Florence Majani
UTAFITI uliofanywa na Taasisi ya kifedha ya Finscope, umebaini kuwa, asilimia 21 tu ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam na vitongoji vyake ndiyo wenye elimu ya usimamizi wa fedha huku asilimia 48 tu, wakiwa na ufahamu wa jinsi ya kujiwekea akiba.
Matokeo ya utafiti huo yanamaanisha kuwa, karibu asilimia 80 ya wakazi wa Dar es Salaam, hawana elimu hiyo muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi.
Aidha utafiti huo ulionyesha kuwa, wanawake ni asilimia 54 ya wakazi wa jiji ambao huchukua mikopo na ni kundi ambalo ni waathirika wa ukosefu wa elimu hiyo ya kifedha.
Utafiti huo uliofanywa mwaka 2009 ulibaini kuwa idadi kubwa ya Watanzania wanashindwa kufikia malengo ya kimaendeleo kwa kukosa elimu hii ya usimamizi wa kifedha na wengine kudidimia zaidi katika umasikini kwa sababu hiyo.
Akizungumza wakati wa semina kwa waandishi wa habari jana jijini, mtoa mada Ally Goronya alisema kutokana na hali hiyo, taasisi ya Nuebrand inatarajia kutoa elimu ya huduma ya kifedha na uwekezaji bure kwa muda wa siku nne kuanzia Oktoba 10 hadi 13, katika Viwanja vya Mnazi Mmoja.
Kuhusu madhara ya ukosefu wa elimu hiyo kwa Watanzania, Goronya alisema wateja wengi wanaochukua mikopo wamekuwa wakidhulumiwa haki zao kwa sababu hawana elimu ya kutosha ya kifedha.
“Watanzania wengi wanakwenda kuchukua mikopo, lakini wanashindwa kujua haki zao jambo linalosababisha mikopo hiyo kutowasaidia na badala yake kuwadidimiza katika lindi la umasIkini,” alisema Goronya
Alisema wengi huchukua mikopo bila kupata elimu na kujua haki zao ili kuwalinda na kunufaika na mikopo hiyo akitolea mfano, riba kubwa, muda wa marejesho na haki ya kuvunja mkataba wa marejesho kama masuala yanayowatesa wakopaji.
“Wakati mwingine watoaji wa mikopo huacha kwa makusudi kuwaelewesha vizuri au kuwapa elimu watumiaji wa huduma hiyo, ili wawadhulumu haki zao, hasa katika marejesho na riba,” alifafanua Goronya.
Aliongeza zaidi na kusema kuwa ni vyema Watanzania wakapata elimu hiyo ili wajue uchaguzi sahihi wa taasisi za fedha za kupata huduma, kwa kuangalia kiasi cha riba kinachotozwa, muda wa marejesho, muda wa kupewa mkopo na usiri wa taarifa za mtumiaji.
Ofisa Mawasiliano wa Kampuni hiyo, Deogratius Kishombo alisema katika kampeni hiyo ambayo imepewa jina la ‘Wiki ya Huduma za Kifedha na Uwekezaji’, Watanzania watapewa elimu ya kukabiliana na madeni, kuhifadhi fedha, bajeti na nidhamu ya mikopo.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment