo mengine yanayozungumzwa bungeni hayatokani na ubaya wa sheria, bali uwezo mdogo wa kufikiri.
Alitoa maneno hayo wakati akihitimisha mjadala juu ya Muswada wa Marekebisho ya Sheria mbalimbali ya Mwaka 2011 hasa katika eneo lililohusu uendeshaji wa Mfuko wa Jimbo ambao wabunge walilalamika kuwa kuna matatizo makubwa katika utekelezaji wake.
Akijibu hoja hizo za wabunge, Jaji Werema alisema: “Nasema uwezo mdogo wa kufikiri kwa sababu hakuna ubunifu na kama hakuna ubunifu basi ndiyo uwezo umefikia hapo.”
Alisema haoni sababu kwa nini kuna ucheleweshaji wa malipo na wakati fedha zimeshatolewa na Bunge.
“Sioni sababu yoyote na kwamba fedha zimetumika hata Mbunge hajui kama fedha imekuja.
Nafikiri hayo ndiyo tunasema ni uvivu wa kufikiri...Ninasema hivyo bila kuogopa chochote kwa sababu najua kwamba ninachosema ni kweli,” alisema Jaji Werema.
Alifafanua baadhi ya hoja za wabunge, Jaji Werema alisema kwa Tanzania Bara mhusika wa mfuko huo wa jimbo ni Waziri anayehusika na Serikali za Mitaa na kwa Tanzania Zanzibar ni Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia mambo ya Muungano.
Alisema kama kuna matatizo ambayo wabunge wengi waliyasema kuna kudai kuna usumbufu na urasimu wampelekee aone kama ni matatizo ya kisheria au yanatokana na uvuvi wa watu wa kufikiri.
Wakati huo huo, Jaji Werema alisisitiza kuwa kutungwa kwa sheria inayotaka mafisadi kufilisiwa mali zinazotokana na wizi, kamwe sio kuvunja Katiba ya nchi kwani sheria hiyo inashughulika na mali zile tu ambazo mtuhumiwa ameipata bila uhalali.
Jaji Werema alisema Katiba ya nchi inasema ‘kila mtu anayo haki ya kumiliki mali na haki ya hifadhi ya mali yake kwa mujibu wa sheria’ baada ya kunukuu akasema kifungu hicho kiko wazi ni kwa mujibu wa sheria kama mtu ana mali halali kwa mujibu wa sheria hakuna mtu atakayemnyang’anya mali hiyo na mali hiyo ina hifadhi ya sheria.
Alisema Ibara 24(2) ya Katiba inasema, ni marufuku kwa mtu yeyote kunyang’anywa mali yake kwa madhumuni ya kuitafisha au madhumuni mengineyo bila idhini ya Sheria ambayo inaweka masharti ya kutoa fidia inayostahili.’
No comments:
Post a Comment