ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, April 19, 2012

Zitto azilipua bungeni Tanesco, ATCL



Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), imependekeza kwa serikali iwakamate na kuwafikisha mahakamani maofisa wa serikali walioingia mkataba wa ukodishaji wa ndege ya ATCL, Air Bus 420-214, mwaka 2007.

Hali kadhalika, kamati hiyo imelishutumu Shirika la Umeme nchini (Tenesco), kwa kufanya manunuzi ya Sh. bilioni 600 bila kufuata sheria za manunuzi.

Hayo yalisemwa bungeni jana na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Zitto Kabwe, wakati akiwasilisha taarifa yake, kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 30, 2010.

Zitto alisema fedha hizo ni nyingi hivyo ni muhimu msisitizo na hatua za kisheria zitaendelea kuchukuliwa kwa taasisi zote ambazo zinakiuka sheria za manunuzi ya umma  kuisababishia serikali hasara kubwa.



“Mifano ya wazi kuhusu upotevu wa fedha za umma kutokana ana kutozingatiwa kwa sheria za manunuzi ya umma inaweza kuelezwa kwa ufasaha katika mashirika mengi yaliyojihusisha na vitendo hivyo,” alisema.

Kuhusu mapungufu katika ukodishaji wa ndege uliofanywa na Shirika la Ndege (ATCL), Zitto alisema kamati imebaini upungufu mkubwa ambao utaitia serikali hasara kubwa.

Alisema upungufu huo ni ukodishaji wa ndege aina ya Air Bus uliofanywa ATCL ambapo kamati ilibaini kuwa Msajili wa Hazina kwa niaba ya serikali alitoa dhamana kwa ATCL mwaka 2007 ili liweze kukodi ndege aina ya Air Bus 420-214 kutoka kampuni ya Wallis Trading ya Lebanon kwa muda wa miaka sita.

Alisema kamati ilikagua na kujiridhisha namna mchakato huo ulivyofanywa na kubaini  mapungufu makubwa kuwa ukodishaji wa ndege hiyo ulifanywa Oktoba, 2007, wakati dhamana ya serikali kwa ATCL ilitolewa 2/04/2008.

 Alisema ni wazi ndege hiyo ilikodiwa kabla ya kutolewa dhamana ya serikali wakati ni kinyume kabisa na sheria inayosimamia utoaji wa dhamana za mikopo serikalini.

“Mkataba uliingiwa kinyume na ushauri wa wataalamu ambao katika taarifa yao walisema sio sahihi kukodi ndege ambayo baada ya miezi sita itatakiwa kwenda Ufaransa kwa matengenezo makubwa, kamati ilibaini kuwa walioingia mkataba huo walijua kabisa kwamba ndege hiyo italazimika kwenda matengenezo,” alisema.

Alisema dhamana ya serikali iliyotolewa ilikuwa na thamani ya Dola za Marekani 60,000,000 na hadi kufikia Juni ,2011 dhamana hiyo pamoja na riba ni Sh. bilioni 108.

Zitto alisema eneo linguine ambalo kamati yake imeridhia kuwa kuna usimamizi usioridhisha wa fedha za umma ni katika Bodi ya Pamba Tanzania TCB. Alisema mwaka wa fedha ulioishia Juni 30,2010, ilionekana kuwa TCB ilipata hati yenye shaka ya ukaguzi kutokana na usimamizi usioridhisha wa fedha za umma zilizotolewa na serikali ili kunusuru wakulima wa pamba kutokana na kuanguka kwa bei ya zao hilo.

Alisema kwa mujibu wa ripoti ya mkaguzi wa nje aliyoifanya kwa niaba ya CAG, alibaini kuwa Sh. 2,472, 348,080 zilikuwa zimelipwa kwa wakulima lakini hakukuwa na uthibitisho wowote kuwa fedha hizo zimewafikia wakulima.

CHANZO: NIPASHE

No comments: