ANGALIA LIVE NEWS
Saturday, June 23, 2012
Hofu yatanda mgomo wa madaktari nchini
MAHAKAMA YAZUIA,MADAKTARI WABANDIKA MATANGAZO MUHIMBILI KUHAMASISHANA
Na Waandishi Wetu
MTAFARUKU kati ya Serikali na Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) kilichotangaza kuanza mgomo wa nchi nzima leo, umechukua sura mpya baada Mahakama Kuu ya Tanzania Kitengo cha Kazi, jana kutoa amri ya kusitishwa jambo hilo huku wanataaluma hao wa tiba wakisisitiza kushikilia msimamo wao. Mahakama hiyo ilitoa amri kuwataka madaktari hao kuendelea na kazi hadi madai yao msingi katika mgogoro huo, yatakaposikilizwa.
Wakati uamuzi huo ukitolewa, Katibu wa Jumuiya ya Madaktari, Edwin Chitega amepinga jambo hilo na kueleza kuwa mgomo wa madaktari uko palepale na utazuiwa tu kwa Serikali kutekeleza madai yao.
"Mgomo wetu hauwezi kuzuiwa na Mahakama, utazuiwa kwa madai yetu kutekelezwa," alisema Chitega.
Awali, Jaji Sekela Moshi alisoma hukumu hiyo iliyotolewa jana jioni wakati gazeti hili likienda mtamboni kwa kusema kuwa zuio hilo ni la muda na linalenga kupata fursa ya kusikiliza kwanza maombi ya msingi kuhusu mgogoro huo.
"Kwa maelezo hayo, ninasitisha mgomo huo ulioitishwa na Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), hivyo MAT na wanachama wake hawapaswi kushiriki mgomo huo leo kama walivyopanga hadi pande zote mbili zitakaposikilizwa," alisema Jaji Sekela.
Katika hukumu hiyo iliyosomwa bila wawakilishi wa MAT, Jaji Sekela alipanga Jumanne ijayo kuwa siku ya kusikiliza maombi hayo ya msingi na kueleza kuwa hukumu itakayotolewa, itafungua ukurasa mpya kuhusu mgogoro huo.
Mapema kabla ya amri hiyo ya Mahakama kutolewa jana, madaktari walisisitiza kutekeleza azma yao ya kugoma kwa kubandika matangazo ya kuhamasishana kwenye kuta za Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na Taasisi ya Mifupa Muhimbili (Moi).
"Tangazo kwa madaktari na wafanyakazi wote wa sekta ya afya. Kama mnavyokumbuka, baada ya siku 90 za mazungumzo na Serikali tarehe 9.6.2012 tulipata mrejesho wa mazungumzo hayo.
"Madaktari kwa ujumla wetu tuliikataa taarifa hiyo na kutangaza mgogoro na Serikali kwa wiki mbili na baada ya hapo, ifikapo tarehe 23.6 kama Serikali itakuwa haijatekeleza madai yetu tutaanza mgomo usiokuwa na kikomo nchi nzima, mpaka hapo ufumbuzi utakapopatikana.
"Kwa taarifa hii tunapenda kuwakumbusha kuwa mgomo wetu utaanza rasmi tarehe 23 mwezi huu nchi nzima," linasomeka moja ya bango la matangazo hayo.
Matangazo hayo yalizua tafrani kwa baadhi ya wagonjwa ambao kwa nyakati tofauti waliishauri Serikali kumaliza tatizo hilo kwa kutekeleza madai ya madaktari.
“Ningeshauri Serikali iwasikilize madaktari ili kumaliza tatizo hili kama watagoma watu wengi wataathirika hususan wasio na uwezo wa kumudu gharama za matibabu kwenye hospitali binafsi,” alisema Zuberi Balama.
Ofisa Uhusiano wa Moi, Jumaa Almasi alisema uongozi wa taasisi hiyo hauwezi kuzungumzia tangazo la mgomo huo kwa kuwa halikutolewa na utawala.
"Taarifa hii ni ya Jumuiya ya Madaktari na si ya uongozi wa taasisi. Wao ndio wanaostahili kuulizwa kama wanaendelea na mgomo ama la, sisi katika hili hatuna cha kusema," alisema Jumaa alipotakiwa kuzungumzia tangazo hilo.
Uongozi wa Hospitali ya Muhimbili haukupatikana jana kuzungumzia suala hilo kutokana na vikao vilivyodumu kwa muda mrefu, hata alipotafutwa msemaji wake, Eminael Aligaesha kwa simu hakupatikana.
Serikali yawatahadharisha
Wakati matangazo hayo yakibandikwa Muhimbili, Dar es Salaam, Serikali imewatahadharisha madaktari hao kuacha mgomo, ikieleza kuwa ni batili na ni kinyume cha viapo vyao vya kazi.
Wito huo ulitolewa jana bungeni na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi ambaye alisema kuwa Serikali imeamua kutoa amri hiyo kutokana na ukweli kuwa madhara yatokanayo na mgomo wa madaktari ni makubwa na yanagharimu maisha ya watu.
“Kabla ya kuendelea na mpango huo, madaktari hawana budi kufikiria kwa kina ili kuepuka madhara ambayo yatagharimu maisha ya Watanzania wasio na hatia,’’ alisema Dk Mwinyi na kuongeza:
“Mimi ni mgeni katika Wizara ile, Naibu Waziri ni mgeni hali kadhalika Kaimu Katibu Mkuu na Kaimu Mganga Mkuu, lakini madaktari wenzangu wameshindwa kabisa kunipa ushirikiano pale ninapoomba wafanye hivyo wamekuwa wakikaidi, nawasihi sana wakubali tuzungumze,’’ alisisitiza Mwinyi.
