ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, June 27, 2012

Milovan alia kumkosa Ngasa

Kocha wa Simba, Mserbia Milovan Cirkovic amefichua kuwa alivutiwa sana na kiwango cha juu kilichoonyeshwa na winga Mrisho Ngasa wa klabu ya Azam katika msimu uliopita wa Ligi Kuu ya Bara na kwamba anasikitika kumkosa kwenye kikosi chake cha msimu ujao utakaoanza Septemba Mosi.

Akizungumza jana baada ya mazoezi ya timu yake kwenye viwanja vya Sigara, Chang’ombe jijini Dar es Salaam, kocha huyo alisema kuwa awali aliuomba uongozi wa klabu yake kufanya kila wanaloweza ili wamalizane na Azam na kumsajili Ngasa; jambo ambalo anasikitika kuona kuwa halikufanyika.



“Ni mchezaji mzuri (Ngasa), nilimtaka sana katika kikosi changu,” alisema Milovan.

Hata hivyo, kocha huyo alisema kuwa amevutiwa vilevile na usajili wa wachezaji wengine wote kwani wanaonyesha uwezo mkubwa mazozini na anaamini kwamba Simba itafanya vizuri katika michuano mbalimbali inayowakabili, ikiwemo ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame).

“Msimu ujao tutaonyesha kiwango kizuri zaidi ya msimu uliopita kwa sababu tumeimarisha kikosi chetu,” alisema.

Jana, wachezaji wa mabingwa hao wa soka Tanzania Bara walionekana kujituma katika muda wote wa mazoezi yao na mashabiki waliofika kwenye viwanja vya Sigara waliwashangilia sana wachezaji wapya, hasa mshambuliaji Patrick Kanu ambaye baada ya kumalizika kwa mazoezi hayo alibebwa juu juu huku wengine wakimuelezea kuwa ndiye “muuaji wao mpya”.

KIPA MPYA, KASEJA

Kipa Waziri Hamad aliyesajiliwa na Simba akitokea JKT Oljoro ya Arusha anaendelea kuonyesha kiwango cha juu na kuelezewa kuwa anatishia nafasi ya Juma Kaseja ya kuwa ‘chaguo la kwanza la kudumua’ kwa nafasi ya kulinda lango.

Licha ya kufanya vizuri mazoezini, Hamad pia aling’ara katika mechi yao ya kujipima nguvu dhidi ya Toto African iliyofanyika hivi karibuni kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza ambapo Simba ilishinda 2-0.

Hamad ambaye pia aliwahi kuichezea Majimaji ya Songea, alidaka vizuri na kutoruhu bao katika dakika 45 za mechi waliyotoka sare ya 1-1 dhidi ya Express ya Uganda.

Msimu uliopita, Kaseja alirudia kuandika rekodi yake ya kucheza mechi zote peke yake kama alivyofanya msimu wa 2008/ 2009.
Hata hivyo, Akimzungumzia Hamad, Kaseja ambaye msimu uliopita alirudia rekodi yake ya kucheza mechi zote za Simba kama alivyofanya msimu wa 2008/ 2009, alisema kuwa anaonyesha uwezo wa hali ya juu na kwamba amefurahishwa na usajili wake.

Kaseja aliongeza kuwa Simba imefanya usajili makini na anaamini kuwa kutakuwa na ushindani mkali msimu ujao utakaoinufaisha timu yao.

Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange 'Kaburu' alisema kuwa wanajivunia kufanya usajili wa kimya kimya, lakini wenye manufaa kwa kuwajumuisha wachezaji wenye vipaji vya hali ya juu.

"Hatuna papara katika usajili wetu, ila tunawaahidi mashabiki wa Simba kuwa watafurahi, njooni kwenye mazoezi mshuhudie vijana wanavyofanya kazi," alisema Kaburu.

Baadhi ya wachezaji wapya waliosajiliwa na Simba ambao wameshaanza mazoezi ni pamoja na Kigi Makasi, Salim Kinje, Lino Musomba na Kanu.

Mbali na kujiandaa na msimu ujao wa ligi, Simba, Azam na Yanga zinajiandaa kuiwakilisha Tanzania Bara katika mashindano ya Kombe la Kagame yatakayoanza Julai 14 jijini Dar es Salaam.

 
CHANZO: NIPASHE

No comments: