ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, June 30, 2012

Msafara wa Rais wakumbwa na tafrani




Msafara wa Rais Jakaya Kikwete jana ulikumbwa na tafrani maeneo ya Tegeta, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam baada ya wananchi wenye hasira kurusha mawe hovyo wakati wakipambana na mabaunsa waliokodiwa na tajiri mmoja aliyenunua kiwanja eneo hilo kuamuru wananchi hao wavunjiwe nyumba zao.
Tukio hilo la aina yake lililosababisha askari polisi kutumia mabomu ya machozi na risasi za moto kuwatawanya wananchi wenye hasira, lilitokea majira ya asubuhi  wakati msafara wa Rais ukielekea Bagamoyo kwenye shughuli za kikazi.
Kundi la mabaunsa na askari wa kampuni binafsi ya ulinzi ya Nas walifika eneo la Namanga na kuvunja nyumba 10 za wananchi.

Mjumbe wa shina wa eneo hilo, Lameck Fidel, aliiambia NIPASHE Jumamosi kuwa kumekuwepo na mgogoro wa muda mrefu kati ya wananchi waliovunjiwa nyumba pamoja na mmiliki wa kituo cha mafuta cha Gapco ambacho kwa sasa kinamilikiwa na Big Bon.

Fidel alisema kuwa uvunjaji huo haukuwa halali kwani bado kesi yao ipo mahakamani na pia kuna hati ya zuio kwa mmiliki wa kituo hicho kufanya lolote katika eneo hilo.

"Kwa kweli nashindwa kuelewa ina maana wengine wapo juu ya sheria hivi kama suala hili lipo mahakamani na hakuna hati yoyote ya uvunjaji inakuwaje huyu Mwarabu anajichukulia sheria mkononi kwa kuvunja nyumba za watu,?"alihoji Fidel.

Aliitaka serikali kuchukulia suala hilo kwa mapana kuepusha maafa makubwa zaidi.

Naye mmoja wa wananchi waliovunjiwa nyumba zao, Waziri Rashid alisema kuwa wanaishi eneo hilo miaka mingi na wapo hapo kihalali kwa kuwa wana hati za asili.

Rashid alisema kuwa mmiliki wa kituo hicho amekuwa akiwanyanyasa sana hasa baada ya juhudi zake za kuwahamisha kushindikana.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, aliyefika eneo la tukio muda mfupi baada ya vurugu hizo, alilaani vikali kitendo kilichovyofanywa na wananchi  waliorusha mawe wakati  msafara wa Rais ukipitia eneo hilo kwa kuitia ni kitendo cha kihuni.

"Hivi msafara wa Rais ulikuwa na makosa gani kwani ndiye aliyewatuma kuja kuvunja nyumba, nawaomba acheni kujichukulia sheria mkononi na tutafanya uchunguzi kuhusiana na kitendo hiki cha kihuni ili watakaobainika sheria ichukue mkondo wake mara moja," alisema Kenyela.

Kuhusiana na tukio la uvunjaji nyumba, alisema kuwa jeshi la polisi linafanya uchunguzi kuhusu uhalali wa uvunjaji huo ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.
Kenyela alisema kuwa katika tukio hilo watu wawili ambao ni askari wa kampuni ya ulinzi ya Nas wameumizwa vibaya na kukimbizwa Mwananyamala kwa matibabu.
Alisema kuwa mmiliki wa kituo cha mafuta aliyemtaja kwa jina la Hemed Salum (39) mkazi wa mikocheni amekamatwa pamoja na mabaunsa 44 waliotumwa kuvunja nyumba na askari 54 wa kampuni binafsi ya ulinzi ya Nas.
Kenyela pamoja na kuwapa pole  wananchi waliokutwa na tukio hilo la kuvunjiwa nyumba zao lakini pia amewataka kuacha jazba ambazo zinaweza kusababisha wakajikuta pabaya kwa  kushindwa kufuata taratibu za kisheria.
CHANZO: NIPASHE

No comments: