BAADHI ya mahabusu wa gereza kuu la Segerea mkoani Dar es Salaam, wameithibitishia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi, kuwa katika kumaliza matamanio yao ya muda mrefu ya kimwili, wamejikuta wakiingiliana kingono kinyume cha maumbile.
Wafungwa hao wamedai pia kuwa sababu nyingine inayosababisha kuwepo kwa ashki hiyo ni msongamano mkubwa wanaokabiliana nao katika vyumba vya mahabusu na kutopewa haki ya kukutana kimwili na wake zao kwa muda mrefu.
Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Rosweeter Kasikila alisema hayo jana alipozungumza na gazeti hili, kuhusu ziara ya kamati hiyo katika gereza hilo lililopo jijini Dar es Salaam.
“Kitu kilichotugusa tulipofika pale ni msongamano mkubwa wa mahabusu katika chumba kimoja, kwani tuliona chumba kinachotakiwa kuwa na mahabusu 40 walikuwa mahabusu 183, inatisha na ni hatari kwa afya zao,” alisema Makamu Mwenyekiti huyo.
Alisema hata wajumbe wa kamati hiyo walipozungumza na mahabusu hao, walikiri kuwa hali
hiyo ni ngumu kwao kwa kuwa hulazimika kulala kwa kubanana na kwa kuwa wengi ni vijana na rijali, hujikuta wakilazimika kufanya ngono kinyume cha maumbile ili kupunguza matamanio ya muda mrefu yanayowasumbua.
“Pia walisema wapo mahabusu wa muda mrefu, lakini wamekuwa hawapewi fursa ya kukutanishwa na wake zao, hali ambayo huwapatia wakati mgumu na kuwafanya wafanye vitendo visivyofaa,” alisema.
Watoto washuhudia
Pamoja na hayo, Kasikila ambaye ni Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), pia alisema kamati hiyo iliguswa baada ya kubaini kuwa katika gereza hilo kwa upande wa wanawake na wanaume, pia wamo watoto wenye umri chini ya miaka 18 wakiwa wamechanganywa na watu wazima, jambo ambalo ni hatari kwa usalama na afya zao.
Hata hivyo, alisema kamati hiyo ilifurahishwa na utaratibu wa kuwapima mahabusu afya zao hasa Ukimwi kwa hiari, kupatiwa dawa za kupunguza makali ya Ukimwi (ARVs) kwa wale walioathirika na elimu ya kujikinga kwa wale wasioathirika.
“Ingawa kwa wale walioathirika wamesema kuwa chakula wanachopewa hakiendani na hali zao, jambo ambalo linawafanya wengine waogope kunywa dawa zao za ARVs kwa kuhofia afya zao kudhoofika zaidi kutokana na nguvu ya dawa hizo,” alisema Kasikila.
Alisema baada ya maelezo hayo na kujionea hali halisi, kamati hiyo inaviomba vyombo husika, ikiwamo mahakama kuangalia namna ya kupunguza msongamano wa mahabusu hao kwa kuwa wengi wao upelelezi wa kesi zao umechukua muda mrefu huku wakiwamo wengine ambao adhabu za kesi zao zingefaa kuwa vifungo vya nje na kuitumikia jamii.
Upimaji Ukimwi kwa lazima
Wakati hali ikiwa hivyo magerezani, Mbunge wa Busega, Dk Titus Kamani (CCM) amependekeza mfumo wa sasa wa upimaji kwa hiari Ukimwi, ubadilishwe na uwe wa lazima ili kupunguza kasi ya maambukizi ya ugonjwa huo.
Pamoja na Dk Kamani, Mbunge wa Masasi, Mariam Kasembe (CCM) alishauri kuwa ili kuhamasisha upimaji wa ugonjwa huo, wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi waoneshe njia kwa kuandaa mpango wa kupima wao kwanza wanapofanya ziara zao hasa vyuoni.
Walitoa hoja hizo mara baada ya vyuo vikuu viwili; Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Mzumbe kutoa taarifa zao za maambukizi ya Ukimwi chuoni.
“Uwekwe utaratibu iwe lazima mtu akiumwa akienda hospitali apimwe na Ukimwi, ugonjwa huu ni janga la taifa si lazima tusubiri mtu akubali kupima kwa hiari wakati akiendelea kuusambaza bila kujua,” alisema Dk Kamani.
Alisema tatizo kubwa la kukabiliana na ugonjwa huo ni kutokuwepo kwa takwimu za uhakika za idadi ya walioathirika na sababu kubwa ni mfumo uliopo wa kupima kwa hiari.
“Si sahihi kuendelea kubembeleza hiyo haki, mtu huyuhuyu tunampaje haki asipime, lakini
anaendelea kuusambaza?” alisema.
Kwa upande wake, Kasembe alisema tatizo la Ukimwi nchini litakuwa vigumu kuisha kutokana na Watanzania wengi kukwepa kupima.
“Ndio maana nashauri sisi Kamati ya Bunge ya Ukimwi tufanye kampeni kama ile ya
Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete tuanze kupima wenyewe ili tuhamasishe wengine,” alisema.
Hata hivyo, Sera ya Ukimwi pamoja na Sheria ya Ukimwi vimeweka wazi kuwa upimaji
Ukimwi utakuwa kwa hiari na kuweka adhabu kwa watakaothibitika kuambukiza wenzao kwa
makusudi.
Awali, akiwasilisha mada ya Chuo Kikuu cha Dar es Saalam kuhusu Ukimwi, Mhadhiri wa chuo hicho, Dk Kitila Mkumbo, alisema pamoja na programu mbalimbali za elimu na ushauri kwa wanafunzi, watumishi na majirani wa chuo hicho, matokeo kwa waliojitokeza kupima yanaonesha kasi ya maambukizi chuoni hapo ni chini ya asilimia tatu.
Naye Mbunge wa Mtambile Masoud, Abdallah Salim (CUF) alivitaka vyuo vikuu nchini kuzingatia suala la maadili hasa mavazi kwa wanafunzi wa vyuoni huku akitolea mfano wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) ambacho hivi karibuni kilipiga marufuku uvaaji usio wa maadili kwa wanafunzi wa chuo hicho.
Kwa upande wake Makamu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Faustin Kamuzora, alisema hali ya maambukizi katika chuo hicho ni asilimia 6.5 ambapo waliojitokeza kupima walikuwa wanafunzi, watumishi na majirani wa chuo hicho.
Waziri wa Afya katika Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (DARUSO), Nzowa Cosmas, alisema tatizo la Ukimwi na ukosefu wa maadili katika chuo hicho linatokana na Tume ya Vyuo Vikuu kuongeza udahili wa wanafunzi huku vyuo vikiwa havina uwezo wa kuchukua wanafunzi wengi.
Aliishutumu Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HELSB) kwa kuchelewa kuwapatia majibu wanafunzi waliochaguliwa vyuoni, lakini wakiwa wamekosa fursa ya kukopeshwa kwa kuwa wengi wao hasa wa mikoani huenda vyuoni bila fedha na kuishia kujiuza au kuhifadhiwa na ‘mashugamami’ ili kujikimu.
Habari Leo
No comments:
Post a Comment