ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, July 18, 2012

Hotuba ya upinzani yazua mtafaruku


  Yazuiwa kusomwa bungeni ikielezwa kuingilia mahakama
Spika wa Bunge, Anne Makinda
Hotuba ya Kambi ya Upinzani Bungeni kuhusu makadirio ya matumizi na mapato ya Wizara ya Mambo ya Ndani kwa mwaka wa fedha 2012/13, imezua mtafaruku mkubwa ndani ya Bunge baada ya Spika wa Bunge, Anne Makinda, kuamuru sehemu ya hotuba hiyo isisomwe kwasababu kuna kesi mahakamani.

Mvutano huo ulifuatia baada ya msemaji wa kambi ya upinzani kwa upande wa wizara hiyo, Vincent Nyerere,  kuanza kusoma sehemu ya mauaji yenye sura ya kisiasa.

Kufuatia hali hiyo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alilazimika kuomba mwongozo wa Spika kuhusu sehemu hiyo na nyingine zilizokuwa bado kusomwa lakini kesi zake zipo mahakamani.



Lukuvi aliomba mwongozo kwa kutumia kifungu cha 64 (1) kwa kusema katika hotuba hiyo ukurasa wa tatu hadi wa nne, mambo yanayozungumzwa yako mahakamani na mengine yapo kwenye uchunguzi wa polisi.

Alisema maelezo yaliyotolewa na kambi ya upinzani katika hotuba hiyo yangeweza kutumika kama ushahidi wa kutosha kwa polisi badala ya kuyawasilisha bungeni.

Aliomba Spika kutumia busara yake na kuyatoa mambo hayo kwasababu yataharibu uchunguzi unaofanywa na Jeshi la Polisi na pia ni kuingilia uhuru wa Mahakama.

Baada ya kumaliza kuongelea jambo hilo, Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, alisimama na kumtaka Spika na Bunge lake kuwatendea haki wabunge wachache wa kambi ya upinzani kwa kuacha hotuba yote isomwe badala ya kuiondoa.

Alisema juzi wabunge wengi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), walikuwa wakizungumzia jambo hili na wengine kutoa hukumu kuhusiana na vurugu zilizotokea katika mkutano wa hadhara uliohutubiwa na Chadema katika kata ya Ndago Wilaya ya Iramba.

Lissu alisema hajawahi kuona hata siku moja tangu kuingia bungeni msemaji wa kambi ya upinzani ama serikali akikatishwa kusoma hotuba yake.

“Serikali ituache tuendelee kuwasilisha hotuba yetu, kwani kufanya vingenevyo ni kutotutendea haki mheshimiwa Spika,” alisema Lissu ambaye pia ni Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni.

Hata hivyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema, ambaye alikiri kweli kanuni ya tano inamtaka Spika kutenda haki lakini kwa kufuata kanuni.

 “Si kweli kwamba jana (juzi) waliongea kwamba Chadema walihusika…nilisema kuwa wabunge watakaoombwa kutoa ushirikiano waende na maelezo haya yako ukurasa wa nne ndiyo yanatakiwa kutolewa huko,” alisema.

Akijibu mwongozo huo, Spika Anne Makanda alisema sehemu ya hotuba hiyo iliyobeba kichwa cha habari cha ‘mauaji yenye sura ya kisiasa’ isisomwe hadi hapo Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, itakapokaa mchana na kutoa ushauri wake.

Spika Makinda alisema yeyote ambaye atakwenda kinyume cha kanuni ataingiliwa ili asiendelee hata kama ni waziri ama si waziri.

Alimtaka Lissu kwenda kusoma kumbukumbu rasmi za Bunge kuangalia kama wabunge wa chama tawala wamekuwa hawaingiliwi wanapozungumza kinyume cha taratibu.

“Kwa yale yaliyoko mahakamani hapana, yalioko kwenye upelelezi mnaweza kusema kwa kuwa mtawasaidia polisi, yaliyoko mahakamani niambieni hayapiti hapa ipo katika kanuni ya 64,” alisema Makinda.

Akijibu hilo, Lukuvi alisema, “wanaozungumza wote wanazungumza kwa nia ya kujenga na kwamba yeye hana nia mbaya na mnadhimu wa kambi ya upinzani (Lissu).”

Kauli hiyo ilileta minong'ono na mishangao ya baadhi ya wabunge hadi pale Spika Makinda alipoingilia kati na kutuliza jambo hilo na hivyo Lukuvi kuendelea na maelezo.

Alitaja kesi zilizopo mahakamani ambazo zimetajwa katika hotuba ya msemaji wa kambi ya upinzani kuwa ni ile ya
Mbunge wa Iringa, Mchungaji Peter Msigwa dhidi ya kada wa CCM, mauaji yaliyotokea wiki iliyopita Wilayani Iramba mkoani Singida, wabunge wawili waliopigwa na kuumizwa mkoani Mwanza na utekaji nyara wa Dk. Stephen Ulimboka.

Hata hivyo, Mbunge wa Nyamagana (Chadema), Ezeckia Wenje, alisema anachoelewa kikanuni inakataza kuzungumzia kesi zilizoko mahakamani lakini katika hotuba hiyo hawakuzungumzia kuhusiana na mwenendo wa kesi hizo.

“Mbunge wa Serengeti (CCM) Stephen Kebwe jana (juzi ) alisema live kwamba wanachama wa Chadema wameshiriki katika mauaji…hotuba yetu haizungumzii mwenendo wa kesi zilizoko mahakamani isipokuwa inazungumzia maelezo ya jumla ya kesi hizo,” alisema.
Alisema kilichotajwa ni matukio na wala si mwenendo wa kesi zilizoko mahakamani.

Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Chiku Abwao, aliomba mwongozo wa Spika, alitaka kujua ni kanuni ipi ambayo imetumika katika mwongozo uliombwa na Waziri Lukuvi, kwa kuwa ndio kwanza msemaji wa kambi yao alikuwa ameanza kusoma hotuba yake.

Alisema Nyerere alikuwa hata hajasoma vipengele ambavyo vimeomba kutosomwa na Waziri Lukuvi.

Akijibu mwongozo huo, Spika Makinda, alisema mwongozo huo hauna msingi kwa kuwa hoja zinazowasilishwa mezani zinaruhusiwa kusomwa na wabunge kabla ya msemaji kusoma na kisha kusema wanachoona kuwa hakifai kusoma.

Naye Mbunge wa Bariadi Mashariki (UDP), John Cheyo, aliomba utaratibu kutumia kanuni ya 76 (1) inayosema “kwa madhumuni ya kuthibiti fujo endapo itatokea ndani ya ukumbi wa Bunge Spika ataona kuwa kuna haja ya kutumia nguvu basi anaweza kuahirisha shughuli za Bunge bila ya hoja yoyote kutolewa au kusitisha kikao kwa muda atakautaja ili fujo hiyo iweze kudhibitiwa na mpambe wa Bunge.”

Alisema kwamba ubishi uliokuwa wakati huo bungeni unaweza kusitishwa kwa kupeleka hotuba hiyo katika kamati hiyo ili kuangaliwa kama mambo hayo yako mahakamani.

Alisema ni vizuri hoja hiyo ikasitishwa hadi hapo mambo hayo yatakapoangaliwa yamo katika mahakamani.

“Niwaombe wote sisi ambao tumetoka wote wananchi wanategemea sana kambi ya upinzani, iwe na utulivu iweze kutoa kitu ambacho wananchi wanategemea ili watu wote wasikilize kwa utulivu bila kuvunja madeksi ,”alisema.

Spika Makinda alisema hoja hiyo inaweza kutumika lakini kwa hatua iliyofikia katika jambo hilo haiwezi kutumika na kumtaka Nyerere kuendelea kusoma kwa kuruka sehemu hiyo ya sura yenye sura ya kisiasa.

Alisema kutokana na jambo hilo, kusoma kwa sehemu hiyo kutaleta sura kuwa Bunge linaingilia mhimili mwingine wa mahakama.

Hata hivyo, baadaye jioni, akitangaza ushauri wa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, Spika Makinda alisema  masuala matano kati ya sita yaliyokuwemo katika sura hiyo, yamebainika kuwa yako mahakamani.

Alisema jambo ambalo halipo mahakamani imethibitika kuwa ni la kuuwawa kwa kada wa Chadema Mbwana Masudi lilotokea wakati wa uchaguzi mdogo wa jimbo la Igunga mkoani Tabora.

Spika Makinda alitolea mfano kesi ya Singida watu sita wako mahakamani wakati suala Arusha na Dar es Salaam, mtu mmoja mmoja amefikishwa mahakamani.

 
CHANZO: NIPASHE

No comments: