ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, July 18, 2012

CHANGAMOTO KWA VIJANA KABLA YA NDOA -4


HELLO marafiki! Bila shaka mpo sawa na mnaendelea vyema na majukumu yenu ya kila siku. Kwa upande wangu nipo mzima kabisa. Mchakamchaka unaendelea.

Katika kuhitimisha mada hii, nitasimulia visa viwili (lakini ni halisi) nilivyokutana navyo wiki hii katika kazi yangu ya kushauri. Ni vya msichana na mvulana (majina na namba zao nahifadhi)

Kwa kawaida huwa situmii njia ya sms kushauri ila inapolazimika kuwa hivyo. Wawili hawa walikuwa kati yao. Hebu angalia namna nilivyowasiliana nao, utajifunza kitu.

MSICHANA: Kaka Shaluwa ninaye mpenzi wangu, nampenda sana lakini sisi tupo wawili (akimaanisha wanachangia mwanaume mmoja) tatizo akiwa na mimi anamponda mwenzangu na akienda kwa mwenzangu ananiponda. Kwa ushauri wako nifanyeje?

ALL ABOUT LOVE: Sasa mwanaume mwenye mwanamke mwingine wa kazi gani?

MSICHANA: Hata mimi nashangaa, maana huyo msichana ndiye amenikuta mimi.

ALL ABOUT LOVE: Hapo ni suala la kukutwa au uamuzi wa huyo boyfriend wako kuwachanganya? Kwani alilazimishwa au yeye ndiye aliyemfuata?

MSICHANA: Kwa kweli sijui, lakini kikubwa naomba unishauri cha kufanya.

ALL ABOUT LOVE: Huyo mwanaume si mwaminifu. Tafuta mwanaume wa peke yako.

MSICHANA: Lakini nampenda, siwezi kumuacha, nitafanyaje?

ALL ABOUT LOVE: Kimya...


MSOMAJI MWINGINE

MVULANA: Bro vipi? Kuna demu ananizingua sana, mimi nampenda na nimejaribu kumweleza ukweli, amekataa. Anasema ana jamaa yake na hajui namna ya kumuacha. Hebu nishauri, nimwambie aachane naye kwa mtindo gani?

ALL ABOUT LOVE: Kama amekuambia ana wake, ya nini kumuhangaikia?

MVULANA: Yeye amesema ananipenda, lakini tatizo hajui namna ya kumuacha, ndiyo nataka unisaidie.

ALL ABOUT LOVE: Huoni kama hata nikikusaidia, baadaye anaweza kutongozwa na mwanaume mwingine, akaomba kusaidiwa namna ya kukuacha? Tafuta wako, achana naye. Au unaona sawa kushea mapenzi?

MVULANA: Ila kama hanitaki, mbona amesema anatamani kuja chumbani kwangu, tukae wawili tu halafu tuangalie mkanda wa kikubwa? Anataka nini sasa hapo bro?

ALL ABOUT LOVE: Una umri gani?

MVULANA: Kwa nini umri?

ALL ABOUT LOVE: Nataka kujua jibu la kukupa lililo sawa na umri wako.

MVULANA: Miaka 22.

ALL ABOUT LOVE: Sawa sawa, ndiyo maana majibu yangu hayajakutosheleza. Tatizo mimi nazungumzia mapenzi, wewe unawaza ngono...ni vyema sasa ukabadili mtazamo wako mdogo wangu. Fikiria kuhusu maisha yako zaidi ya starehe za muda mfupi. Maisha yako yapo mikononi mwako.

MVULANA: Ahsante bro, nimekuelewa.


HEBU TUJIFUNZE

Bila shaka kuna kitu umejifunza kupitia vijana hawa wawili. Wa kike anaonekana hajui thamani yake. Yupo tayari kuwa na yeyote, hata kama atakuwa na mtu mwingine. Huyu mawazo yake ni kwamba, mapenzi kwa mwanamke ni kunyanyaswa.

Ni kuonewa, mwanaume ana uwezo wa kuwa na idadi ya wanawake aitakayo. Si kweli. Hayo ni mawazo ya kizamani sana. Kadhalika mvulana anaonekana kuwa na mawazo ya ngono zaidi kuliko mapenzi.

Hafikirii kuhusu mapenzi ya kweli wala mipango ya baadaye ya maisha yake. Anataka kupata mwanamke wa kupotezeana naye muda tu. Ni lazima kijana ujitambue. Ni kweli kuna changamoto nyingi sana kwenye ujana lakini lazima ukabiliane nazo.

Ukishindwa kujipanga ungali kijana, ukiwa mtu mzima hutaweza. Kama una mtazama kama vijana hawa, kwa kweli inakupasa ubadilike haraka sana. Wakati haukusubiri ndugu yangu.

Hebu sasa twende tukaone vipengele vilivyosalia ambavyo inakupasa uwe navyo makini sana wakati ukitafuta mwenzi wa maisha.


IMANI ZA DINI

Inapendeza zaidi kama mkioana ndani ya imani moja ya dini. Upo utararibu wa wachumba kufunga ndoa bomani, ambapo kila mmoja huwa na dini yake. Siku za hivi karibuni wengi wanafanya hivi, lakini si sahihi kwa asilimia mia moja.

Ndoa imara ukiacha juhudi za wahusika wenyewe hujengwa na kulindwa na imani thabiti ya dini ya wahusika. Mnapokuwa katika imani moja ni rahisi kumfikia Mungu pamoja katika maombi au kwenda kwa viongozi wa dini na kupewa ushauri wa kiroho.

Jambo hili lisiwe la mwisho, kama tayari dalili za kuoana zinaonekana wazi, muanze kujadiliana mapema juu ya suala la dini.


MWISHO KABISA

Ni vizuri kuzijua changamoto mapema na namna ya kukabiliana nazo. Acha kuamini kwamba kwenye ndoa kuna furaha tu - starehe tu. Kuna mengi ya kukabiliana nayo ambayo unapaswa kuwa makini tangu mapema.


Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia magazeti ya Global Publishers, ameandika vitabu vya True Love, Let’s Talk About Love na Who is Your Valentine? vilivyopo mitaani.

No comments: