MNADHIMU wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu ameingia matatani
kutokana na kauli yake kwamba Rais Jakaya Kikwete amekuwa akiteua majaji
wa Mahakama Kuu wasiopendekezwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama.
Kutokana
na kauli hiyo aliyoitoa wakati akiwasilisha maoni ya kambi yake, kuhusu
hotuba ya makadirio ya matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria, Lissu
ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) atajadiliwa na
Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge.
Wakati akisoma
hotuba yake, mbunge hiyo alisema majaji wanaoteuliwa na Rais hawafanyiwi
‘vetting’ (uchunguzi) na tume hiyo kuona kama uwezo na ujuzi wao unafaa
kukabidhiwa madaraka ya ujaji.
Mwenyekiti wa Bunge, Jenista Mhagama ndiye aliyeamuru suala la Lissu
kupelekwa katika kamati hiyo baada ya mbunge huyo kukataa kufuta kauli
yake ambayo kwa mtazamo wa Serikali iliwadhalilisha majaji.
Hata
hivyo, jana alipotakiwa kueleza kama ana taarifa rasmi za kuitwa kwenye
kamati hiyo Lissu alisema: “Sijaitwa, lakini nina taarifa kuwa naweza
kuitwa.’’
Alisema, hata wakimwita hatakuwa na jambo lolote la
kuzungumza kwa kuwa Mwenyekiti wa Bunge aliyeongoza kikao hicho juzi
(Jenista Mhagama), alikosea kwa kuwa ndiye aliyepaswa kumpa adhabu.
Mbunge
huyo alisema juzi aligoma kufuta kauli yake kama alivyotakiwa na
Mwenyekiti kwani aliamini kuwa hata Mwanasheria Mkuu alikuwa amekosea.
Alibainisha
kuwa endapo ataitwa katika kamati hiyo, atahoji kama waliomwita
wamegeuka kuwa wenyeviti wa Bunge na kama si hivyo, anaamini watakosa
neno la kumhoji.
Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe na
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema kwa nyakati tofauti
wakati wakijibu hoja za wabunge juzi jioni walisema: “Lissu aliwakashifu
majaji bungeni, hivyo alipaswa kuomba radhi.”
No comments:
Post a Comment