Na Edson Kamukara
KAMBI ya Rasmi ya Upinzani bungeni imeeleza kushangazwa kwake na hatua ya Serikali kushindwa kuwa na takwimu za kiasi gani cha fedha zimepatikana kama stahiki yake ya kodi kutoka kwenye sekta ya michezo hususani uuzaji na ununuzi wa wachezaji kwa timu za ndani na nje.
Pia, kambi hiyo iliitaka serikali kueleza wazi ni uwekezaji gani unaofanyika kwa lengo la kupata faida na baada ya muda gani kutokana na uwekezaji wa sh bilioni 56.4 uliofanywa na serikali kwenye uwanja wa michezo wa Taifa.
Kauli hiyo ilitolewa jana na msemaji wa kambi hiyo kwa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Joseph Mbilinyi (Chadema), wakati akiwasilisha maoni ya upinzani
Alisema, ni mara nyingi wamekuwa wakiishauri serikali kuanzisha uwekezaji mkubwa katika sekta ya michezo kwa ujumla, lakini mapendekezo na ushauri wao vimeshindwa kuchukuliwa kwa umakini.
Kuhusu malipo ya makocha wazalendo, Mbilinyi maarufu kama Sugu, alisema yapo malalamiko ya muda mrefu ya makocha hao wanaofundisha timu za ndani kulipwa ujira kiduchu mno ikilinganishwa na wageni.
“Kambi ya upinzani inataka serikali kutoa majibu kuhusu
hatua iliyofikiwa kuhusiana na maandalizi ya mikataba kwa makocha wazalendo. Hii ni kwasababu katika randama iliyotolewa na Wizara kuhusu fungu 96, ukurasa wa 27 serikali imetenga sh milioni 400 kwa
ajili ya makocha wa kigeni,” alihoji.
Akizungumzia viwanja vya michezo, Mbilinyi alisema wanapendekeza vile vinavyomilikiwa na CCM virejeshwe serikalini vitumiwe na wananchi wote bila kujali itikadi lakini pia hatua hiyo ni baada ya chama hicho kushindwa kuviendeleza.
Alisema, hiyo imevifanya viwanja hivyo kukosa hadhi ya kutumika kwenye mashindano ya kimataifa.
Katika sekta ya utamaduni, kambi ya upinzani imeitaka serikali kuweka msimamo wake wazi kuhusu mashindano ya Big Brother Africa kwani licha ya kuyapinga ikidai hayaendani na tamaduni na mila za kitanzania, bado yanaendelea kuoneshwa na Watanzania wanashiriki.
Mbilinyi pia aligusia kazi za wasanii ambapo licha ya kumpongeza Waziri aliyepita katika wizara hiyo, Dk. Emmanuel Nchimbi kuwa alijitahidi, alisema kuwa pendekezo lao la kuitaka wizara kuunda kikosi kazi kufanya kazi ya kutafiti namna ya kilinda kazi za wasanii nchini, bado inasuasua.
Naye mbunge wa Kinondoni, Idd Azzan (CCM), aliiunga mkono hoja ya Mbilinyi kuhusu viwanja vya CCM akisema kuwa ni licha ya kumilikiwa na chama hicho, bado mapato yanasimamiwa na TFF, hivyo akaitaka serikali kuviendeleza.
Mbunge wa Viti Maalum, Grace Kihwelu (Chadema), katika hilo aliwataka CCM wasione ugumu kwani hatua hiyo itakuza michezo nchini maana chama kimeshindwa kuvihudumia na kuingiza mapato makubwa kwa serikali.
Kuhusu timu ya soka ya Taifa ya wanawake, Twiga Stars, Kihwelu alidai kuwa serikali imekuwa ikionesha upendeleo kwa timu ya wanaume, ‘Taifa Stars,’ hivyo ya wanawake kutembeza bakuli kwa wafadhili licha ya kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa.
“Twiga Stars inahitaji kuhudumia kama Taifa Stars, wachezaji hawa nao wanapaswa kuwekewa bima kama wenzao wanaume ili wakiumia wawe na uhakika wa matibabu lakini vile vile wanapaswa kulazwa mahali pazuri na kulishwa chakula kizuri,” alisema.
No comments:
Post a Comment