Mwinyi alibainisha kuwa katika kifungu cha 76 (1) cha Sheria ya Mahusiano Kazini namba 6 ya mwaka 2004, inabainisha makundi ya wafanyakazi ambao hawaruhusiwi kugoma kuwa ni pamoja na kada hiyo ya udaktari ambao wanahudumia afya na maabara.
Waziri aliainisha mambo 10 ambayo madaktari walikuwa wamepanga kutekelezewa na kusema kuwa kwa sehemu, yametekelezwa na baadhi ya mambo yaliyobakia wanaweza kuyazungumza.
Aliwasihi madaktari kuachana na mgomo huo na kusema kuwa jambo hilo liko chini ya Mahakama kupitia Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (The Commision for Mediation and Arbitration) na kwamba Serikali pamoja na madaktari wanatakiwa kufuata taratibu za kurudisha suala hilo kwenye tume hiyo kwa hatua zaidi.
Katika hatua nyingine, hali katika hospitali za Mwananyamala, Temeke na Amana jijini Dar es Salaam jana iliendelea kuwa shwari kwa madaktari kuendelea na shughuli.
Hata hivyo, baadhi ya madaktari walisema wana taarifa za mgomo huo na kueleza kuwa watashiriki kikamilifu ukianza rasmi leo.
Dodoma
Huduma za matibabu zilionyesha kuanza kusuasua katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma jana na kuwafanya wananchi waliofika hosptalini hapo kuanza kulalamika.
Gazeti hili jana lilishuhudia kundi kubwa la wagonjwa waliofika hospitalini hapo kupata huduma wakiwa wanasubiri bila mafanikio kwa muda mrefu huku baadhi yao wakieleza wasiwasi wao kuhusu mgomo huo.
Walisema chumba kimoja kilichopo eneo la mapokezi, ndicho kilichokuwa kikifanya kazi jambo walilosema limesababisha msongamano wa
wagonjwa.
Mkazi wa eneo la Kikuyu, Hamisi Ramadhani, alisema yeye alifika hospitalini hapo tangu saa 1.00 asubuhi lakini hadi saa nne alikuwa hajapata matibabu, hatua iliyomfanya akate tamaa.
“Mimi sijui kama kuna mgomo, lakini nimekuja tangu saa moja asubuhi nasumbuliwa na kichwa na hivi sasa ni saa nne mchana sijapata matibabu ya aina yoyote hapa,” alisema Ramadhani.
Kilimanjaro
Mkoani Kilimanjaro madaktari katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC, walishikilia msimamo wao wa kuanza mgomo leo huku wenzao katika Hospitali ya Mkoa wa Kilimanjaro ya Mawenzi, wakiwa wamegawanyika katika makundi mawili.
Habari za uhakika kutoka Hospitali ya Mawenzi zinasema, baadhi ya madaktari walikuwa tayari kushiriki mgomo huo ingawa wengine walisita kwa hofu ya kupoteza ajira zao.
“Sisi tuko tayari kuanza mgomo kesho (leo), lakini kuna wenzetu waoga wanasita kutuunga mkono na hili linaweza kutuathiri kwa sababu tukiingia wachache, italeta shida,” alidai daktari mmoja wa hospitali
hiyo.
Hata hivyo, wakizungumza na gazeti hili baadhi ya madaktari wa KCMC walisema wao wameshakubaliana kuanza mgomo na hakuna kitakachowazuia kwa kuwa walivuta subira lakini majibu yanayotolewa na Serikali yanakatisha tamaa.
Dk Petro Arasumin wa Kitengo cha Dawa cha hospitali hiyo
alisema, Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) kimekaa meza ya majadiliano na
Serikali mara sita lakini hakuna suluhu iliyopatikana na Serikali imekuwa ikitoa majibu yasiyoeleweka.
“Walitaka wakae na madaktari ikaundwa kamati imekaa na Serikali mara
sita lakini hakuna kilichotokea wao wanasema madaktari wanataka fedha
nyingi tumewauliza ni kiasi gani lakini haitaki kusema, sasa sisi
tumeamua kufanya mgomo mpaka pale Serikali itakapoona malalamiko yetu
ni ya maana,” alisema.
Mbeya
Katika Hospitali ya Mkoa wa Mbeya, madaktari wamesema wataungana na wenzao katika mgomo huo.
Wakizungumza jana kwa sharti la kutotajwa majina yao gazetini, walisema wapo tayari kuungana na madaktari kote nchini kugoma ili kuishinikiza Serikali kuwatimizia madai yao.
“Sisi leo (jana), tunaendelea na kazi kama unavyoona tunachosubiri ni kesho tutakapoungana na wenzetu kote nchini kufanya mgomo usiokuwa na kikomo hadi hapo Serikali itakapokubaliana na madai yetu,” alisema mmoja wa madaktari hao.
Daktari mwingine ambaye hakutaka kutajwa gazetini, alisema, “Tumechoka. Serikali ikubali kututekelezea madai yetu na kuboresha huduma za afya katika hospitali zote nchini ili kuondokana na adha iliyopo."
Habari hii imeandaliwa na Rehema Matowo, Moshi, Masoud Masasi na Habel Chidawali, Dodoma, Godfrey Kahango, Mbeya, Geofrey Nyang’oro na Elizabeth Edward, Dar
Mwananchi
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment