Mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Dk. Stephen Ulimboka, alisema jana kwa njia ya simu kuwa, huduma za dharura zitasitishwa katika hospitali hizo kutokana na serikali kutoonyesha nia ya kutatua madai yao kama ilivyotoa ahadi na badala yake kinachofanyika ni propaganda tu.
Dk. Ulimboka alisema wanashangaa kusikia kuwa serikali imeweka zuio mahakamani kushinikiza madaktari wasigome, hatua ambayo alidai ni propaganda tu zinazofanywa na serikali kwani madaktari hawajapewa rasmi taarifa hizo.
“Kauli za serikali na zuio la mahakama tunazichukulia kama ni propaganda tu, kwanza sababu hilo zuio hatujalipata rasmi zaidi ya kusikia kwenye vyombo vya habari, kwa hali hiyo kesho (leo) wagonjwa watakuwa na wakati mgumu sana, maana tumekusudia kusitisha huduma zote za dharura katika hospitali zote nchini, ” alisema.
Alisema ufumbuzi wa mgogoro wa madaktari na serikali unashindwa kupatikana haraka kwa sababu viongozi wakuu wa serikali wanaelezwa mambo ya uongo na watu wa chini jambo linalopelekea kutokuwa na habari sahihi za utekelezaji wa madai yao.
Alisema kutokana na serikali kupuuza madai yao italazimika kuwajibika kikatiba katika suala la kuwahudumia wagonjwa ambao wataendelea kupata tabu kwa kukosa huduma za matibabu.
Hata hivyo, wakati madaktari hao wakitangaza msimamo huo, NIPASHE lilielezwa kuwa viongozi wa jumuiya hiyo walikuwa wamejificha katika sehemu isiyojulikana ambako walikuwa wakifanya mkutano wao wa siri.
HUDUMA MUHIMBILI ZASUASUA
Katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, jana utoaji wa huduma kwa wagonjwa zilikuwa zikisuasua ambapo wagonjwa walieleza hali hiyo ilianza kujitokeza tangu juzi.
Katika wodi ya watoto, wauguzi waliokuwa wanaonekana wakifanya kazi ni wale walioitwa kwa dharura na wengi wa madaktari hawakuonekana katika sehemu zao za kazi.
Mmoja wa daktari katika wodi hiyo, ambaye aliomba jina lake lisiandikwe gazetini alisema, wameamua kusitisha huduma mpaka serikali itakaposikiliza hoja zao za msingi.
Alisema watoto wengi wanakufa kwa ukosefu wa hewa ya oksijeni wanapofanyiwa upasuaji kutokana na kukosekana kwa vifaa vya kuvutia hewa.
Alisema kamati iliyoundwa na Rais Jakaya Kikwete kutatua matatizo yanayowakabili madaktari imekuwa ikidharau vikao hivyo, na kila siku wanapokutana kunakuwa na watu wengine tofauti na wale waliokutana nao awali.
“Kila kikao tunachokaa na wawakilishi kutoka serikalini wanakuwa wapya, kikao hiki wanakuja hawa, kikao kinachofuata wanakuja wengine wapya, jambo linalopelekea kutopiga hatua katika mwafaka,” alisema daktari huyo.
Daktari huyo alisema wanamshangaa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi kwa kauli yake ya kusema anataka kuzungumza na madaktari upya wakati anafahamu kuwa mazungumzo na serikali yameshafanyika mara kadhaa bila ya kuafikiana madai yao.
HOSPITALI YA TEMEKE
Msimamizi Mkuu wa hospitali hiyo, Dk. Rolesta Kinunda, alisema hakuna mgomo kwa madaktari wanaendelea na kazi kama kawaida na wanaendelea kupokea wagonjwa kutoka maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam.
Huduma katika hospitali hiyo zilionekana kuendelea kama kawaida, ambapo madaktari walionekana wakipita wodini na kutoa huduma kama kawaida.
Rashid Ndwangila, mkazi wa Mbagala, ambaye amelazwa kwenye wodi namba saba ya wanaume hospitalini hapo baada ya kufanyiwa operesheni ya henia alisema kwa jana madaktari walipita kama kawaida na kuwahudumia wagonjwa wote kwa kuwapatia dawa pamoja na kuwafunga vidonda.
AMANA NA MWANANYAMALA
Huduma katika hospitali hizo zilionekana kuendelea kama kawaida ambapo wagonjwa walikuwa wakihudumiwa na madaktari.
MBEYA: JAMAA WAONDOA WAGONJWA
Baadhi ya jamaa wa wagonjwa wameanza kuwaondoa katika Hospitali ya Rufaa Mbeya kwa ajili ya kwenda kutafuta matibabu kwenye hospitali za watu binafsi.
NIPASHE jana liliwashuhudia baadhi ya wagonjwa wakipandishwa kwenye magari na kuondoka kwenda kusikojulikana.
Averine Ngeya, mzazi wa mtoto Miliam Alex ambaye ameungua vibaya kwa maji ya moto, alisema tangu juzi baada ya madaktari kuanza mgomo, wagonjwa hawapati huduma nzuri za matibabu zaidi ya kupewa na wauguzi vidonge vya kutuliza maumivu.
“Tangu jana (juzi) hakuna matibabu ya maana ambayo mwanangu ameyapata, wauguzi ndio wanatupatia panado za kutuliza maumivu na kutuambia kuwa tusubiri daktari anaweza kuja wakati wowote, lakini madaktari hawatokei,” alisema Ngeya.
Nipashe limetembelea katika Hospitali ya Rufaa ya Wazazi iliyopo eneo la Meta mjini hapa na kushuhudia eneo la hospitali likiwa halina watu kutokana na matangazo yaliyobandikwa kwenye mbao za matangazo na kuta za hospitali hiyo yakionyesha kuwa hakuna huduma.
Ofisi za hospitali hiyo na ile ya rufaa zilikuwa zimefungwa na wauguzi waliokuwa vibarazani walikataa kuzungumza lolote kuhusiana na hali hiyo kwa madai kuwa wao sio wasemaji.
Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa Mbeya, Dk. Eliuter Samky, alithibitisha kuwepo kwa mgomo wa madaktari walio kwenye mafunzo ya vitendo wanaofikia 70.
Hata hivyo, alisema anao uhakika kuwa madaktari 10 bingwa wataendelea kufanya kazi na hivyo huduma kwa wagonjwa hasa wale walio katika hali ngumu na wale wa dharura zitaendelea.
KCMC WAENDELEA KUGOMA
Mgomo huo umeiathiri Hspitali ya Rufaa ya KCMC mjini Moshi, ambapo inasemekana kila idara ina
daktari mmoja wa zamu huku wengi wakiwa kwenye mgomo.
Habari ambazo zimethibitishwa na baadhi ya madaktari waliopo kwenye mgomo zinasema sio rahisi kubaini athari kwa kuwa jana ilikuwa siku ya mapumziko.
“Kuanzia leo (kesho) ndio athari za mgomo wetu zitaonekana vizuri, kwani tutaachia maeneo yote na kubakiza eneo la wagonjwa mahututi na majeruhi wa ajali mbalimbali,” alisema daktari mmoja na kuongeza: “Lengo si kuwaumiza wananchi bali kuishinikiza serikali kutekeleza madai yetu.”
Mwanahamisi Ally aliyelazwa wodi ya majeruhi na Haji Rashidi anayemuhudumia baba yake katika wodi namba mbili, walisema huduma si za kuridhisha sana kwani kuna mabadiliko ya wazi tangu madaktari walivyotangaza mgomo na wanaoumia zaidi ni wagonjwa, madaktari hawaonekani wakitoa huduma na hata wakihitajiwa hawaonekani.
“Tunaiomba serikali kumaliza tatizo hili kwa haraka, sidhani kama mahakama inaweza kuwa ndiyo suluhisho la kushinikiza madaktari warudi kazini, wakirudi kwa mtindo huo hali haitakuwa nzuri,” alisema Rashid.
DODOMA 34 WAGOMA
Madaktari 34 walioko katika mafunzo kwa vitendo katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Dodoma, juzi hawakufika kazini licha ya kutakiwa kuwepo.
Hata hivyo, huduma katika hospitali hiyo na Kituo cha Afya cha Makole zilikuwa zikiendelea kama kawaida.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Ezeckiel Mpuya, alisema wameendelea na huduma za matibabu kama kawaida katika hospitali yao.
MGOMO BUGANDO WATHIBITISHWA
Uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Bugando ya jijini Mwanza umetihibitisha baadhi ya madaktari wake kuanza mgomo rasmi.
Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali hiyo, Dk. Japhet Gilyoma, ameliambia NIPASHE jana kuwa, licha ya mgomo huo kuanza, lakini hali ya huduma za matibabu bado si mbaya sana kwa sababu kuna madaktari bingwa ambao waliendelea kuhudumia wagonjwa juzi na jana.
“Ni kweli kwamba madaktari wetu pia wameingia katika mgomo, lakini kama unavyojua leo(jana ) ni weekend (mwisho wa juma) madaktari wanaokuwa zamu ni wachache, ninachoweza kusema kwa sasa ni kwamba hali ya matibabu si mbaya kwa sababu specialists (madaktari bingwa) wanaendelea na matibabu, ” alisema.
TANGA SHWARI
Katika Hospitali ya Mkoa wa Tanga ya Bombo, jana madaktari waliokekana wakiwa wanatoa huduma za katibabu kwa wagonjwa kama kawaida.
PADRI: MGOMO NI HALALI
Padre Baptiste Mapunda wa Kanisa katoliki, amesema mgomo wa madaktari ni halali. Alitoa kauli hiyo jana wakati akiendesha ibada katika Kanisa la Mtakatifu Karoli Lwanga la Yombo Dovyo, Dar es Salaam.
Padri Mapunda ambaye ni Mkurugenzi wa Shirika la Farijika Afrika Mashariki, alisema kuwa serikali ilitakiwa kuwapatia haki zao kwani wananyanyaswa na kwamba madai yao ni ya msingi.
Padre Mapunda alisema madaktari hao wanatakiwa wapatiwe haki zao ili waweze kufanyakazi katika mazingira bora na na kuwa serikali isizungumze masuala ya amani wakati haki za wananchi hazipatikani, hivyo ni halali yao kufanya mgomo ili wapatiwe wanachokitaka.
Imeandikwa na Thobias Mwanakatwe, Samson Fridolin, Gwamaka Alipipi, Beatrice Shayo, Dar; na Dege Masoli, Tanga; Emmanuel Lengwa, Mbeya; Salome Kitomari, Moshi; Sharon Sauwa, Dodoma na George Ramadhan, Mwanza.
CHANZO: NIPASHE
1 comment:
wacheni wagome kawaleteni madoctor kutoka INDIA NA CHINA.
HAWA PIA HAWAKO KWA AJILI YA UMMA WA KITANZANIA WAKO KWA AJILI YAO NA MAFISADI WAKUBWA
Post a Comment