ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, July 26, 2012

Kinu cha nyukilia mbioni kujengwa




Serikali inaandaa mpango wa kujenga kinu cha utafiti wa nyuklia nchini katika mpango wake wa muda wa kati ili kuboresha utoaji wa huduma mbalimbali zinazohusu nguvu za atomiki.

Hayo yalisemwa bungeni jana na Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa, wakati akiwasilisha bajeti yake kwa mwaka wa fedha 2012/2013.

Alisema teknolojia ya nyuklia inamchango mkubwa katika maendeleo ya Tanzania hivyo inahitaji kutumiwa na kuendelezwa kwa nia ya kuleta maendeleo endelevu.

Alisema baadhi ya sekta ambazo teknolojia hiyo inaweza kuleta mchango muhimu kuwa ni pamoja na afya, kilimo, mifugo, mali, elimu, utafiti na viwanda.



Wakati huo huo, Profesa Mbarawa amesema Tanzania imeanza kutekeleza mfumo mpya wa anuani za makazi na Simbo za Posta katika maeneo mbalimbali.

Alisema utekelezaji huo ulianza katika kata nane za Manispaa ya Arusha ambapo uzinduzi rasmi ulifanyika Januari, 2010.

Aidha, alisema utekelezaji pia ulifanywa katika kata nane za Manispaa ya Dodoma.

Profesa Mbarawa alisema uzinduzi wa utekelezaji wa mfumo wa anuani za makazi kwa jiji la Dar es Salaam ulifanywa Novemba mwaka jana na juhudi zinafanywa kupata fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mfumo huo kwa jiji hilo.
CHANZO: NIPASHE

No comments: