ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, July 26, 2012

Pinda ajitosa kumwokoa Katibu Mkuu Nishati




Kikao cha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda,  na wajumbe wanaotoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) walioko katika Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, kimeshindwa kuzaa matunda baada ya wabunge kushikilia uamuzi wao wa kutaka wale wote waliohusika na ukiukwaji wa kanuni za manunuzi ya mafuta ya kuzalisha umeme wa dharura kuwajibika.

Pinda aliitisha kikao hicho jana katika ofisi yake iliyoko ndani ya viwanja vya Bunge, lengo likiwa ni kuokoa bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini ambayo itawasilishwa bungeni kesho.

Wabunge watano wa CCM walishikilia msimamo wa kukataa wazo hilo na kuongeza uwezekano wa bajeti ya wizara hiyo kukwama kama ilivyokuwa mwaka jana.


Makadirio ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2011/12 yalikwama baada ya wabunge kuitaka serikali kutafuta fedha za kutosha kwa lengo la kuinusuru nchi iondokane na mgawo wa umeme.

Pinda aliitisha kikao hicho ili wabunge wa Kamati ya Nishati na Madini waache kuishinikiza serikali kumwajibisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, ambaye anatuhumiwa kukiuka Sheria ya Manunuzi ya Umma katika kutoa zabuni ya ununuzi wa mafuta mazito ya kuzalishia umeme wa dharura katika kwa kampuni ya Puma ambayo ilipewa vibali vya kuiuzia serikali mafuta lita milioni tisa kwa mwaka 2011 na lita milioni tisa kwa mwaka huu.

Kibali cha kwanza kilitolewa Septemba 28, mwaka jana, huku kingine kikitolewa kwa utaratibu huo huo wa kutofuata Sheria ya Manunuzi ya Umma Julai 12, mwaka huu kwa ajili ya kuuza lita milioni tisa.

Habari kutoa ndani ya kikao hicho zinasema kuwa, Waziri Mkuu, aliwaambia wabunge hao kuendelea kushikilia uamuzi huo wa kutaka waliohusika na sakata hilo  kujiuzulu kutaiathiri serikali kwa kuwa ni muda mfupi kumefanyika mabadiliko katika Baraza la Mawaziri.

Chanzo chetu kilisema Pinda aliwaambia wabunge hao kuwa, kitendo cha kushinikiza mawaziri kujiuzulu kinaweza kuitia aibu serikali kwa mara nyingine.

Kikao hicho pia kiliwashirikisha Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na manaibu wake, George Simbachawene na Steven Masele.

Kwa mujibu wa taarifa toka ndani ya kikao hicho, wabunge waliopinga kuachana na mpango wa kuhoji ukiukwaji wa Sheria ya Manunuzi ya Umma ni Mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher ole Sendeka; Mbunge wa Korogwe Mjini (CCM), Yusuph Nassir; Mbunge wa Igalula (CCM), Athuman Mfutakamba; Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Sara Msafiri; Suleiman Zedi (Mwenyekiti) na Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Munde Abdallah.

Habari zinaeleza kuwa wabunge hao walihoji kwa nini aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, David Jairo, aliwajibishwa kutokana matumizi mabaya ya fedha za umma, lakini waliohusika katika tuhuma za kutoa kibali cha kuagiza mafuta kwa kampuni ya Puma kinyume cha sheria ya manunuzi ya umma waachwe bila kuchukuliwa hatua.
Walihoji, inakuwaje Jairo anawajibishwa kwa kuchangisha Sh. bilioni moja, wakati Maswi wahusika watoe zabuni yenye thamani ya Sh. bilioni 13 bila kuchukuliwa hatua.

Aidha, wabunge hao waliitaka serikali kuacha kuudanganya umma kuwa hakutakuwa na mgao wa umeme kwa kuwa fedha haijaonyesha ni wapi zitapatikana kwa ajili ya kununulia mafuta ambazo ni Sh. bilioni 40 kila mwezi wakati kwa miezi mitano iliyobaki kumaliza mwaka huu zitatakiwa Sh. bilioni 200.

Wabunge wa kamati hiyo kutoka CCM walitarajiwa kuungwa mkono na wajumbe wenzao kutoka upinzani.

Habari zaidi zinasema kuwa, kutokana na kutofikiwa kwa mwafaka katika kikao hicho, Sendeka, anakusudia kupeleka bungeni hoja binafsi akitaka kuundwa kwa kamati teule kuchunguza sakata hilo ama Bunge kuazimia Waziri  Muhongo pamoja na Katibu Mkuu Maswi, kujiuzulu nafasi zao.

Kutokana na kikao hicho kushindwa kufikia makubaliano, wabunge wa CCM walitarajiwa kukutana jana saa 3:00 usiku.

Hata hivyo, tofauti na vikao vingine vya wabunge wa chama hicho ambapo hutangaziwa bungeni, jana wabunge hao katika muda tofauti walipokea ujumbe mfupi wa maneno (SMS) wakitakiwa kukutana muda huo.




 
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: